Chadema yaja na mambo mapya

Mweyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe akionyesha picha ya  Mbunge wa zamani wa Singida Mashariki, Tundu Lissu kwenye simu alipokuwa anazungumza kwa njia ya mtandao wakati wa mkutano mkuu wa chama hicho uliofanyika jijini Dar es Salaam jana.

Dar es Salaam. Wajumbe wa mkutano mkuu wa Chadema wamekesha hadi usiku wa manani kupanga safu ya uongozi wa chama chao kwa miaka mitano ijayo na wakatumia nafasi hiyo kupitisha mikakati mipya.

Nafasi zilizokuwa zikiwaniwa ni pamoja na mwenyekiti na makamu wake wawili kwa upande wa Tanzania Bara na visiwani.

Freeman Mbowe alikuwa na nafasi kubwa ya kushinda na kutetea nafasi ya mwenyekiti dhidi ya Mbunge wa Ndanda, Cecil Mwambe.

Aliyekuwa mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu alikuwa anatazamiwa kutwaa nafasi ya makamu mwenyekiti upande wa Bara dhidi ya Sophia Mwakagenda. Matokeo tofauti na hayo yangekuwa ni miujiza kama ya soka.

Issa Mohamed Issa aliyekuwa mgombea pekee wa nafasi ya makamu mwenyekiti kwa upande wa Zanzibar alikuwa na nafasi kubwa ya kushinda katika uchaguzi huo ambao umekwenda mpaka usiku mzito.

Mchakato huo wa uchaguzi ulianza jana usiku kwenye ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam baada ya mkutano mkuu kuanza mapema saa tatu asubuhi.

Hata hivyo, pamoja na uchaguzi huo kulikuwa kuna mambo ya kusisimua yaliyotokea kwenye mkutano huo siku nzima ya jana mchana .

Mbowe alitumia mkutano huo kufichua jinsi maisha yake ya gerezeni yalivyomsaidia kubuni mikakati ya kuimarisha chama hicho.

Naye Lissu aliwasisimua wajumbe wa mkutano mkuu wa chama hicho kwa hotuba yake aliyotoa kwa mtandao wa kijamii wa WhatsApp kutoka Ubelgiji.

Siri ya Chadema msingi na Segerea

Mbowe, ambaye alikabidhiwa tuzo na chama hicho, alitumia nafasi hiyo kuelezea namna alivyobuni sera ya Chadema msingi ambayo imeleta wanachama wanaodaiwa kuwa zaidi ya milioni sita.

Chama hicho kilizindua sera hiyo ya ‘Chadema msingi’ kama mbinu ya kuvuta wanachama kwa njia ya kidigitali baada ya Mbowe kutoka mahabusu Machi mwaka huu akiwa amekaa gerezani karibu miezi minne.

Siku 104 alizokaa mahabusu ya gereza la Segerea zilitafsiriwa na wanachama wa Chadema na wapigania demokrasia kama mateso dhidi ya viongozi wa upinzani.

Ni kipindi ambacho Mbowe akiwa mwenyekiti wa Chadema alikosa fursa za kushiriki vikao na shughuli zingine binafsi na za chama, hata hivyo jana kiongozi huyo alisema alitumia nafasi hiyo kutafakari jinsi ya kusonga mbele katika harakati za kisiasa.

Mbowe alisema Chadema msingi ambayo ina lengo la kuwasajili wanachama wapya kuanzia ngazi ya chini, aliipata akiwa gereza la Segerea baada ya kusoma kitabu cha mwanazuoni aliyeandikia taasisi ya NDI, Jean Sharp kinachoitwa `From dictatorship to democracy; how to fight dictatorship’.

Mbowe na mbunge wa Tarime Mjini, Esther Matiko walikaa Segerea kuanzia Novemba 23 mwaka jana hadi Machi 7, baada ya Mahakama Kuu kuwapa dhamana iliyokuwa imefutwa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Wawili hao walifutiwa dhamana na Mahakama ya Kisutu kwa madai ya kukiuka masharti ya dhamana katika kesi inayowakabili viongozi tisa wa Chadema.

