Chadema yaita wagombea uchaguzi mkuu 2020

Kaimu Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana. Kushoto ni Mbunge wa Tarime vijijini, John Heche na kulia ni Mkurugenzi wa Itikadi Mawasiliano na Mambo ya Nje, John Mrema. Picha na Ericky Boniphace

Dar/Mwanza. Harakati za uchaguzi mkuu zimeanza kushika kasi baada ya Chadema kuwataka wanachama wake wanaotaka kuwania udiwani, ubunge au urais kuandika barua za kuonyesha nia.

Chadema imetangaza hatua hiyo ikiwa imebaki miezi takribani kumi kabla ya kufanyika kwa uchaguzi huo unaohusiosha nafasi za urais, ubunge, udiwani na uwakilishi visiwani Zanzibar.

Wito huo umekuja siku chache baada ya CCM kuitisha kikao cha viongozi wa wilaya, mkoa na wa jumuiya zake ambacho mwenyekiti wake. John Magufuli alikitumia kuwataka waanze kujipanga kwa uchaguzi mkuu, huku akiwaonya kuwa upinzani umebadilika.

Chama kingine kinachoonekana kuanza kutekeleza mikakati ya maandalizi ni ACT_Wazalendo ambayo inazungukia wanachama na wadau wengine kuomba maoni ya kujumuisha katika ilani yake ya 2020.

Jana, Chadema ilisema itakuwa na mgombea urais anayekubalika na atakayeshinda ili kuleta mabadiliko ya kweli ya kidemokrasia na maendeleo yanayotarajiwa na wananchi.

“Katika hatua ya sasa nitoe wito si tu kwa wenye dhamira ya kugombea urais, wanaotaka kugombea udiwani, ubunge, popote pale katika maeneo ya nchi yetu wajitokeze kwa kuandika barua za kuonyesha nia,” alisema John Mnyika, katibu mkuu wa Chadema alipokuwa akizungumza katika mahojiano maalum na kituo cha televisheni cha ITV

“Tunataka kufanya mkakati thabiti wa kuwaandaa watu wetu kwa mabadiliko, na kati ya watu tunaowaandaa ni wagombea. Lazima tuwafundishe misingi ya chama, falsafa, itikadi ya chama ili ukiingia kwenye uongozi uwe kiongozi wa tofauti.

Baadaye, Mnyika aliiambia Mwananchi kuwa “kwa wale wanaotaka kugombea ubunge, barua watazindika kwa katibu mkuu kupitia kanda zao na wa udiwani watazindika kwa katibu wa wilaya kupitia kata zao”.

Lakini Mwananchi ilipotaka kujua mafunzo hayo yatatolewa kwa mfumo upi, Mnyika alisema “huwezi kuweka hadharani mbinu zote, hata Rais Magufuli hivi karibuni amesema upinzani unaimarika, unapanga mikakati ya hadharani na sirini, sasa na sisi tunaendelea na mikakati”.

Akijibu swali kama hatua hiyo haitavuruga majimbo na kata wanazoziongoza kwa sasa, Mnyika alisema ndiyo maana wamewataka waandike barua.

“Wasitangaze huko kwenye mitandao na magazeti, waandike kwa chama,” alisema katibu huyo wa Chadema ambayo iliingiza wabunge takriban 100 katika uchaguzi mkuu wa 2015.

“Kisha tutatoa maelekezo ya nini cha kufanya kwenye majimbo na kata tunazoziongoza na maeneo ambayo hatuongozi.

“Hii itasaidia kuepusha mipasuko ndani ya chama na kuendelea umoja wetu, utu wetu na nguzo ya ushindi na ndiyo maana tumewataka waandike mapema hizo barua na tutatoa utaratibu wa mwisho utakuwa lini, kikubwa waanze sasa.”

Akigusia nafasi ya urais, Mnyika alisema hata kama hawatajitokeza watu watakaoonyesha nia ya kuwania urais, kazi hiyo inaweza kufanywa na kamati kuu ya chama hicho kisha ikapata jina la mgombea ambaye anakubalika.

“Mimi ni msimamizi wa uchaguzi na uteuzi wa mgombea ni sehemu ya uchaguzi. Naomba kwa sasa nisiseme chama kinalenga kumsimamisha nani kugombea urais na katiba ya chama chetu inasema kamati kuu ndiyo yenye mamlaka ya kutafiti jina la mgombea urais,” alisema mbunge huyo wa Kibamba akijibu swali za tetesi kwamba Tundu Lissu anaweza kupewa nafasi hiyo.

Chadema ni moja ya vyama vilivyopata wafuasi wengi kabla ya uchaguzi wa 2015 na baadhi yao wakapewa nafasi za kugombea na kushinda ubunge na udiwani, lakini kikakumbwa na hamahama iliyohusisha wanachama wengi waliokumbwa na wimbi hilo.

Lakini Mnyika alisema safari hii wameamua kudhibiti hali hiyo.

“Ndiyo maana tumeamua kutangaza mapema ili tupate wagombea walioandaliwa, wanaojua falsafa, itikadi na wawe wanachama waaminifu kwa chama,” alisema.

Mbowe na maridhiano

Kuhusu haja ya kuwa na maridhiano ya kitaifa miongoni mwa wanasiasa na viongozi iliyoelezwa na jijini Mwanza na mwenyekiti Chadema, Freeman Mbowe siku ya maadhimisho ya miaka 58 ya Uhuru wa Tanganyika, Mnyika alisema huo ndio msimamo wa chama hicho unaobeba kauli mbiu ya “No Hate, No Fear” inayolenga kujenga nchi ya amani, upendo haki kwa wote.

“Maendeleo na demokrasia ni mapacha wanaoenda pamoja. 2020 ni mwaka wa mabadiliko yanayolenga kuwaunganisha Watanzania bila kujali tofauti zao. Tunataka tujenge jamii inayoishi kwa upendo,” alisema Mnyika.

Kutekeleza hilo, Mnyika alisema Mbowe anatarajiwa kutangaza hatua ya pili ya mwelekeo wa kufanikisha maridhiano hayo.

“Kila kitu kitaamuliwa kulingana na wakati na mahitaji,” alisema.

Alisema licha ya zuio la mikutano ya hadhara, Chadema imetumia mkakati wa kujijenga kwa kutafuna chini kwa chini, kama mchwa, kuanzia ngazi ya msingi katika mkakati wa wao wa “Chadema ni msingi”.