Marekani yajiandikia historia, rekodi mpya Uchaguzi Mkuu 2020

Muktasari:

Ni Joe Robinette Biden jr. Ukimwita Joe Biden inatosha na utaeleweka zaidi. Mwaka 1978, alikuwa kijana mwenye umri wa miaka 44. Ni kijana kwa siasa za Marekani hasa ngazi ya urais. Mwaka huo, Biden alijitosa kuwania tiketi ya Democratic kuwa mgombea urais katika uchaguzi wa mwaka 1988.

Yule mwanasiasa mahiri kijana, aliyekuwa na nafasi kubwa ya kuteuliwa kuwa mgombea urais Marekani kupitia chama cha Democratic, akalazimika kujiondoa kwenye mbio baada ya kuandamwa na vyombo vya habari kwa kashfa ya udanganyifu, sasa ndiye anayeelekea kuwa rais mzee zaidi kuwahi kutokea kwenye nchi hiyo.

Ni Joe Robinette Biden jr. Ukimwita Joe Biden inatosha na utaeleweka zaidi. Mwaka 1978, alikuwa kijana mwenye umri wa miaka 44. Ni kijana kwa siasa za Marekani hasa ngazi ya urais. Mwaka huo, Biden alijitosa kuwania tiketi ya Democratic kuwa mgombea urais katika uchaguzi wa mwaka 1988.

Kipindi hicho, Biden alikuwa na miaka 14 kwenye Seneti. Matumaini yakawa makubwa mno upande wake ya kushinda tiketi ya Democratic. Ikaibuliwa kashfa kuwa alitumia maneno yasiyo yake kwenye hotuba kwamba Biden alinakili maneno mengi kwenye hotuba moja ya kiongozi wa zamani wa chama cha Labour, Neil Kinnock na kuyageuza kuyafanya yake.

Biden ni mwanasheria. Alikumbwa na kashfa nyingine ya kukuza matokeo yake ya chuo, alipokuwa anasoma shule ya sheria. Kashfa hizo mbili, ndizo zilisababisha Biden aitishe mkutano wa waandishi wa habari Septemba 23, 1987, akatangaza kujiondoa kwenye mchuano wa kusaka tiketi ya Democratic.

Mwaka 2007, akiwa seneta mkongwe kwa miaka 34, alitangaza tena kuwania tiketi ya Democratic kuwa mgombea urais kwenye uchaguzi wa mwaka 2008.

Lakini alizidiwa na maseneta wawili; Hillary Clinton aliyekuwa seneta kwa miaka sita, na Barack Obama aliyekuwa seneta kwa miaka miwili, kwa umaarufu na ushawishi.

Alipoona mzani wa mchuano umelalia kwa Obama na Hillary, akaamua kujitoa baada ya kuambulia asilimia moja tu ya kura za awali katika jimbo la Iowa.

Obama alimteua Biden kuwa mgombea mweza wake, kisha wakashinda. Biden akawa Makamu wa Rais wa Marekani kwa miaka minane.

Mwaka 2015, Biden alionekana angeingia kwenye kinyang’anyiro cha kuomba tiketi ya Democratic kuwa mgombea urais 2016. Mwaka huo, akafiwa na mwanaye kipenzi, Beau. Kifo cha Beau kwa kiasi kikubwa kilimwathiri Biden. Hakujitokeza.

Mwaka 2019, akiwa na nishati za kutosha, alijitosa ulingoni. Akashinda ndani ya Democratic, kisha ameshinda urais katika hatua mbili muhimu, ameongoza kura za umma (popular votes), ameongoza pia kwa kujinyakulia wajumbe wengi wa baraza la uchaguzi (electoral college) ambao watapiga kura za majimbo Desemba 14, mwaka huu, kumuidhinisha kuwa Rais.

Kwa nini historia imeandikwa

Historia imeandikwa kwa sababu Biden ataapishwa kuingia madarakani akiwa na umri wa miaka 78. Atakuwa Mmarekani anayeongoza kwa umri mkubwa kuapa kuwa Rais wa Marekani. Mungu akimpa uhai, miaka minne ijayo atakuwa Rais atakayeondoka Ikulu akiwa na miaka 82, ambao ni umri mkubwa zaidi.

Kama Biden ataongoza vipindi viwili, ataondoka madarakani akiwa na umri wa miaka 86.

