IGP apangua Ma RPC wanne, yumo wa Morogoro

Muktasari:

  • Inspekta Jenerali wa Polisi nchini Tanzania (IGP), Simon Sirro ametangaza mabadiliko ya makamanda wa polisi nchini humo ambayo yameelezwa yanalenga kuboresha ufanisi wa utendaji kazi kwa jeshi hilo.

Dar es Salaam. Inspekta Jenerali wa Polisi nchini Tanzania (IGP), Simon Sirro amefanya mabadiliko madogo ya makamanda wa polisi wa mikoa (RPC).

Akizungumza na Mwananchi leo Jumanne Septemba 17, 2019 Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini humo, David Misime amesema katika mabadiliko hayo Wilbroad Mutafungwa amehamishiwa makao makuu akitoka Morogoro.

Misime amesema nafasi ya Mutafungwa imechukuliwa na Hamisi Issa aliyekuwa Kilimanjaro. 

Amesema Saidi Hamdani aliyekuwa Njombe amehamishiwa Kilimanjaro na Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Geita, Daniel Sillah anakwenda kuwa Kamanda wa Polisi Njombe.

“Mabadiliko haya ni ya kawaida katika kuboresha utendaji kazi wa jeshi la polisi,” amesema Misime

Ingawa Misime amesema mabadiliko hayo ni ya kawaida lakini huenda kwa Kamanda wa Polisi wa Morogoro yamefanyika ikiwa ni utekelezaji wa maagizo ya Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa aliyoyatoa Bungeni jijini Dodoma.

Septemba 13, 2019 wakati akiahirisha mkutano wa 16 wa Bunge la 11 hadi Novemba 3,2019 Bungeni jijini Dodoma, Majaliwa alisema kamati aliyoiunda kuchunguza ajali ya lori la mafuta ya petroli iliyotokea Agosti 10, 2019 mkoani Morogoro imekamilisha shughuli yake.

“Lengo lilikuwa kufahamu chanzo cha ajali, mazingira baada ya ajali na hatua gani zichukuliwe kuzuia matukio kama haya sambamba na kuwawajibisha wale wote ambao hawakutekeleza wajibu wao ipasavyo kabla na baada ya ajali kutokea,” alisema Majaliwa

Katika ajali hiyo, jumla ya watu 104 walipoteza maisha na wengune kujeruhiwa na kusababisha uharibifu wa mali.

Tayari Mkuu wa Jeshi la Zima Moto na Uokoaji nchini Tanzania, Thobias Andengenye naye Septemba 3,2019 alifanya mabadiliko ya makamanda wa zima moto akiwamo wa Morogoro Gilbert Mvungi aliyemwamishia makao makuu na nafasi yake ikichukuliwa na Goodluck Urio.