RIPOTI MAALUMU: Mahudhurio ya wajawazito kliniki yaongezeka nchini

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu. Picha ya Maktaba

Ustawi wa maisha ya binadamu hutegemea na namna alivyoandaliwa kabla ya ujauzito, wakati wa ujauzito, wakati wa kuzaliwa na baada ya kuzaliwa.

Hata hivyo haiishii hapo bali huenda mbali zaidi na kuhesabu siku muhimu au kipindi muhimu cha siku 1,000 za kwanza baada ya kuzaliwa na maisha yatakayofuata.

Duniani kote, karibu nusu ya vifo vya watoto wa umri wa chini ya miaka mitano kila mwaka hutokana na ukosefu wa lishe bora na ya kutosha, unaosababisha kudhoofika kwa kinga za mwili dhidi ya magonjwa.

Wataalamu wanaeleza kuwa endapo mama hakupata lishe ya kutosha wakati wa ujauzito au mtoto wake hakupata lishe ya kutosha ndani ya siku 1,000 za mwanzo wa maisha yake, ukuaji wa mtoto kimwili, kiakili na maendeleo yake hudumaa. Hali hiyo hairekebeshiki mtoto atakapokuwa mkubwa – itamuathiri mtoto kwa kipindi chote cha maisha yake.

Nchini Tanzania idadi ya kina mama wanaohudhuria kliniki imezidi kuongezeka, kwa sasa zaidi ya asilimia 98 ya wajawazito huhudhuria kliniki walau mara moja, tangu utafiti wa Tanzania Demographic Health Survey (TDHS) mwaka 2015/16.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu amesema juhudi mbalimbali zilizofanywa zimewezesha wajawazito wengi kupata huduma za dawa kinga kama SP, ambayo ni kinga tiba dhidi ya malaria.

Pia ametaja dawa nyingine kama Fefol ambayo ni kinga au tiba dhidi ya upungufu wa damu, vipimo vya pressure, kaswende, wingi wa damu, sukari na huduma nyingine muhimu kwa kiwango kikubwa.

Hata hivyo kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa mwaka 2018, wajawazito 2,086,930 walihudhuria kliniki wakati wa ujauzito ikilinganishwa na wanawazito 2,009,879 mwaka 2017.

Mwongozo wa utoaji huduma za afya ya uzazi na mtoto unaelekeza wajawazito kuanza huduma mapema kabla ya majuma 12 ya mwanzo na kuhudhuria kliniki angalau mara nne katika kipindi cha ujauzito ili wapate huduma zote muhimu.

Kipindi cha mwaka 2018 asilimia 25 ya wajawazito nchini waliweza kufanya hudhurio la kwanza kabla ya majuma 12 ikilinganishwa na asilimia 18 mwaka 2017, huku takwimu zikionyesha ongezeko la idadi ya wajawazito waliohudhuria kliniki angalau mara nne imeongezeka kwa mwaka 2018 na kufikia asilimia 57 ikilinganishwa na asilimia 46 mwaka 2017.

Ikilinganishwa na kipindi cha nyuma, takwimu zinaonyesha upatikanaji wa dawa ya Oxytocin na dawa nyingine muhimu kama antibiotiki zinazotumika wakati wa kujifungua kwa ajili ya kuzuia na kutibu matatizo ya kutokwa na damu nyingi pamoja na uambukizo umekuwa ni wa uhakika na kuridhisha kwa kipindi chote cha kuanzia mwaka 2017, 2018 hadi mwezi Februari 2019 ambapo dawa hizi sasa zinapatikana kwa zaidi ya asilimia 94 katika vituo vyote vya kutolea huduma nchini.

Upatikanaji wa dawa za chaguo la pili yaani Ergometrin au Misoprostol ambazo hutumika pale ambapo dawa hiyo ya oxytocin inapopungua au kukosekana nao umekuwa wa uhakika zaidi kwenye vituo vyote vinavyotoa huduma za uzazi hususani za kujifungua.

Kwa upande wa huduma za kujifungua katika vituo vya kutolea huduma za afya (Institutional deliveries), Waziri Ummy anasema kwa kipindi cha Julai - Desemba 2018, ilitolewa kwa jumla ya wajawazito 762,676, sawa na asilimia 72, ikiwa ni ongezeko kubwa la wanawake wanaojifungulia kwenye vituo ukilinganisha na asilimia 63 ya mwaka 2015.

Huduma baada ya kuzaliwa

Waziri Ummy anasema akina mama na watoto wachanga, wanaohudhuria kliniki baada ya kujifungua wamezidi kuongezeka.

