Bashiru awataja tena wenyeviti wa mashina CCM

Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk Bashiru Ally

Muktasari:

Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk Bashiru Ally  amesema anawapa kipaumbele wenyeviti wa mashina katika huduma kutokana na kazi wanazozifanya katika chama hicho kutokuwa na malipo.

Dodoma. Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk Bashiru Ally  amesema anawapa kipaumbele wenyeviti wa mashina katika huduma kutokana na kazi wanazozifanya katika chama hicho kutokuwa na malipo.

Akizungumza katika uzinduzi wa Uhuru ya Kijani leo Alhamisi Septemba 12, 2019 mjini  Dodoma, Dk Bashiru alirejea kauli yake kuwa wenyeviti wa mashina wasipange foleni katika maeneo wanayohitaji huduma kwa kuwa wao ndio chimbuko na msingi katika usimamizi wa shughuli za chama, wanajitolea.

“Nasisitiza, wenyeviti wetu wa mashine na mabalozi wanafanya vizuri huko mashinani, marufuku kwa kiongozi yeyote wa serikali kumzimia au kuacha kupokea simu ya kiongozi wa shina, hata wakipiga saa nane za usiku pokea simu zao,” amesema Dk Bashiru.

Amesema tofauti na nafasi nyingine, viongozi hao wanafanya kazi ya kujitolea moja kwa moja katika maeneo ambako wapo wanachama wa chama hicho tawala.

Amesema katika uchaguzi wa serikali za mitaa, mabalozi na wajumbe wa mashina ndio wataumia zaidi  kuwanadi na kuwashawishi wagombea kujitokeza.