Chadema yaahidi kuheshimu utu, uraia na faragha

Muktasari:

Mwalimu alisema hayo jana wakati wa kampeni zake katika majimbo ya Kigoma Kusini na Kasulu na kusisitiza kuwa Serikali lazima iheshimu uraia wa watu wake kwa kuwa hawakuchagua kwenyewe kuwa mpakani bali ni mipango ya Mungu.

Kigoma. Mgombea mwenza wa Chadema, Salum Mwalimu amesema serikali ya chama chake itaheshimu utu na faragha ya wananchi na katika utawala wao hakuna raia wa mpakani atakayehojiwa kuhusu uraia wake, huku hati ya kusafiria ikiwa ni haki ya kila mwananchi na kwamba itapatikana wakati wowote.

Mwalimu alisema hayo jana wakati wa kampeni zake katika majimbo ya Kigoma Kusini na Kasulu na kusisitiza kuwa Serikali lazima iheshimu uraia wa watu wake kwa kuwa hawakuchagua kwenyewe kuwa mpakani bali ni mipango ya Mungu.

“Watu wa Kigoma hamjajiumba kuwa karibu na Congo na Burundi; ni mipango ya Mungu na lazima Serikali iheshimu, kuwa mpakani haiwezi kuwa sababu ya manyanyaso na tabu, lazima raia wa mpakani wawe huru na kufurahia sawa na wale wa maeneo mengine,” alisema Mwalimu.

Alisema Tanzania inahitaji serikali inayotambua watu wake, kuwalinda na kuheshimu uraia wao kwa gharama yoyote ile na sio kuwasumbua usiku na mchana kuwajaza hofu, huku akiongeza kuwa kama Serikali ya sasa inaona watu wa Kigoma sio raia, basi iwapeleke inakodhani ndiyo kwao.

“Mtu umezaliwa Kigoma, baba ni Kigoma, babu ni Kigoma, lakini mtu anakuja anakwambia wewe sio raia kisa umelalamika hakuna maji safi, wewe ni mfanyabiashara umelalamika kodi inaua biashara au unaishangilia Chadema,” alisema Mwalimu alipozungumza na wakazi wa Kigoma Kusini.

Aidha, Mwalimu alisema Chadema itatoa fursa kwa wananchi kufanya biashara kwa uhuru na nchi nyingine bila vikwazo tofauti na miaka mitano iliyopita ambapo wakulima walilazimishwa mahali pa kuuza.

Kuhusu elimu, alisema sera ya elimu bure ni ya chama chao, lakini inatekelezwa tofauti kwani hivi sasa kinachofanyika ni elimu bila malipo.

“Sera ya Elimu Bure ni ya Chadema CCM hawakuwa nayo huko nyuma waliichukua kwetu lakini sisi hatukumaanisha kuondoa ada ya Sh20,000 na kuacha michango mingi kwa wazazi,” alisema Mwalimu wakati aliposimama kuwasalimia wananchi wa Uvinza.

Alisema Sera ya elimu bure ya Chadema ni kutoa elimu bora bila malipo, watoto wasome katika madarasa mazuri, miundombinu mizuri na walimu wapo kiasi kwamba mtoto anafuraha kwenda shule.

“Sisi tunasema elimu bora sio bora elimu, elimu sio kutoa ada tu bali na kuhakikisha miundombinu na waalimu wanakuwepo. Tukifanya mchezo na elimu yetu Taifa letu litadidimia,” alisema Mwalimu.

Mwalimu aliongeza kuwa Chadema ikishinda dola itabadili mfumo wa elimu nchini ili kuruhusu mtoto kuchagua fani anayoitaka kuanzia elimu ya msingi sanjari na kuongeza elimu ya ujasirimali ili hata anayemaliza darasa la saba aweze kujiajiri.

Aidha, Mwalimu amewasihi wananchi kufanya maamzi sahihi katika uchaguzi huu kwakuwa ndani ya miaka mitano iliyopita Watanzania wakiwemo wa Mkoa wa Kigoma wameishi maisha magumu lakini wakiichagua Chadema maisha yao yatabadilika katika nyanja tofauti za biashara, kilimo na uhuru wa raia na haki zao.