Breaking News

Dk Bashiru ataja sifa nne zinazoipa CCM jeuri ya ushindi

Sunday October 18 2020

 

By Jesse Mikofu, Mwananchi

Mwanza. Katibu mkuu wa Chama cha Mpinduzi (CCM), Dk Bashiru Ally amesema chama hicho kina uhakika wa kushinda urais na majimbo ya mjini kutokana na sifa nne zinazowapa jeuri.

Vilevile, Dk Bashiru ametaja malengo makuu matatu ya chama hicho katika uchaguzi huu. Amebainisha hayo jana katika kikao cha ndani alipozungumza na viongozi wa mashina, kata na Wilaya ya Nyamagana katika Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza na kwamba ushindi ni lazima kwa chama hicho.

Sifa ya kwanza inayowabeba alisema ni muundo na historia inayobebwa na moyo wa kujitolea wa wanachama wake.

Sifa nyingine aliyoitaja mtendaji mkuu huyo wa CCM ni kudumisha nidhamu ndani na nje ya chama hicho sifa ambazo hazipo kwa vyama vingine vinavyoshindana kwenye uchaguzi huu.

“Nidhamu ni sifa muhimu sana katika mafanikio ya binadamu, vipo vyama haviheshimiani hata viongozi wao, jeuri yetu sisi ni mshikamano na nguvu yetu vinavyotokana na nidhamu. Udhaifu wa wapinzani wetu ni utovu wa nidhamu,” alisema Dk Bashiru.

Sifa ya tatu aliyoitaja kuwapa ushindi mwaka huu alisema CCM kusimamisha wagombea bora, wenye sifa na waliofundwa kuliko vyama vyote kuanzia ngazi za udiwani, ubunge hadi urais.

Advertisement

Aliitaja sifa ya nne kuwa chama hicho ndicho chenye ilani bora iliyosheheni miradi mikubwa ya kimkakati katika maeneo yote ya nchi hivyo kuwagusa wananchi popote walipo nchini.

Aonya migogoro

Licha ya kujimwagia sifa hizo, Dk Bashiru alisema kuna wakati chama hicho hukumbwa na tofauti na chokochoko kutokana na baadhi ya viongozi na wanachama kuzushiana mambo ya uongo hivyo kukiumiza.

Alisema wapo baadhi ya makada wanaowatuhumu wenzao wakiwasingizia kwamba mchana wanakuwa CCM lakini usiku wanageuka na kuunga vyama vingine bila kuwa na ushihidi wa maneno hayo.

“Tusizushiane na kutoleana tuhuma, wapo baadhi yetu wana tabia hiyo, kufanya hivyo tunakiumiza chama na kukidhoofisha, hakikisha unapomtuhumu mtu kwa kosa la usaliti uwe na ushahidi wa kutosha maana adhabu ya kosa la kukisaliti chama ni kufukuzwa uanachama moja kwa moja ndani ya chama,” alisema

Alisema iwapo kuna watu wanawatuhumu wenzao lazima wawe na ushaidi wa kutosha kuthibitisha tuhuma hizo bila kuacha shaka yoyote na wazipeleke katika mamlaka za nidhamu za chama hicho ili zikashughulikiwe kwa mujibu wa utaratibu uliopo.

Malengo katika uchaguzi huu

Katika kikao hicho Dk Bashiru alibainisha malengo matatu ya CCM katika uchaguzi mkuu huu ikiwa ni pamoja na kuumaliza huku Taifa likiendelea kuwa na amani, mshikamano na upendo zaidi.

Alisema chama hicho kimejiwekea malengo ya kulinda tunu za Taifa ambazo ni uhuru, haki, usawa, muungano na kujitegemea ili zibaki zikimeremeta baada ya uchaguzi.

Pia alizitaka timu za ushindi wahakikishe wanahamasisha watu wajitokeze kwa wingi kupiga kura angalau wasipungue asilimia 90 ya waliojiandikisha wajitokeze kupiga kura na kati yao wengi wakipigie Chama cha Mapinduzi.

Katika kikao hicho Bashiru alisisitiza wagombea na viongozi wengine wa chama kujikita kutoa elimu ya kupiga kura na kujihadhari kutovunja sheria za nchi hata kama wanarushiwa maneno makali na wapinzani wao lakini wasijibu mashambulizi badala yake watoe taarifa kwenye vyombo husika huku wakiendelea kupanga mikakati ya ushindi.

Bashiru ambaye ni mlezi wa Mkoa wa Mwanza yupo kwenye ziara ya siku nne akizungumza na viongozi wa wilaya za Nyamagana, Ilemela na Kwimba katika vikao vya ndani kuweka mikakati ya ushindi.

Advertisement