Hizi ndi sura mbili za Dk Bashiru

Thursday September 05 2019
bashiru pic

Kauli za katibu mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally zinamuweka katika sura mbili tofauti, huku baadhi ya wachambuzi wa siasa wakisema kuna mambo anayoyaamini ambayo yanatofautiana na mtazamo wa chama chake.

Dk Bashiru, ambaye ana zaidi ya mwaka mmoja katika taasisi hiyo tangu alipoteuliwa Mei 2018, amerithi nafasi iliyoachwa wazi na Abdulrahman Kinana aliyestaafu.

Moja ya kauli za Dk Bashiru ni ya hivi karibuni aliyoitoa wakati wa ziara yake ya kufungua mashina kwa Mkoa wa Dar es Salaam.

Katika ziara hiyo Dk Bashiru alionyesha kutotambua uwepo wa umoja wa walimu wa CCM.

Walimu hao waliitisha kongamano lenye lengo la kumpongeza Rais John Magufuli kwa kile walichoeleza kuwa ni kutekeleza ilani ya uchaguzi ya chama hicho na kusema mgeni rasmi angekuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Jenister Mhagama.

Awali katika ziara hiyo, Dk Bashiru aliwapongeza walimu hao akisema amekutana nao na wamekubaliana kushirikiana katika masuala mbalimbali.

Advertisement

“Nawapongeza mlioanzisha shirikisho la makada CCM walimu, wengine nimekutana nao wiki iliyopita, tumezungumza tumepanga kwa hiyo nawapongezeni sana kwa niaba ya shirikisho la walimu makada walioko nchi zima,” alisisitiza.

Lakini wakati akiwa Shule ya Msingi Ubungo Kisiwani, kiongozi huyo aliwabadilikia walimu hao aliposema kuwa walimu ni watumishi wa umma kama wengine, hivyo hawapaswi kushiriki katika siasa waziwazi.

“Sitaki kusikia utambulisho huu, walimu kama wanataka kufanya kazi za kitaaluma waende kwenye vyama vya wafanyakazi, wakija kwenye chama makundi ni hayo. Huji kama mwalimu, unakuja kama mwanaCCM,” alisema Dk Bashiru.

Alisema kuna maadili ya ualimu yanayogongana na uanachama kwa sababu ukiwa darasani unafundisha watoto wa Taifa hili, bila kujali itikadi za wazazi wao na kwamba ukiwa mwalimu unafundisha Taifa zima.

“Mwalimu ni mtumishi wa umma unalipwa na walipakodi ambao ni Watanzania wa vyama vyote. Sasa nasikia kuna upepo mbaya unapita huko, makatibu wa mikoa na wilaya msitambue makundi hayo kwa utambulisho huo. Tambueni makundi ya wanachama wakulima na wafanyakazi,” alisisitiza.

Kauli nyingine tata iliyowahi kutolewa na Dk Bashiru ni pale alipoonekana kuchoshwa na wadhifa wake kiasi cha kutaka kujiuzulu.

Akiwa katika shule hiyo ya Ubungo Kisiwani, Dk Bashiru alisema wadhifa alionao ulikuwa mzigo kwake na ilifikia wakati alitaka kujiuzulu, lakini alipewa moyo na mwenyekiti wa chama hicho, Rais John Magufuli na watu wake wa karibu.

“Nilikejeliwa sana nikaitwa majina ya uonevu wakati mwingine nampigia mwenyekiti (Magufuli) hii kazi uliyonipa vipi,” alisema siku hiyo.

“Mtoto wangu mkubwa alisema kama angekuwa na hiari kuamua kazi inayonifaa angeniambia baba achana na kazi hii (ya ukatibu mkuu), Magufuli alinishauri maana anajua misukosuko ya uongozi.”

Mbali na kauli hiyo, Dk bashiru pia ameonyesha umuhimu wa viongozi kupewa mafunzo ya uongozi huku akiwataja wakuu wa mikoa wawili; Paul Makonda (Dar es Salaam) na Albert Chalamila (Mbeya), kwamba wanatakiwa kupata mafunzo ya uongozi ili wawe bora zaidi.

