Waziri wa afya aambukizwa virus vya corona

Thursday February 27 2020

 

Tehran. Iran. Naibu Waziri wa Afya nchini Iran, Iraj Haririch ameambukizwa virusi vya corona.

Kwa mujibu wa ripoti za vyombo mbalimbali vya habari vya kimataifa, naibu waziri huyo amegundulika kuwa na maambukizi ya virusi hivyo baada ya kuonyesha dalili za homa kali na kufanyiwa vipimo.

Imeelezwa kuwa waziri huyo kwa sasa ametengwa katika eneo maalum akiendelea na matibabu chini ya uangalizi.

Taarifa zinasema kuwa mpaka sasa ugonjwa huo umeua watu 16 nchini humo huku idadi ya maambukizi ikiongezeka kwa kasi.

“Watu 95 wameambukizwa virusi hivyo mpaka sasa huku idadi ya visa vipya ikiongezeka siku hadi siku,” ilisema taarifa ya wizara ya afya ya nchi hiyo.

Iran ni miongoni mwa nchi ambazo ziko hatarini katika maambukizi ya virusi vya ugonjwa huo ambao unasambaa kwa kasi katika nchi mbalimbali duniani.

Advertisement

Watu zaidi ya 2,700 wamefariki kutokana na ugonjwa huo mpaka sasa huku kukiwa na watu zaidi ya 80,200 wenye maambukizi ya ugonjwa huo ulioanza miezi mitatu iliyopita.

Katika hatua nyingine, Wizara ya Afya ya Algeria imethibitisha maambukizi ya virusi vya corona kuingia katika taifa hilo.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, wizara hiyo imepokea kisa cha kwanza cha mgonjwa wa corona jana.

Wazri wa Afya Algeria, Abdel Rahman Ben Bouzid alisema mgonjwa huyo mwanaume raia wa Italia aliwasili nchini humo Februari 17.

Shirika la Habari la Reuters lilisema kwa sasa mgonjwa huyo ametengwa katika eneo maalum ili kuzuia maambukizi kusambaa.

Algeria imekuwa nchi ya pili barani Afrika kuthibitisha kupata virusi vya corona. Nchi ya kwanza ni Misri.

Hata hivyo, mgonjwa huyo aliyepatikana nchini humo alitibiwa na kupona kabisa.

Wakati huo huo, visa vipya 95 vya ugonjwa wa corona vimeripotiwa nchini Iran.

Kufuatia hali hiyo, Shirika la Afya Duniani (WHO), limeonya serikali za nchi mbalimbali duniani kujiandaa kwa uwezekano wa virusi vya corona kusambaa.

Kwa mujibu wa shirika hilo, maambukizi ya ugonjwa huo sasa yanasambaa kwa urahisi kutoka kwa mtu mmoja hadi mwingine katika maeneo mengi duniani tofauti na awali.

Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo, Dk Tedross Adhamo Ghebreyesus alisema kwa sasa ugonjwa huo unaonyesha kupungua nchini China lakini kasi ya maambukizi inazidi katika mataifa mengine duniani ukilinganisha na awali.

Advertisement