China yalaani ubaguzi wa rangi dhidi ya waafrika

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje nchini China, Zhao Lijian

Dar es Salaam. Wizara ya Mambo ya Nje ya China imekemea vitendo vya unyanyasi na ubaguzi dhidi ya waafrika wanaoishi kusini mwa China katika jimbo la Guangdong, na imesema kwamba serikali ya China itaendelea kuhakikisha raia wote wa kigeni wanapatiwa haki sawa nchini humo.

China imesema haya baada ya video na picha kuzagaa kwenye mitandao ya jamii ikiwaonyesha waafrika wengi wakiwa wamezagaa mitaani katika maeneo mbalimbali nchini China wakiwa na mabegi ya nguo wakidai wamefukuzwa kwenye nyumba zao na mahotelini.

Taarifa zaidi zimedai kwamba vitendo hivyo vya kinyume na haki za binadamu vimekuwa vikifanywa na mamlaka za serikali ya China ambazo zinawashutumu raia wa kigeni hususani waafrika kwamba wanasambaza ugonjwa wa corona nchini humo.

“Tunapitia changamoto nyingi kwani tumejifungia ndani kwa takribani miezi mitatu. Changamoto kubwa ni ubaguzi wa rangi kwani imefikia wakati sasa haturuhusiwi kupata huduma za afya katika mahospitali..” alisema mmoja wa waafrika ambaye kwa sasa anaishi nchini China wakati wa mahojiano kupitia televisheni ya nchini Uganda.

Taarifa zaidi zinaeleza kwamba, waafrika wanaoshi nchini China hawaruhusiwi kununua bidhaa kama chakula katika masoko makubwa na pia wanazuiliwa kula katika migahawa nchini humo.

Akijibu tuhuma hizo, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje nchini China, Zhao Lijian, alisema “Tangu mlipuko wa corona, China na nchi za Afrika zimekuwa zikishirikiana kupigana na ugonjwa huu. Hivyo hatuwezi kusahau msaada uliotolewa na nchi za Afrika wakati ambapo tulikuwa tumeathirika zaidi na ugonjwa huu,” alisema msemaji huyo kwenye barua ambayo ilitolewa kwa gazeti la Mwananchi na Ubalozi wa China nchini Tanzania.

Pia, Serikali ya China imeziagiza mamlaka nchini China kuboresha namna zinavyofanya kazi na kuwataka raia wa kigeni wanaoishi nchini humo kuzingatia maelekezo na miongozo ya afya inayotolewa na mamlaka nchini humo kwa lengo la kuzuia maambukizi ya corona ndani na nje ya China.

“Kwa sasa tunafatilia kwa ukaribu kinachoendelea nchi za Afrika. Serikali ya China na watu wake tunajitahidi kufanya kila linalowezekana kusaidia nchi za Afrika kipindi hiki cha mlipuko wa corona,” alisema msemaji huyo.

Lijian pia alisema China imeweka mikakati thabiti kuzuia maambukizi ya corona ndani na nje ya China ambayo ilikuwa nchi ya kwanza kutangaza mlipuko wa ugonjwa wa corona mwezi Desemba mwaka jana.

Kutokana na taarifa za unyanyasaji dhidi ya waafrika nchini China, Balozi wa Tanzania nchini China Mbelwa Kairuki, aliliambia Mwananchi kwamba alikuwa na taarifa hizo na akaongeza kwamba Balozi za Afrika nchini humo zilikuwa zinafuatilia suala hilo kwa ukaribu.

Alipoulizwa kama kuna Mtanzania yeyote nchini humo ambaye aliathirika na vitendo hivyo vya unyanyasaji, Balozi Kairuki alisema kwamba, mpaka kufikia saa 9 usiku, hakukuwa na taarifa zozote zinazoelezwa kwamba kuna Mtanzania aliyefukuzwa kwenye nyumba yake au hotelini. “Ubalozi unafuatilia suala hili kwa ukaribu sana. Tumeshawasiliana na jumuiya ya Watanzania wanaoishi Guangzhou. Taarifa ni kwamba hakuna Mtanzania aliyefukuzwa, wote wanaishi kwenye nyumba zao,” alisema Balozi Kairuki.