Viongozi G7 wahaha kunusuru moto misitu ya Amazon

Muktasari:

  • Viongozi hao wanakutana nchini Ufaransa pamoja na mambo mengine wamejadili ni kwa jinsi gani Brazil inapaswa kupatiwa msaada wa haraka.

Biarritz, Ufaransa. Viongozi wa mataifa saba yenye uchumi mkubwa wa viwanda dunia (G7) wamekubalina kutoa msaada wa hali na mali ili kuthibiti moto unaoendelekea kwenye msitu wa Amazon.

Mkutano huo unaoendelea katika mji wa Biarritz nchini Ufaransa pamoja na mambo mengine umejadili ni kwa jinsi gani Taifa hilo la Brazil linapaswa kupatiwa msaada wa haraka.

Mwenyeji wa mkutano huo, Rais Emmanuel Macron aliwaambia waandishi wa habari kwamba viongozi hao wanaendelea kuwasilana na mataifa yote ambayo yamezungukwa na misiti hiyo ili kujua ni ahadi gani ya msaada wa kiufundi na kifedha watoe.

"Urejeshaji wa misitu hiyo ni muhimu lakini pia kulikuwa na mitazamo tofauti ya viongozi wa G7, kwani yote yanategemeana na mataifa yenyewe na Amazonia ambayo yana mamlaka ya kisiasa kwenye eneo hilo,” alisisitiza Rais Macron.

Hata hivyo, Rais Marcon alisema kutokana na umuhimu wa misitu hiyo kwa maisha ya viumbe mbalimbali, hewa ya oksijini na vita dhidi ya kupanda kiwango cha joto ulimwenguni lazima jitihaza za kuuotesha upya msitu huo zifanyike.

Misitu ya Amazon inapatika kwa asilimia 60 nchini Brazil na asilimia 40 inapita katika mataifa manane. Mataifa hayo ni Bolivia, Colombia, Ecuador, Guiana ya Ufaransa, Guyana, Peru, Suriname na Venezuela.

Awali Rais wa Brazil, Jair Bolsonaro alilaani vikali hatua ya viongozi hao wa G7 kuweka ajenda ya misitu hiyo katika mkutano huo akisema kuwa ni uingiliaji kati wa mataifa ya kigeni katika mambo ya ndani ya nchi yake.

Kiongozi huyo wa siasa kali za mrengo wa kulia alikiita kitendo hicho cha ni akili ya kikoloni.

Katika hatua nyengine, Rais Macron alikanusha madai kwamba mataifa hayo ya G7 yalikuwa yamempa mamlaka ya kufanya mazungumzo na Iran kwa niaba ya kundi hilo linalotambuliwa kwamba ni nchi zenye demokrasia ya hali ya juu ulimwenguni.

“G7 ni klabu isiyo rasmi, hakuna kitu kama mamlaka rasmi ambayo mtu mmoja humpa mwengine,” alisema Rais huyo.

Rais huyo alisema badala yake agesaka njia za kuzungumza na Iran kwa niaba ya Ufaransa na kwa kuzingatia majadiliano yake na mataifa ya Magharibi na Japan.