UCHOKOZI WA EDO: Homa ya dengue ni zaidi ya bajeti na Taifa Stars

Tuesday June 25 2019

 

By Edo Kumwembe

Unapoona picha ya Rais wa nchi katika ukurasa wa mbele wa magazeti akienda kutoa pole katika familia iliyopoteza watoto wawili wakubwa ,wasomi wa kiume kwa ugonjwa unaosababishwa na mbu, inafikirisha sana.

Namba Moja ana mambo mengi ya kufanya. Anaweka kando kila kitu na kugonga mlango wa ndugu yetu mmoja kutoa pole kwa kupoteza vijana wawili kwa ugonjwa unaosababishwa na mbu. Ni simanzi. Tumeshindwa vita dhidi ya mbu? Hapana. Tumekwama wapi sasa?

Kitu cha kwanza kabisa ni jinsi ambavyo ugonjwa wenyewe unavyochukuliwa. Kuna kauli za mzaha ndani yake. Rafiki yenu akiumwa unasikia watu wanasema katika vikao vya baa “Ahh kalala zake kapigwa na dengue balaa sisi acha tuendelee kunywa”.

Ni kawaida ya Watanzania kuchukulia kwa umakini mdogo kitu kikubwa. Ndani ya habari ambayo ungedhani ni nzito Watanzania huwa wanaitafutia upande wa pili wa mzaha.

Hata yeye mwenyewe akipona unakuta anaongea kwa mzaha “Ahh imenipiga lakini imenikosa, mhudumu niongeze chupa nyingine”. Anazungumza kama vile alikuwa anaumwa ugonjwa wa kawaida. Chini ya kapeti dengue imeua watu wengi mpaka sasa.

Mpaka sasa hatujajua namna ya kukabiliana na Dengue kikamilifu. Nadhani inatokana na ubinafsi unaotutawala. Hatuoni kama ni janga la kitaifa. Tunaona ni janga la mtu mmoja mmoja. Ingekuwa Ulaya katika nchi ambazo zinajali watu wake nadhani dengue ingekuwa inazungumzwa ‘kijanga’ zaidi kuliko ambavyo tunaizungumza sasa.

Advertisement

Kinachochekesha zaidi ni pale watu wanapojadiliana kuhusu dengue. Huwa wanazungumza zaidi kuhusu matibabu yake. Maji na Panadol. Hawazungumzii kuhusu chanzo chake. Tunatokomeza vipi mbu wa Dengue? Hili linapaswa kuwa suala kubwa kuliko kuzungumzia maji na Panadol.

Kwa nini tusianzishe operesheni ya kutokomeza mbu katika vyanzo vyake. Hofu ni kwamba baada ya kupungua dengue na malaria unaweza kuja ugonjwa mwingine wa mbu huyo huyo. Hatujui utaitwaje na hatujui utatwaa roho ngapi za wenzetu.

Kwa sasa tuko bize na maongezi ya matokeo ya Taifa Stars pamoja na habari ya bajeti. Dengue ni tatizo zaidi ya hayo.

Advertisement