Mfumo wa dunia ulivyotikiswa unapaswa ufumwe upya tena

Thursday February 20 2020

 

By Ezekiel Kamwaga, aliyekuwa Japan

Kuelewa kuhusu kinachoendelea sasa katika eneo la Asia Mashariki ni muhimu sana kurejea katika historia na kujifunza kuhusu watu, siasa na utawala wake wa miaka mingi kabla ya sasa.

Baada ya kutembelea Japan na kuzungumza na wanasiasa, wasomi, askari na wananchi wa kawaida, nimejifunza kwamba tatizo kubwa la eneo hilo mfumo wa sasa wa kuendesha dunia unaonekana umepitwa na wakati na unahitajika mwingine kuendana na hali ya sasa.

Hili si jambo gumu kulielewa. Chukulia mfano wa nchi nne muhimu katika eneo hili; Japan, China, Korea Kusini na Korea Kaskazini. Zote zimefungamanishwa na historia yenye maelfu ya miaka. China ndiyo ya kwanza katika eneo hili kustaarabika. Yenyewe ilianza kustaarabika miaka 2000 kabla ya kuzaliwa kwa Yesu Kristo. Kwa hiyo, China ilikuwa inajitambua hata kabla dini za Kimagharibi hazijashika mizizi.

Lakini Korea; wakati huo ikiwa moja kabla ya kugawanywa, ilikuwa ya kwanza kujenga Taifa la kisasa miaka 195 kabla ya Yesu. Kisha Japan ikatengeneza Katiba yake ya kwanza kama nchi mwaka 604 baada ya kuzaliwa kwa Yesu.

Kufikia mwanzoni mwa milenia ya kwanza, China tayari lilikuwa taifa kubwa lenye nguvu kiuchumi duniani. Kwa mujibu wa rekodi zilizopo, China ilikuwa na Pato la Taifa (GDP) kubwa kuliko nchi yoyote duniani kwa miaka 1,000 ya kwanza baada ya Yesu.

Ndiyo sababu unatakiwa kuwa makini wakati watu wanaposema miaka 50 iliyopita China na Tanzania zilikuwa hazipishani sana kiuchumi. Ilikuwa kama nchi ya karne takribani 20 kabla Tanzania haijawa nchi.

Advertisement

Kuna kipindi karibu nchi zote za Asia Mashariki zilikuwa chini ya utawala wa himaya ya Mongolia iliyoongozwa kina Genghis Khan na Kublai Khan.

China na Korea zote ziliingizwa kwenye himaya hiyo ambayo baadaye ilikufa.

Katika karne ya 17, nchi karibu zote za eneo hili ziliamua kujifungia dhidi ya dunia ya nje kwa kipindi ambacho Wajapani wanakiita Edo. Lakini wao wakawa wajanja kwenye karne ya 19 kwa kujibadili na kufuata mfumo wa utawala wa kimagharibi kupitia utawala wa Meiji.

China ikaendelea na utawala wake wa Ufalme chini ya Qing hadi mwaka 1912 wakati Mfalme wa mwisho wa utawala huo alipoachia ngazi na nchi kuwa ya Kijamhuri.

Lakini wakati huo, Japan ilikuwa tayari imejiingiza kwenye mfumo wa utawala wa dunia ikifuata mfumo wa kimagharibi. China ikawa imechelewa.

Japan iliingia ndani ya mfumo huo ikajikuta ikichukua tabia za kibeberu kwa kuikalia Korea kimabavu mwaka 1910 hadi Vita ya Pili ya Dunia. Hadi leo Wakorea wana makovu na uchungu kutokana na matukio yaliyotokea wakati wakikaliwa na Wajapani.

China na Japan nazo zimewahi kuingia vitani mara mbili. Katika Vita ya Pili ya China na Japan iliyofanyika katikati ya karne ya 20, zaidi ya watu milioni 20 walipoteza maisha.

Halafu Japan ikashindwa kwenye Vita ya Pili ya Dunia. Baada ya kumalizika kwa vita hiyo, Korea Kusini na Korea Kaskazini zilizogawanywa kwa sababu ya vita baridi, nazo zikaingia vitani.

Hivyo, hili ni eneo ambalo vita zimekuwa jambo la kawaida kwa muda mrefu. Kabla ya Vita ya Pili ya Dunia, kwa kila nyakati, kulikuwa na himaya moja iliyokuwa ikitawala nyingine na mfumo uliwekwa na mtawala huyo.

Kwa sasa, eneo zima la Asia Mashariki linaongozwa na mfumo uliowekwa na mataifa ya Urusi na Marekani baada ya kumalizika kwa Vita ya Pili ya Dunia.

Japan kwa upande wake imeamua haitaki tena mambo ya vita na jukumu la ulinzi wa watu, mipaka na mali zake liliachwa kwa Jeshi la Marekani.

Kupitia makubaliano hayo maarufu kwa jina la Makubaliano ya San Francisco, jaribio lolote la kuishambulia Japan kijeshi, ni sawa na kuishambulia Marekani.

Hata hivyo, mfumo huu kwa sasa una matatizo. Wakati unatengenezwa, China haikuwa na nguvu za kijeshi wala kiuchumi ilizonazo sasa. Hata wakati mabeberu wanagawana bahari za Asia mwaka 1892, China haikuwa mojawapo ya nchi hizo.

Ukweli ni kuwa, China sasa ina nguvu za kiuchumi kuliko hata Urusi (Russia) iliyotengeneza mfumo huu wa kidunia. Wachumi na wataalamu wengine wa masuala ya kistratejia wanaamini China itaipiku Marekani kama taifa kubwa kiuchumi katika muongo huu. Maana yake lazima mfumo wa sasa unaotawala dunia na Bara la Asia uendane na ukweli huu. Katika historia ya dunia, hakujatokea wakati taifa lenye nguvu za kiuchumi na kijeshi likaheshimu mfumo usio na faida kwake.

China haikuwa sehemu ya ‘wakubwa wa dunia’ wakati bahari za dunia na visiwa vyake vikigawanywa haikuwa sehemu ya Makubaliano ya San Francisco na haikuwa sehemu ya wakubwa wakati Vita ya Pili ya Dunia inamalizika.

Kwa mtazamo wake, kizazi chao kilikuwa na machungu na kumbukumbu nyingi za nyuma na hivyo pengine hakikuwa kizazi mwafaka kwa maridhiano. Lakini vizazi vipya; vilivyozoea maridhiano na ushirikiano mwema baina ya watu wao, vinaweza kuvuka mtihani na kuleta amani na ustawi wa kudumu katika eneo hili nyeti kwa dunia.

Tusisahau kwamba takribani theluthi moja ya wanadamu hapa duniani wanaishi katika ene hili pekee.

Advertisement