Putin atua Ujerumani kusaka amani ya Libya

Muktasari:

Ni baada ya mbabe wa kivita anayeongoza vikosi vya jeshi Mashariki ya Libya, Khalifa Haftar kuondoka mjini Moscow, Urusi bila kutia saini mkataba wa kusitisha mapigano.

Berlin. Rais wa Urusi, Vladimir Putin anatarajiwa kuhudhuria mkutano wa kimataifa kuhusu mchakato wa kutafuta amani nchini Libya.

Taarifa ya ikulu ya Kremlin nchini Urusi ilisema kuwa mkutano huo unatarajiwa kufanyika kesho mjini Berlin, Ujerumani.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, mkutano huo ulioandaliwa na Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel, utaleta matumaini mapya baada ya mazungumzo ya awali ya amani kuhusu Libya yaliyofanyika mjini Moscow, Urusi kugonga mwamba.

Inaelezwa kuwa mkutano huo unalenga kuimarisha makubaliano ya kusitisha mapigano baina ya pande hasimu nchini Libya yaliyofikiwa wiki iliyopita.

Kwa mujibu wa nyaraka za Umoja wa Mataifa (UN), mkutano huo unatarajiwa kufikia makubaliano ya kusitisha moja kwa moja mapigano nchini Libya na utekelezaji wa marafuku ya kuingiza silaha kwenye Taifa hilo la Afrika Kaskazini.

Alhamisi iliyopita mbabe wa kivita anayeongoza vikosi vya jeshi Mashariki ya Libya, Khalifa Haftar aliondoka mjini Moscow, Urusi bila kutia saini mkataba wa kusitisha mapigano.