Kwa sasa Rais anayeshikilia rekodi ya kuondoka Ikulu akiwa na umri mkubwa zaidi ni wa 40, Ronald Reagan aliyeondoka Ikulu ya Marekani akiwa na umri wa miaka 77, miezi 11 na siku 14. Yaani ilikuwa bado siku 17 angeondoka White House akiwa na umri wa miaka 78.

Ni uchaguzi wa rekodi

Rais wa 45 wa Marekani, Donald Trump, ameingia kwenye orodha ya marais wa Marekani ambao walishindwa kwenye uchaguzi wa kuwania muhula wa pili.

Sasa Marais wa Marekani walioshindwa kwa kura katika kinyang’anyiro cha kurejea madarakani muhula wa pili wamefikia 10. Mpaka sasa Trump hajakubali matokeo kama ilivyo utamaduni wa uchaguzi wa Marekani. Hoja zake nyingi ni kwamba kaibiwa kura.

Hata mwaka 2016 alisema angeibiwa kura, lakini aliposhinda alifurahia matokeo. Kabla ya uchaguzi mwaka huu, Trump aliulizwa kama angekubali matokeo na kukabidhi nchi kwa mshindi kama angeshindwa, hakusema kama angekubali kushindwa.

Biden alipoulizwa kuhusu nini kitafanyika kama Trump atagoma kuondoka ikulu, alijibu: “Jeshi litamtoa.” Jawabu hilo linamaanisha kuwa kukaa madarakani au kuondoka haijawahi kuwa uamuzi wa mtu, isipokuwa mifumo ambayo inafanya kazi kikatiba na sheria zilizotungwa kuendana na Katiba ya Marekani.

Uchaguzi, uthibitisho wa rais, kiapo cha rais na ukomo wa rais, kila kitu kimeandikwa ndani ya Katiba. Ibara ya II ya Katiba ya Marekani, inasema; “Rais ataongoza muhula wenye miaka minne.” Mabadiliko ya Katiba ya 20 yanasema: “Ukomo wa Rais na Makamu wa Rais ni saa 6:00 mchana ya Januari 20.”

Kwa maana hiyo, ikifika Januari 20, mwakani, saa 6:00 mchana, kwa mwongozo wa Katiba ya Marekani, itakuwa ni kikomo cha Trump na makamu wake, Mike Pence, kuendelea kuihudumia nchi hiyo kwa nafasi za Rais na Makamu wa Rais, hivyo kuruhusu mwanzo wa muhula mpya wa Biden na makamu wake, Kamala Harris, kama watathibitishwa.

Kwa takriban miaka 250 sasa, marais wa Marekani walioshindwa uchaguzi baada ya kumaliza muhula mmoja au waliomaliza mihula miwili, wamekuwa wakiheshimu Katiba. Hakuna ambaye amewahi kung’ang’ania madaraka baada ya ama kushindwa uchaguzi au kumaliza mihula miwili.

Rais wa Pili wa Marekani, John Adams, japo alikuwa mwenye kinyongo baada ya kushindwa, lakini aliachia madaraka. Rais wa 37 wa nchi hiyo, Richard Nixon, baada ya hoja ya kupigiwa kura ya kutokuwa na imani naye kupita kwenye Seneti, alijiuzulu mwenyewe.

Hivyo, hapajawahi kutokea kuwepo matumizi ya nguvu kumuondoa Rais madarakani aliyeng’ang’ania.

Kwa muktadha huo, kama Trump ataendelea kung’ang’ania madaraka na matokeo yake kuondolewa kwa nguvu, ataandika historia mpya, hivyo kuufanya uchaguzi wa Rais Marekani 2020 kuwa na historia ya aina yake.

Rekodi ya Kamala Harris

Januari 20, mwakani, Biden atakapomaliza kuapa kuwa Rais wa 46 wa Marekani, Kamala Harris pia atakula kiapo cha kuwa Makamu wa Rais wa taifa hilo. Ataweka rekodi tatu kwa wakati mmoja, kwanza ni mwanamke wa kwanza kusimama kama mgombea mwenza na kushinda kiti cha urais.

Pili, atakuwa mwanamke wa kwanza kuwa makamu wa rais wa Marekani. Tatu, ataandika rekodi ya kuwa mwanamke wa kwanza mwenye asili ya Afrika na Asia, kushika nafasi kubwa zaidi Marekani. Kwa kifupi, Marekani hakujawahi kuwa na mwanamke aliyepata kushika nafasi kubwa kama aliyoipata Kamala akishakula kiapo Januari 20, mwakani.

