Unido waja na majiko mbadala wa mkaa, kaya 110,000 zanufaika

Muktasari:

Kaya 110,000 za jijini la Dar es Salaam mbioni kuondokana na matumizi ya kuni na mkaa kutokana na kuanza kutumia majiko yanayotumia mafuta ya ethanol yanayotajwa kuwa salama na rafiki wa mazingira.

Dar es Salaam. Kaya 110,000 za jijini la Dar es Salaam mbioni kuondokana na matumizi ya kuni na mkaa kutokana na kuanza kutumia majiko yanayotumia mafuta ya ethanol yanayotajwa kuwa salama na rafiki wa mazingira.

Mafuta hayo yanatengenezwa kwa kutumia mabaki ya miwa baada ya kutengeneza sukari.

Akizungumza leo Jumatano Februari 19, 2020 katika mkutano uliowakutanisha viongozi mbalimbali wa kata za jijini Dar es Salaam, mratibu wa Nishati na Mazingira wa  Shirika la Umoja wa mataifa linaloshughulikia Maendeleo ya Viwanda (Unido), Victor Akim amesema uamuzi huo umefikiwa ili kuenda sambamba na malengo ya kupunguza kasi ya matumizi ya kuni na mkaa.

“Dar es Salaam ni Mkoa unaoongoza kwa matumizi ya kuni na mkaa ndio maana tumelenga sana soko hili kwa kuwapatia nishati mbadala ambayo kila mtu anaweza kuimudu.”

“Majiko hayo 110,000 ni katika awamu ya kwanza ya majaribio iliyoanza Novemba 2019 na itafanyika kwa miezi 18,” amesema Akim.

Amesema awamu hiyo ya kwanza itafanyika katika kata 20 za wilaya ya Ilala na baadaye mradi utaendelea katika wilaya nyingine.

Akizungumzia upatikanaji wa majiko hayo, mkurugenzi mtendaji wa kampuni ya Consumer’s Choice Limited, Frida Mlingi amesema wanunuaji wa majiko hayo hupewa ruzuku ya dola 7 za kimarekani katika jiko huku ununuaji wake ukiwekewa utaratibu maalumu.

“Ili mtu apate jiko anatakiwa kujaza  fomu kwa kiongozi wa mtaa wake na kuweka kifurushi anachohitaji, tunaposema kifurushi ina maana inakuwa ni jumla ya bei ya jiko pamoja na mafuta ya kuanzia.”

“Tuna vifurushi aina tofauti ambavyo huanzia kati ya Sh51,000 hadi Sh114,000 kila kifurushi huwa na lita mbili za mafuta za kuanzia,” amesema Frida.