Maji Nyumba ya Mungu yaashiria hatari

Sunday February 16 2020

 

By Daniel Mjema,Mwananchi [email protected]

Moshi. Hali ni tete katika vijiji ambavyo vinapitiwa na mkondo wa maji yanayotoka Nyumba ya Mungu kutokana na bwawa hilo kujaa maji na kuwepo uwezekano wa mafuriko na tayari uongozi wa wilaya ya Mwanga umewataka wananchi katika maeneo hayo kuhama haraka.

Kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya ya Mwanga pamoja na kamati ya maafa, zimewataka wananchi hao kuondoka haraka, vinginevyo itatumia polisi kuwahamisha ili kuepusha madhara.

Mtaalamu wa haidrolojia wa ofisi ya Bonde la Pangani (PBWO), Philipo Patrick alililiambia gazeti hili jana kuwa wakuu wa mikoa na wilaya zinazozunguka bwawa hilo wameshajulishwa.

Bwawa hilo linazungukwa na wilaya za Mwanga na Moshi za mkoa wa Kilimanjaro na Simanjiro kwa mkoa wa Manyara na maji yake hutiririka na kuingia mto Pangani na baadae kuingia Bahari ya Hindi.

“Bwawa limeanza kujaa tangu Januari 8, si leo tu. Wakuu wa mikoa ya Kilimanjaro na Manyara, wakuu wa wilaya zinazozunguka bwawa na watendaji wa vijiji wote tumeshawapa taarifa,” alisema Philipo.

Mkuu wa wilaya ya Mwanga, Thomas Apson aliliambia gazeti hili jana kuwa tayari kamati ya maafa iko kazini kujiandaa na akaonya kuwa endapo wananchi hawatahama kwa hiari, Serikali itatumia nguvu kuwahamisha.

Advertisement

“Sisi tumeona kuna hatua mbili za kuchukua. Ya kwanza ni uongozi wa bonde la Pangani kutusaidia kufunga kitaalamu mtiririko ule wa maji. Kitaalamu inawezekana,” alisema Apson.

“Njia ya pili ni kamati yetu ya maafa na idara ya mifugo na uvuvi kwa kutumia watendaji wa kata za Kiria na Lang’ata kuhamasisha wananchi walio katika huo mkondo wa maji kuhama.”

Mkuu huyo wa wilaya alisema endapo hadi Jumatatu uongozi wa bonde la Pangani utakuwa umekwama kufunga mtiririko, itabidi tuwahamishe watu kwa lazima kwa kutumia Jeshi la Polisi kuliko tusubiri kupoteza maisha ya watu,” alisema.

Diwani wa Kata ya Shighatini, Enea Mrutu aliupongeza uongozi wa serikali ya Mwanga kwa namna walivyolichukua suala hilo kwa uzito, akisema wananchi wanaotakiwa kuhama ni wale walio katika hatari tu, hasa kijiji cha Kiria.

Mbunge wa Mwanga, Profesa Jumanne Maghembe alisema bwawa hilo limeanza kutema maji lakini mvua imesimama hivyo huenda madhara yasiwe makubwa iwapo hazitaendelea kunyesha.

“Nadhani hakutakuwa na shida sana kama mvua itakoma,” alisema mbunge huyo aliyekuwa waziri katika serikali ya Awamu ya Nne na ya Tano.

“Mvua imenyesha tangu Septemba (2019) mpaka sasa. Ilikoma kwa siku tano, lakini juzi (Alhamisi) imeanza tena kunyesha. Tusubiri wiki ijayo tuone.”

Profesa Maghembe aliungana na mkakati wa serikali ya wilaya kuwa kama utiririshaji huo wa maji kutoka bwawa hilo utatishia uhai wa wananchi, hakuna njia nyingine zaidi ya kuwahamisha walio jirani na pia kufunga barabara ya Ngorika kwa upande wa Simanjiro.

Advertisement