Akizungumzia tuzo aliyopewa ya ufanyakazi kazi bora kutoka kwa mkurugenzi wa Operesheni na Mafunzo wa chama hicho, Benson Kigaila, Mbowe alisema, “tuzo hii sistahili kuipokea mimi, nilitimiza wajibu wangu kama kiongozi.”

“Mwaka 2016 baada tu ya uongozi wa awamu ya tano kuingia madarakani, tulikuwa katika shambulizi kubwa sana. Baada ya shambulizi kulifuatiwa na chaguzi ndogondogo za ajabu ajabu, chama chetu kilipooza kama vyama vingine,” alisema Mbowe huku wajumbe zaidi ya 1,300 wakimsikiliza

“Wakati chama kikipooza, kama kiongozi mkuu lazima uonyeshe `solution’ (suluhisho). Haikuwa kazi nyepesi. Chama ambacho kilikuwa na wanachama wanakipenda wakaogopa hata kuvaa fulana za chama. Kombati zetu zikakaa kabatini.”

Alisema hali ilikuwa mbaya baada ya mikutano ya hadhara kuzuiwa, mikutano ya Bunge ilipozuiliwa kurushwa moja kwa moja na wabunge wa upinzani kunyanyaswa kwa kufukuzwa huku aliyekuwa mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu akishambuliwa kwa risasi.

“Kama kiongozi mkuu, nilipata wakati mgumu sana. Wapo viongozi wenzangu waliokuwa wakinijia wakilaumiana, yaani ikawa sasa ni chama tunalaumiana ndani ya chama,” alisema.

Alisema licha ya kikao cha Baraza Kuu kilichofanyika baada ya Pasaka ya mwaka 2016 kuamua wafanye uchaguzi, ilishindikana baada ya baadhi ya viongozi kugoma wakitaka kwanza walipwe.

“Tukaenda kwenye uchaguzi mdogo wa Kinondoni, maumivu yakaendelea. Yaliyotokea mnayajua na kesho (leo) tunakwenda mahakamani. Pasaka ya mwaka jana, mimi na watuhumiwa wenzangu tukawekwa ndani. Kwa hiyo kipindi chote cha Pasaka tukakitumia jela ya Segerea,” alisema.

Mbowe alisema, “kipindi kile ndiyo nilipata wazo la Chadema ni msingi.”

“Kwamba viongozi wetu wamekufa ganzi tunafanyaje? Nikasoma andiko, kitabu cha mwanazuoni aliyeandikia taasisi ya NDI, Jean Sharp kinaitwa ‘From dictatorship to democracy; how to fight dictatorship’ (kutoka udikteta hadi demokrasia; jinsi ya kupambana na udikteta) Nilisoma nikiwa Segerea na kutafakari sana, nikasema hii lazima tukaifanye.”

Alisema baada ya kutoka gerezani alikutana na viongozi wenzake na kuwaambia azma ya kuanzisha ‘Chadema ni msingi’ kwa kwenda vijijini bila kujali gharama za kazi hiyo.

“Nikasema tunaweza kwenda nchi nzima bila mikutano ya hadhara, tunaweza kwenda nchi nzima bila magari, wakasema haiwezekani.

“Nikawaambia viongozi wangu kama huko chini kuna wananchi wanaishi na sisi tutakwenda kuishi nao. Kama wanalalia virago na sisi tutalalia virago na hili zoezi mimi kama mwenyekiti wa Taifa nitalisimamia mwenyewe bila kufuata mfumo wowote wa kichama,” alisema.

Kutokana na mkakati huo alisema zaidi ya asilimia 70 ya wajumbe wa mkutano mkuu waliohudhuria mkutano huo ulioisha usiku wa kuamkia leo wanatokana na Chadema ni msingi.

“Tulikataa hofu isitutawale, tulikataa fedha isiwe kigezo. Tulikubalika na kuunda mifumo isiyo ya kichama kwa kibali cha kamati kuu.