“Hii ina manufaa katika kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi na vifo vya watoto wachanga kwani asilimia kubwa ya vifo hutokea ndani ya siku saba baada ya kujifungua. Hivyo mahudhurio sahihi ndani ya saa 48 na siku ya saba baada ya kujifungua ni muhimu. “Niwaombe wanawake wenzangu na watoa huduma za afya kuhakikisha kuwa huduma baada ya kujifungua zinaendelea kuimarishwa ili kufanya ufuatiliaji wa karibu wa afya ya mama na mtoto kama ilivyoelekezwa kwenye miongozo iliyotolewa na Wizara.” Amesema.

Takwimu za TDHS zilizochapishwa mwaka 2015 zilionyesha kuwa kwa kila vizazi hai 100,000 nchini kulitokea vifo 556 vya akina mama kwa mwaka.

Lakini Waziri Ummy anasema takwimu hizo ni za miaka minne iliyopita, na ni uashiria wa matukio ya miaka 5-10 iliyopita kabla ya mwaka 2015.

“Ninapenda kuwahakikishia Watanzania kuwa takwimu zilizokusanywa kutoka kwa waratibu wa huduma za Afya ya Uzazi na Mtoto wa mikoa yote Tanzania Bara mwaka 2018 vinaonyesha kuwa vifo vitokanavyo na uzazi vinaendelea kupungua.

“Sambamba na uwekezaji mkubwa kwenye sekta ya afya uliofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano, wataalam wanatufahamisha kwamba tafsiri ya uwiano wa vifo 556 kwa kila Vizazi Hai 100,000 ni vifo halisi vya akina mama ambavyo ni takriban 11,000. “

Anasema ufuatiliaji wa vifo halisi yaani kwenye vituo vya afya na kwenye Jamii, vilivyotokea mwaka 2018 unaonyesha kuwa idadi halisi ya vifo hivyo ilikuwa ni 1,744.

“Kwa hiyo imani yetu ni kwamba utafiti unaofuata wa TDHS utakuja na matokeo yatakayoonyesha kwamba tayari tumepiga hatua kubwa katika kupunguza vifo vya akina mama hapa nchini.

“Hata hivyo ninapenda kusisitiza kwamba sisi kama Serikali tunataka vifo vyote vinavyozuilika tuhakikishe tunavizuia kwani si haki kwa mwanamke kupoteza maisha wakati analeta kiumbe kingine duniani, hivyo niwaombe wanawake wenzangu, wanaume wote nchini na watoa huduma za afya wote tufanye kila linalowezekana kuzuia vifo hivi kwenye maeneo yetu.”

Waziri Ummy anawapongeza wananchi na watoa huduma za afya katika Kijiji cha Uturo, wilayani Mbarali katika Mkoa wa Mbeya kwa kuamua kufanya kweli kwani kwa takribani miaka 20 sasa katika kijiji hicho hakuna mwanamke wala mtoto mchanga aliyepoteza maisha wakati wa kujifungua bila sababu za msingi.

Lishe

Utapiamlo kwa mtoto hujitokeza pale mwili unapokosa kiasi cha kutosha cha nishati (kalori), protini, wanga, mafuta, vitamini, madini na lishe nyingine zinazohitajika kwa ajili ya kufanya viungo vya mwili vikue na kufanya kazi vizuri.

Mtoto chini ya miaka mitano au mtu mzima anaweza kupata tatizo la utapiamlo kwa kukosa lishe ya kutosha au kupewa lishe zaidi ya inavyohitajika.

Kufuatia hili, Waziri Ummy anasema lishe ni moja ya ajenda zilizojadiliwa katika mkutano wa mawaziri wa afya nchi za Sadc na mipango imewekwa.

Anasema changamoto kuhusu lishe ni kubwa nchini na hasa katika mikoa inayozalisha chakula kwani watoto wengi wana utapiamlo licha ya kuwa na chakula cha kutosha. “Tumeweka kanuni za pamoja za katazo la uhamasishaji wa matumizi ya maziwa ya kopo na vyakula mbadala kwa watoto wachanga na wadogo na kumlinda mama anayenyonyesha yaani likizo ya uzazi,” anasema.

Anasema watoto wengi wanashindwa kunyonya kwa kipindi wanachohitaji kiasi kwamba wanaanzishiwa maziwa mbadala mapema jambo ambalo ni kinyume na kanuni za afya.

“Tumeazimia kutumia mfumo wa kikanda kuboresha lishe kwa watoto na mkakati wa kikanda wa kudhibiti uzito uliozidi na kiribatumbo katika jamii,” anasema.

Anasema wameazimia kuwepo kwa matumizi ya kadi alama za lishe kwa nchi za Sadc, na uongwezwaji wa virutubishi vya vitamini na madini wakati wa usindikaji kwenye unga wa mahindi, unga wa ngano, sukari, mafuta ya kula na chumvi.