Si mara ya kwa Dk Bashiru kuyataja majina hayo, akisema wakuu hao watakuwa wanafunzi wa kwanza watakaonufaika na darasa la mafunzo ya uongozi chini ya mpango mpya wa CCM.

Dk Bashiru alisema malengo ya mpango huo ni kuhakikisha vijana wa kizazi cha sasa wanabeba deni la ukombozi wa Afrika dhidi ya wakoloni waliorejea kwa majina mengine.

“Mwenyekiti ameshaelekeza mpango wa kuwaandaa viongozi utekelezwe haraka na walengwa wakubwa ni vijana. Kati ya watakaoanza mafunzo hayo na nimeshawaorodhesha ni Makonda na Chalamila,” alisema Dk Bashiru.

“Tena wa Mbeya ni mwanafunzi wangu wa darasani kabisa. Tunataka kuandaa akina Baba wa Taifa, (Julius) Nyerere wa leo na kesho, akina (muasisi wa Zanzibar, Abeid) Karume akina (Waziri Mkuu wa zamani, Rashid) Kawawa, rais wa zamani wa Afrika Kusini, Nelson) Mandela na (rais wa zamani wa Zimbabwe, Robert) Mugabe.

“Tusipofanya hivyo wakoloni watarudi. Na hawajaondoka, bado wako hapa wanajigeuza majina kwa hiyo vijana katika uongozi wangu mnivumilie.

“Nitakuwa mkali kwenu lakini kwa nia njema. Mna wajibu wa kuishi mapambano ya ukombozi wetu.”

Lakini misimamo hiyo tata imevuta maoni tofauti.

Wachambuzi wamzunguzia

Siyo kwamba CCM ni chama kikubwa kinachoweza kumshinda, ila Dk Bashiru anapata mtanziko kwa sababu kuna mambo anayoyaamini na kuna majukumu anatakiwa kuyasimamia ndani ya chama,” anasema katibu mkuu wa chama cha ACT Wazalendo, Dorothy Semu.

Semu anatoa mfano wa suala la walimu akisema walifanya makosa kujitambulisha kwa chama hicho kwa kuwa ni watumishi wa umma.

“Walimu ni watumishi wa umma na wanaweza kukitumikia chama chochote kilichopo madarakani, kiwe ACT Wazalendo au Chadema au chochote. Kama wanataka siasa, wajitoe kwenye utumishi waende wakatumikie siasa,” anasema Semu.

“Yeye (Dk Bashiru) anaujua ukweli, ndiyo maana anapata shida katika kauli zake. Watumishi siku hizi wanaambiwa wanalipwa mshahara na CCM kwa hiyo lazima wakitumikie chama hicho, wakati si sahihi.”

Hata hivyo, Semu anasema majukumu ya kuwa katibu mkuu yanahitaji uvumilivu na ujasiri kutokana na changamoto za kisiasa wanazokabiliana nazo kila siku.

Akichambua zaidi kauli hizo, mhadhiri wa sayansi ya siasa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Benson Bana anasema anachokifanya Dk Bashiru ni kawaida kwa wanasiasa.

“Mwanasiasa anaweza kutoa kauli moja leo, halafu akaibadilisha kwa kutoa kauli ya pili na ya pili ndiyo kauli sahihi. Inawezekana akatoa kauli ya kwanza kwa kupewa ushauri mbaya,” anasema Dk Bana.

Kuhusu kauli ya kutaka kujiuzulu, Dk Bana anasema “kazi ya kusimamia utendaji wa chama ni ngumu katika mazingira ambayo alibezwa na kutukanwa, lakini anaonekana amekomaa”.

Hata hivyo, Dk Bashiru ambaye ni mwanataaluma wa sayansi ya siasa anasema amekuwa kikitetea chama hicho tangu alipokuwa mwanafunzi na hatimaye kuwa mwanataaluma Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Advertisement