“Leo napewa tuzo hii sistahili kwa sababu ni wajibu wangu. Nimekwenda mikoa yote. Nilipotoka jela mara ya pili sikwenda Hai (Kilimanjaro) nyumbani, nilikwenda Mtwara na kanda ile ya Kusini mara mbili,” alisema.

Awali, akizungumza wakati wa kumkabidhi tuzo hiyo iliyokabidhiwa na mwenyekiti wa bodi ya wadhamini ya chama hicho, Arcado Ntagazwa, Kigaila alisema ilikuwa ni ya kushtukiza na wala Mbowe hakujua, lakini ililenga kutambua mchango wake wa kukifufua chama kilichokuwa kwenye mateso makubwa na tishio la kufa.

Hawatambui uchaguzi serikali za mitaa

Akizungumza wakati wa kufungua mkutano huo, Mbowe alitangaza msimamo wa chama hicho wa kutotambua uchaguzi wa serikali za mitaa na kutaka uchaguzi huo ufutwe ili ikiwezekana ufanyike pamoja na uchaguzi mkuu mwaka 2020.

“Nikubaliane na mmoja wa viongozi wetu kumtaka Rais aepushe Taifa na yaliyotokea. Wala siyo aibu kukiri aibu. Chaguzi zile zifutwe uwepo utaratibu mwingine wa kufanya uchaguzi katika siku za karibuni. Tupo radhi hata chaguzi hizi zisogezwe mbele tufanye pamoja na uchaguzi mkuu zisimamiwe na tume huru,” alisema.

“Hatuna Tume ya Uchaguzi. Tunahitaji kufanya mazungumzo ili tupate tume huru itakayokuwa na uhalali. Tujifunze kwa wenzetu Kenya,” alisema katika mkutano huo uliohudhuriwa na viongozi mbalimbali wa vyama vya siasa, dini, asasi za kiraia na wanadiplomasia.

Lissu ahutubia akiwa Ubelgiji

Aliyekuwa mbunge wa Singida Mashariki, Lissu aliwasisimua wajumbe wa mkutano mkuu wa Chadema baada ya kutoa hotuba fupi ya moja kwa moja akitumia simu ya video (video call) kwa mtandao wa kijamii wa WhatsApp.

Lissu alionekana katika hali ya ucheshi kwenye televisheni kubwa zilizokuwepo ukumbini akiwa amevalia fulana na kofia ya Chadema baada ya kupigiwa simu na katibu mkuu wa chama hicho, Dk Vincent Mashinji, ambaye baadaye alimwomba Mbowe amkaribishe Lissu.

Lissu aliyeshambuliwa kwa risasi Septemba 7, 2017 akiwa jijini Dodoma na kupelekwa kutibiwa Nairobi nchini Kenya na baadaye Ubelgiji kwa mara ya kwanza alikuwa amepata jukwaa la kuzungumza na wajumbe wa mkutano mkuu wa Chadema tangu akumbwe na mkasa huo.

Mashinji alianza kwa kumsalimia Lissu na kumwomba atoe salamu kwa wajumbe.

Lissu alianza kwa kutoa salamu maarufu ya Chadema, `Peoples’ huku ukumbi mzima ukijibu kwa nguvu `Power’ na baadaye kukisema kibwagizo kipya cha Chadema cha `No hate, no fear’.

Lissu aliwapongeza makada wenzake kwa kujenga chama licha ya changamoto wanazokumbana nazo.

Akiongozwa na Mbowe kuzungumza na wajumbe wa mkutano huo, Lissu alisema “baada ya mateso yote tuliyopata, baada ya bonde la uvuli wa mauti, njia iliyobaki ni kuchukua nchi mwaka ujao. Hakuna walichobakiza, wametufunga, wametujeruhi na kila mateso, leo tuna nguvu zaidi kuliko tulivyokuwa.”

