VIDEO: Chadema yaitisha vikao vya dharura kuenguliwa wagombea wao serikali za mitaa kila kona

Muktasari:

Chadema yaitisha vikao vya dharura kujadili mwenendo wa uchaguzi wa Serikali za Mitaa, yasema hali ni mbaya na wagombea wao wanazidi kuenguliwa katika mikoa mbalimbali.

Dar es Salaam. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) nchini Tanzania, kimeitisha vikao vya dharura kwa ajili ya kujadili hujumu na kasoro zinazoendelea kujitokeza katika mchakato wa uchaguzi wa Serikali za Mitaa.

Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano, Uenezi na Mambo ya Nje wa chama hicho, John Mrema amesema wamefikia hatua kutokana na vitendo vya hujuma kuendelea hasa kushamiri kwa hatua ya  wagombea wa chama hicho kuenguliwa katika mikoa mbalimbali nchini.

Mrema ameyasema hayo leo Jumanne Novemba 5, 2019 alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mwenendo wa uchaguzi huo na namna wagombea wa upinzani hasa wa Chadema wanavyopata misukosuko kwenye mchakato katika hatua ya kuchukua fomu na kurejesha.

Uchaguzi wa Serikali za Mitaa utafanyika a Novemba 24, mwaka huu.

“Hadi sasa tunazungumza hapa, wagombea wote wa Chadema Mkoa wa Simiyu, Wilaya ya Ngala (Kagera), Jimbo la Ubungo (Dar es Salaam), Jimbo la Mbeya Mjini na Busokelo wote  na maeneo mengine wameondolewa. Wanaenguliwa na wasimamizi hawatoi sababu licha ya kanuni kuwataka kufanya hivyo.

“Tunajiuliza hivi  mitaa 192 yote yaani hajakosekana hata mgombea  mmoja hata wale waliokuwa wenyeviti wakaamua kugombea tena, wameshindwa kujaza fomu? Mkoa wa Katavi majimbo ya Kavuu, Nsimbo na Tanganyika wagombea wote wameanguliwa,” amedai Mrema.

Amesema kutokana na hali hiyo, Chadema kimeitisha vikao hivyo vitakavyoanza kesho kujadili mwenendo huo na kutoa msimamo wa chama na hatua watakazozichukua kutokana na sintofahamu hiyo.

“Hali hii ya wagombea wa upinzani kuenguliwa ipo nchi nzima, siyo dalili nzuri  kwa Taifa tunamuomba Rais John Magufuli aingilie kati,” amesema Mrema.

Kwa mujibu wa Mrema, kabla ya vikao hivyo kufanyika leo jioni viongozi wakuu wakiongozwa na mwenyekiti wa Chadema Freeman  Mbowe watakutana kwa ajili kushauriana hatua za awali za kuchukua.