Lissu: Nikiwa rais Bunge litarushwa mubashara

Muktasari:

Mgombea huyo aliwataka wananchi kuhamasishana kwenda kupiga kura ili kufanya mabadiliko ya utawala wa nchi yao zikiwa zimebaki siku 9 kufikia siku ya Uchaguzi, Oktoba 28.

Dodoma. Mgombea urais wa Chadema, Tundu Lissu amesema akichaguliwa rais atarudisha utaratibu wa kurusha matangazo ya Bunge moja kwa moja ili wananchi waone wabunge wao wanafanya nini.

Lissu aliyasema hayo jana wakati wa mkutano wake wa kampeni uliofanyika Manyoni mkoani Singida wakati akielekea Dodoma kwa ajili ya mikutano ya kampeni.

Alisema wananchi wana haki ya kujua viongozi waliowachagua wanafanya nini na wanaruhusiwa kuwakosoa pia pale ambapo wanakosea.

“Nikichaguliwa nataka Bunge liwe live (mubashara), tuone wabunge wanafanya nini, kama ilivyokuwa wakati wa (Rais mstaafu, Jakaya) Kikwete,” alisema mgombea huyo.

Lissu alisema Bunge lililopita lilishindwa kufanya kazi yake ipasavyo na kubaki kuwa chombo cha kuisifia Serikali badala ya kuisimamia.

“Mara kadhaa nimemsikia Rais Magufuli akisema mumchagulie wabunge ambao atawadhibiti. Rais akidhibiti Bunge ni maafa kwa wananchi, Bunge haliwezi kufanya chochote,” alisema Lissu.

Mgombea huyo aliwataka wananchi kuhamasishana kwenda kupiga kura ili kufanya mabadiliko ya utawala wa nchi yao zikiwa zimebaki siku 9 kufikia siku ya Uchaguzi, Oktoba 28.

Alisema uchaguzi wa mwaka huu ni muhimu kuliko wakati wowote kwa sababu unakwenda kutengeneza serikali ambayo italinda uhuru, haki na maendeleo ya watu.

“Katika hizi siku 10 zilizobaki, hakikisheni mnahamasishana kwenda kupiga kura ili mfanye mabadiliko ya utawala wa nchi yenu,” alisema mgombea huyo.

Lissu aliwataka wananchi wakapige kura kuchagua uhuru wa kuwasema viongozi waliowachagua na kuwakosoa pale wanapokosea.

“Mkachague chama kitakacholinda uhuru wenu, lazima muwakosoe viongozi mliowachagua,” alisema Lissu huku akishangiliwa na wananchi wa Manyoni.

Kwa upande wake, mgombea ubunge katika jimbo la Manyoni, Aisha Luja aliahidi kuwatatulia wananchi wake kero ya maji ambayo inawakabili kwa muda mrefu.

“Ndugu zangu mkituchagua tutakwenda kuhakikisha kwamba mnapata maji safi na salama. Serikali ya Chadema itasimama pamoja nasi katika changamoto tulizonazo,” alisema Luja.

Akiwa Kongwa, Lissu alisema akiingia madarakani atakuwa na kazi kubwa ya kuliponya Taifa kutokana na mauaji wa watu na vitendo vya dhuluma kila kona ya nchi hii.

“Nipeni kura zenu ili tutengeneze nchi huru na nchi ya haki,” alisema mgombea huyo na kushangiliwa na wananchi wa Kibaigwa.

Alisisitiza kwamba miaka mitano ya dhuluma na unyanyasaji sasa basi huku akiwataka wananchi kwenda kupiga kura itakayomwezesha kufanya mabadiliko ya kiutawala.