Aliwataka wana Chadema kufanya maandalizi ya kutosha ili ngwe iliyobaki aliyosema siyo ndefu lakini ngumu akieleza ili waweze kurudisha nchi katika kile alichodai misingi ya kuheshimu utu, demokrasia na haki za binadamu.

Kuhusu afya yake, alisema madaktari wake wamesema amepona na yuko tayari kurudi nchini.

“Nipo tayari kurudi nyumbani kuungana na makamanda wengine ili tutengeneze nchi. Naombeni tushirikiane ili niweze kurudi nyumbani haraka na salama. Mbele ni kuzuri kuliko huko tulikotoka,” alisema huku akishangiliwa kwa nguvu na wajumbe wa mkutano huo.

Vyama vingine vyazunguma

Mkutano huo ulihudhuriwa na wageni mbalimbali wakiwamo wawakilishi wa vyama rafiki ambavyo vilipata fursa ya kuzungumza na kumpongeza Mbowe kwa kutoa ombi la kuwapo kwa maridhiano ya kitaifa mbele ya Rais John Magufuli.

Mbowe alitoa kauli hiyo, Desemba 9 katika maadhimisho ya miaka 58 ya Uhuru wa Tanganyika baada ya kupewa nafasi na kiongozi mkuu huyo wa nchi .

Mwenyekiti wa UPDP, Fahmi Dovutwa alianza kwa kusifu mkutano mkuu huo wa Chadema, “mwenyekiti alizungumzia maridhiano akiwa Mwanza kwenye maadhimisho ya siku ya Uhuru. Mimi nasema kwa watu mliopo hapa, endeleeni na kasi yenu.”

Dovutwa alimtaka Mbowe kuendelea kukimbia na chama hicho na kutowasikiliza wasiowatakia mema.

“Kwa mbio mlizopo nadhani mnakaribia Magogoni. Mbowe ana viwango vya kimataifa, kwa mwaka 2020 Chadema ndiyo kinategemewa kutwaa nchi,” aliongeza Dovutwa.

Mkurugenzi wa habari na uhusiano wa umma wa CUF, Abdul Kambaya alisema, “mwenyekiti alizungumzia maridhiano pale Mwanza watu wengine walimkosoa kwenye mitandao hawajui tulipotoka.”

Kambaya aliwataka wajumbe wa mkutano huo kutosikiliza maneno ya watu kwenye mitandao ya kijamii wakati wa kuchagua viongozi bali waangalie utendaji na katiba inasemaje.

Katibu mkuu wa chama cha Kijamii (CCK), Renatus Muabhi aliwataka wajumbe wa chama hicho kumchagua tena Mbowe kwa kuwa ndiye anayefaa.

Mwingine aliyetoa salamu ni katibu mkuu wa NCCR-Mageuzi, Elizabeth Mhagama aliyewataka wajumbe kuchagua viongozi bora kwa ajili ya Taifa.

Wakati mgumu kwa Msajili, Shibuda

Msajili msaidizi wa vyama vya siasa, Sisty Nyahoza na mwenyekiti wa baraza la vyama vya siasa, John Shibuda walikumbana na wakati mgumu wakati wakitoa salamu katika mkutano huo jana.

Minong’ono ya wajumbe wa mkutano huo ilimlazimu Mbowe kuwatuliza baada ya kuanza kupiga kelele na kuzomea.

Katika salamu zake, Nyahoza alisema ofisi yake ni mlezi wa vyama na kuvitaka kutii sheria ya vyama vya siasa na sheria za nchi.

Baada ya kauli hiyo baadhi ya wajumbe waliguna huku wengine wakipiga kelele, `tunataka bendera zetu.’

Bendera za chama hicho zilizokuwa zimewekwa barabara ya Sam Nujoma jijini Dar es Salaam jirani na ukumbi wa Mlimani City unakofanyika mkutano huo ziliondolewa juzi saa 4 usiku na polisi kwa agizo la mkurugenzi wa manispaa ya Ubungo, Beatrice Dominic.

