Jiji la Dodoma lang'ara ukusanyaji mapato, Waziri Jafo ataka wakurugenzi kujitathimini

Muktasari:

  • Waziri wa nchi ofisi ya Rais Tamisemi Seleman Jafo ametoa taarifa za mapato ya halmashauri zote katika robo ya kwanza ya mwaka wa mapato Julai mosi hadi Septemba 30, 2019 huku akiwataka wakurugenzi ambao halmashauri zao hazikusanyi vizuri kujitathimini.

Dodoma. Jiji la Dodoma nchini Tanzania limeendelea kuwa kinara katika ukusanyaji wa mapato baada ya kukusanya Sh13.1 bilioni licha ya kuwa kiasilimia wamekusanya asilimia 18 nyuma ya Jiji la Dar es Salaam ambao wako asilimia 38 hadi Septemba 30, 2019.

Takwimu hizo zimetolewa leo Jumatatu Oktoba 21,2019 na Waziri wa nchi Ofisi ya Rais Tamisemi, Seleman Jafo wakati akitoa taarifa za mapato ya halmashauri zote katika robo ya kwanza ya mwaka wa mapato Julai mosi hadi Septemba 30, 2019.

Waziri Jafo amesema wakurugenzi wa maeneo ambayo hawajafanya vizuri waendelee kujitathimini vinginevyo itakula kwao.

Ametoa takwimu za mapato kwa kulinganisha makundi ya halmashauri, miji, manispaa na majiji lakini wilaya ya Buhigwe imeburuza mkia katika makundi yote kwa kukusanya Sh35 milioni.

"Kwa wastani hadi sasa halmashauri zimekusanya Sh166.24 bilioni ambayo ni asilimia 22 ya lengo la kukunya Sh765.48 bilioni ambazo zilipitishwa na Bunge zikusanywe," amesema Jafo.

Katika makundi ya Mikoa, Dar es Salaam imekuwa kinara ikikusanya Sh39.53 bilioni huku Kigoma ikiwa ya mwisho katika kundi hilo kwa kukusanya Sh2.12 bilioni.

Kwa asilimia katika majiji, Dar es Salaam imefikia asilimia 38 wakati mwisho ni Dodoma (18), Manispaa ya Sumbawanga imeongoza kundi hilo kwa asilimia 42, Kigoma Ujiji ikiwa na asilimia 9, Kwa Miji Tunduru ni kinara (39) huku Nanyamba ikishindwa kufurukuta kwa kukusanya asilimia 4.

Kundi la wilaya Msalala imefikisha asilimia 52 Kyelwa ikiburuza mkia kwa asilimia 3.