Mapema mwaka jana, usingedhani kama Kamala angesimama kama mgombea mwenza.

Alijitokeza kuwania tiketi ya Democratic kuwa mgombea urais. Ghafla akaanza kumshambulia Biden kuwa ni mbaguzi wa rangi. Desemba mwaka jana, akajitoa kwenye mbio za kuwania tiketi ya Democratic na kumuunga mkono Biden.

Kipindi ambacho Kamala anamshambulia Biden, ilikuwa mshangao kwa kila aliyefahamu uhusiano wao. Kamala alikuwa rafiki kipenzi wa mtoto wa Biden, Beau, aliyefariki dunia mwaka 2015 kwa ugonjwa wa kansa. Ni Beau aliyemkutanisha Kamala na Biden.

Kamala katika kitabu chake: “The Truths We Hold; An American Journey” – “Ukweli Tunaoukumbatia; Safari ya Mmarekani”, anaeleza kwa undani jinsi ambavyo Beau alivyokuwa rafiki yake mkubwa. Nyakati ngumu za majukumu. Beau akiwa Mwanasheria Mkuu wa jimbo la Delaware na Kamala Mwanasheria Mkuu wa jimbo la California.

“Tulikuwa tukizungumza mara kwa mara. Hata mara nne kwa siku,” Kamala anaeleza kufafanua jinsi ambavyo Beau alipata kuwa mshauri wake mkuu katika nyakati ngumu za kukabili majukumu yake kama Mwanasheria Mkuu wa California. Na ndio ikawa sababu watu kushangazwa na kitendo cha Kamala kumbadilikia Biden, baba wa Beau, na kumwita mbaguzi.

Hata hivyo, Biden akawa hana kinyongo. Baada ya kushinda mbio za uteuzi kuwa mgombea urais wa Democratic, akamteua Kamala kuwa mgombea mwenza. Biden akasema: “Hakuna maoni ambayo huwa nayazingatia kuliko ya Beau.” Hapo Biden alikuwa anafikisha ujumbe kuwa kwa kuwa Beau alimuona Kamala ni mwanamke jasiri, mchapakazi na mwenye weledi, basi haikuwa shida kwake kumteua kuwa mgombea mwenza.

Hoja za Trump na usahihi

Trump amekuwa akilalamika kuwa upigaji kura kwa njia ya barua pepe unazungukwa na wizi. Malalamiko hayo aliyatoa kupitia mtandao wa Twitter kwa zaidi ya mara 70. Ni malalamiko bila ushahidi. Kwa mujibu wa taasisi ya kituo cha haki, Brennan Center for Justice, wizi wa kura Marekani ni vigumu kutokea. Uwezekano wake ni chini ya asilimia 0.0009.

Karibu kila hoja ambayo Trump aliijenga kuhalilisha madai yake ya kuibiwa kura, ilikosa mashiko. Mathalan, katika moja ya tweet za Trump, alilalamika: “Makumi mamilioni ya watu wamepiga kura kinyume na sheria pasipo kuthibitishwa.

Ukweli ni kuwa majimbo tisa, pamoja na wilaya kuu ya Washington DC, utaratibu ulikuwa kupiga kura bila maswali. Majambo matano ndiyo yalitaka uthibitisho kwa sababu ya janga la Covid-19. Majimbo ya Colorado, Hawaii, Oregon, Utah, Washington, California, New Jersey na Vermont, ambayo hayakuwa na mashambulizi makali ya Covid-19, yalipiga kura bila maswali.

Ni utaratibu uliokuwa wazi kwa kila chama. Ukweli ambao upo wazi ni kuwa Democrats wengi walivutiwa kupiga kura mapema na viongozi wa chama hicho walifanya kampeni kwa watu wenye udhuru wa kupiga kura siku ya uchaguzi (absentee), wajitokeze mapema. Republicans wao utamaduni wao ni kupiga kura siku ya uchaguzi.

Mfano ni jimbo la Pennsylvania, katika kura milioni 2.5 za njia ya posta zilizohesabiwa, kura za waliosajiliwa kama Democrats zilikuwa mara tatu ya zile za watu wa Republicans, kuonesha kuwa Democrats walikuwa na mwamko wa kupiga kura mapema. Kipindi Democrats wakihamasishana kupiga kura, Trump alikuwa akilaumu kuwa kura za mapema ni wizi.