Rais Tshisekedi, Museveni wakubaliana kukuza biashara

Muktasari:

Viongozi hao wamekubaliana kujenga barabara na madaraja yatakayounganisha mataifa hayo mawili kwa shabaha za kibiashara, ustawi wa jamii na ulinzi.

Kampala, Uganda. Rais Felix Tshisekedi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) amekutana na mwenzie wa Uganda, Yoweri Mseveni kwa lengo la kukuza biashara baina ya mataifa hayo mawili jirani.

Ziara hiyo ya kikazi inakuja siku chache baada ya Rwanda kufunga mipaka yake kwa nchi ya Uganda.

Wakizungumza katika mkutano mjini Kampala jana Rais Mseveni alisema mataifa hayo mawili yatajenga ushirikiano madhubuti.

Aliongeza kuwa kwa kuanza watajenga barabara na madaraja yatakayounganisha mataifa hayo mawili, akisisitiza kuwa hatua hiyo ina shabaha za kibiashara, ustawi wa jamii na ulinzi.

Biashara kati ya mataifa hayo mawili kwa mwaka uliopita ilifikia thamani ya dola milioni 513 lakini kwa sasa kuna ishara ya kuongezeka baada ya Uganda kuelekeza zingatio lake nchini Congo.

Rwanda ilitangaza kufunga mipaka yake mwezi Februari mwaka huu.

Rais Museveni na Tshisdekedi wamekubaliana pia kujenga barabara ya umbali wa kilometa 1,200 kuanzia Uganda kuelekea katika miji mitatu ya eneo la Mashariki mwa Congo ya Goma, Bunia na Beni.

Rais wa Kongo Felix Tshisekedi yuko nchini Uganda kwa ziara ya kiserikali ya siku tatu  kwa mwaliko wa Rais Museveni ambako alipokelewa katika katika Uwanja wa Ndege wa Entebbe na mwenyeji wake.

Katika ziara hiyo Rais Tshisekedi pia anatarajiwa kuhudhuria mkutano wa kilele wa kwanza wa Uganda katika Hoteli ya Imperial Golf View iliyopo Entebbe.