Katika uondoaji wa bendera hizo, Polisi ililazimika kutumia mabomu ya machozi.

Hata hivyo, Beatrice alisema bendera hizo zilizowekwa katika barabara ya Sam Nujoma jijini Dar es Salaam zimeshushwa kwa sababu chama hicho hakikuomba kibali.

Katika maelezo yake, Nyahoza alisema, “hakuna mlezi anayependa mtoto wake asimtii. Hatupendi watoto watukutu.”

Licha kutulizwa, wajumbe hao waliendelea kupiga makofi na kuzomea jambo lililomfanya Nyahoza kukatisha hotuba yake na kwenda kuketi.

Shibuda ambaye ni mwenyekiti wa chama cha Ada-Tadea naye alijikuta katika wakati mgumu baada ya kuzomewa na wajumbe hao alipoanza kuzungumzia alivyopewa nafasi ya kugombea ubunge wa Maswa mwaka 2010.

“Mimi nimetoka katika mseto wa mafiga matatu, kwanza niliwahi kugombea ubunge kupitia chama hiki pili kwa sasa ni mwenyekiti wa Ada-Tadea na tatu ni mwenyekiti wa baraza la vyama vya siasa,” alisema Shibuda.

Aliendelea kueleza kuhusu mfumo wa vyama vingi akisema alishakutana Rais John Magufuli kuzungumzia mfumo wa vyama vingi.

“Siamini kama Rais John Magufuli ana mpango wa kufuta vyama vya siasa bali hapendi kuona lugha za kudhalilishana,” alisema Shibuda na wajumbe hao kuitikia, “hawezi kufuta mfumo wa vyama vingi.”

Shibuda aliwatuliza wajumbe hao akisema, “hamjui nitamalizaje.”

Baada ya kelele kuenea ukumbini, Mbowe alisimama na kwenda alipokuwa amesimama Shibuda kwa lengo la kuwatuliza wajumbe hao, “hata kama hamkufurahishwa na maneno yake, muwe na nidhamu. Nidhamu ni kitu muhimu.”

Kauli hiyo ilileta utulivu katika ukumbi huo na Shibuda alizungumza kwa dakika chache na kumaliza.

Chanzo kipya cha mapato

Katika hotuba yake, Mbowe alitangaza mkakati mpya ya kidigitali utakaokiwezesha chama hicho kukusanya ada ya wanachama itakayofikia Sh15 bilioni kwa mwaka akisema inatosha kukiendesha chama hicho bila ruzuku ya Serikali.

Kwa mujibu wa Mbowe, kwa sasa Chadema inapata ruzuku ya Sh280 milioni kwa mwezi sawa na zaidi ya Sh3 bilioni kwa mwaka.

Mbowe alisema programu hiyo iliyozinduliwa unahusisha uandikishaji wa wanachama kidigitali (membership registration), ufanyaji wa mikutano kidigitali na kampeni.

“Kila mwaka mwanachama anatakiwa alipie Sh1000 ya ada, kwenye vikao hivi tunapendekeza iwe Sh2,500 kwa mwaka. Maana yake ni nini? Leo hii chama kinapata ruzuku ya Sh3 bilioni. Gharama ya kufanya Baraza Kuu na mkutano mkuu ni zaidi ya Sh1 bilioni. Kwa hiyo ruzuku peke yake haitoshi,” alisema Mbowe.

“Kupitia Chadema Digital tuna digita fund raising (harambee ya kidigitali), tumekubaliana kuchangia Sh2,500. Asilimia 90 wana Chadema wana simu za mkononi, kila mwanachama akilipa kwa simu tutapata Sh15 bilioni kwa mwaka,” alisema

“Tunahitaji kujenga chama cha kujitegemea na hili msajili usikie, maana yake kuna watu wanafikiri chama kinategemea sana ruzuku,” amesema.

Akifafanua zaidi, Mbowe amesema kutokaa na mfumo huo, chama hicho sasa hakihitaji tena kufanya mikutano ya hadhara ili kupata wanachama wapya.