Idris Sultan ahojiwa polisi, apekuliwa nyumbani kwake

Thursday October 31 2019
idriss picc

Dar es Salaam. Mchekeshaji na mshindi  wa mashindano ya Big Brother 2014, Idris Sultan leo Alhamisi Oktoba 31, 2019 amehojiwa kwa saa tano katika kituo cha polisi kati.

Baada ya kuhojiwa, mchekeshaji huyo ambaye jana alitakiwa kuripoti polisi na mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda alikwenda na polisi nyumbani kwake na kupekuliwa.

Alitakiwa kwenda polisi baada ya kuweka picha yenye sura yake huku akiwa ameketi katika kiti chenye nembo ya Taifa.

Pia, Idris aliweka picha nyingine inayoonyesha sura ya Rais John Magufuli akiwa amesimama huku amevaa suruali yenye mikanda inayoshikizwa mabegani (suspenda).

Hata hivyo, dakika chache baada ya Makonda kumtaka msanii huyo kuripoti polisi, waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Hamisi Kigwangalla aliahidi kumuwekea dhamana iwapo angekamatwa.

Eliya Rioba, mwanasheria wa mchekeshaji huyo amelieleza Mwananchi leo kuwa alipigiwa simu asubuhi akitakiwa kumfikisha mteja wake kituo hicho cha polisi kwa mahojiano.

Advertisement

“Walimpigia Sultan hawakumpata, wakampigia meneja wake Dokta Ulimwengu ambaye aliwapa namba zangu na wakanipigia. Nimekwenda naye saa 5 asubuhi na tumehojiwa hadi saa 10 jioni,” amesema Rioba.

Amesema katika upekuzi huo, polisi wamechukua kompyuta mpakato kwa ajili ya uchunguzi, kwamba walipofika kituoni walipelekwa kitengo cha makosa ya mtandaoni.

“Ameshikiliwa  kwa makosa mawili,  la kujifananisha na mtu mwingine na kuchapisha taarifa za uongo. Makosa ambayo yameainishwa kwenye kifungu namba 15 na 16 vya sheria ya makosa ya mtandao ya mwaka 2015,” amesema Rioba.

Ameongeza, “muda huu (saa 12 jioni)  tunarudi kituoni, ninakwenda kushughulikia taratibu za dhamana ikiwezekana atoke leo.”

Kamanda wa polisi mkoa wa Ilala, Zuberi Chembela alipoulizwa kuhusu kushikiliwa kwa mchekeshaji huyo amesema, “mpigie Kamanda Mambosasa kwa sababu issue yake imetoka Kamati ya Ulinzi na Usalama ya mkoa, wao wanaweza kuwa na majibu.”

Mambosasa alipoulizwa kuhusu suala hilo amesema hana taarifa yoyote.

 

Ilivyokuwa

Mkasa ulianza kama masihara kwa Idris kuweka katika ukurasa wa mtandao wa kijamii wa Instagram picha yenye sura yake akiwa ameketi katika kiti chenye nembo ya Taifa huku akiandika “kwa siku moja tukabadilishana kazi ili a-enjoy siku yake ya kuzaliwa kwa amani.”

Baada ya kuweka picha hiyo, Makonda alichangia katika mtandao huo na kumtaka mchekeshaji huyo wa vituko vya ‘Sio Habari’ kujisalimisha polisi.

“Naona mipaka ya kazi yako huijui, nenda sasa hivi kituo chochote cha polisi uwaambie Makonda kaniambia nije utakuta ujumbe wako,” aliandika Makonda.

Baada ya mkuu huyo wa mkoa kueleza hayo, Dk Kigwangalla alishindwa kuvumilia badala yake akaandika katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Instagram, “nimeambiwa kuna msanii wa vichekesho anatafutwa na polisi. Mniambie nitajitolea mwanasheria wa kwenda kumuwekea dhamana na kumtetea. Rais wetu ni mtu wa watu na imejidhihirisha kwa jinsi wananchi walivyojitolea kumuombea dua siku ya kuzaliwa kwake. Wameonesha upendo.”

Alipozungumza na Mwananchi baadaye kuhusu sakata hilo, Makonda alisema “nimesema kweli aende polisi sina utani na watu wa aina hiyo.”

Kuhusu hatua ya Dk Kigwangalla kumwekea dhamana Idris iwapo atakamatwa, Makonda alisema “brother ile Twitt sikumuandikia mtu yeyote zaidi ya Idris, nenda kaisome vizuri.”

 

 

Advertisement