Mjadala Lissu kuhamia ubalozini

Muktasari:

Sakata la makamu mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu kuhamia ubalozi wa Ujerumani kwa madai kuwa ametishiwa maisha, limeibua mjadala huku Jeshi la Polisi likisema halina taarifa za vitisho hivyo.

Dar es Salaam. Sakata la makamu mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu kuhamia ubalozi wa Ujerumani kwa madai kuwa ametishiwa maisha, limeibua mjadala huku Jeshi la Polisi likisema halina taarifa za vitisho hivyo.

Lissu, ambaye alikuwa nje ya nchi kwa takriban miaka mitatu baada ya kunusurika katika shambulio la risas 16, aliiambia Mwananchi juzi kuwa alienda ubalozi wa Ujerumani tangu Jumatatu baada ya kupokea vitisho dhidi ya maisha yake.

Lakini mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Simon Sirro aliiambia Mwananchi jana kuwa hana taarifa rasmi za Lissu, ambaye aligombea urais kwa tiketi ya Chadema na kushika nafasi ya pili, kutishiwa wala kuhamia ubalozi huo alipoulizwa jana kwa simu.

“Na mimi nasikia kama ulivyosikia wewe. Muulize mwenyewe kama ameshawasiliana na chombo chochote cha usalama kama kuna shida hiyo,” alisema IGP Sirro.

Hata alipoulizwa kama Jeshi la Polisi limefuatilia suala hilo baada ya kusikia, Sirro alimwelekeza mwandishi amuulize Lissu.

“Mngemuuliza yeye, maana yake hayo sisi tumesikia kuwa anahojiwa na ubalozi, kwa hiyo tunapata tabu kumuelewa huyo ndugu yetu. Yeye anajua nipo, haji kunijulisha. Tunakutana naye katika magazeti. Si anatafuta hifadhi sisi tutasemaje?” alihoji.

Lissu, aliyezungumza na Mwananchi kwa simu, alisema ameomba hifadhi katika ubalozi huo, baada ya kutishiwa maisha yake.

“Nilianza kutishiwa Jumamosi. Nilipigiwa simu na watu wakanitishia maisha. Jioni ya siku hiyo pia nilipigiwa simu,” alisema Lissu.

Matukio ya raia kukimbilia ubalozini kutokana na hofu ya usalama ni ya nadra nchini Tanzania, ambayo imejijengea sifa duniani ya kuwa “kisiwa cha amani”.

Hiki si kitu cha kawaida,” alisema Profesa Abdallah Safari, ambaye amejikita katika sheria za kimataifa.

“Mimi nimefundisha sheria za kimataifa, sijawahi kuona nchini. Nimeona hao jamaa (wapinzani) wakilalamikia rafu katika uchaguzi na wametoa vilelelezo.”

Profesa Safari alisema Lissu ana haki ya kuogopa kutokana na matukio yaliyompata na kwamba kitendo cha kwenda ubalozini kuomba hifadhi “kimeshaweka doa” kwa nchi.

Alisema sababu alizotoa Lissu zinakubalika kisheria kupewa hifadhi.

“Katika sheria za kimataifa kuna mkataba wa Vienna wa uhusiano wa balozi kuhusu haki ya kutafuta hifadhi; ni kwamba, makazi ya ubalozi ni mali ya nchi husika,” alisema.

“Ni kawaida kwa watu duniani kufanya hivyo wakiona mazingira yao ni hatarishi na kwa kawaida mabalozi hawawezi kumuweka mtu pale bila kuthibitisha kwamba mazingira yake ni ya hatari. Huwa ni mpaka wachunguze kujiridhisha.”

Kuhusu hatua zinazoweza kuchukuliwa kutokana na madai ya Lissu, Profesa Safari alisema ni vyombo vya kimataifa kwani vinaweza kuchukua hatua

Hoja hiyo inalingana na ya profesa wa sheria za kimataifa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Khoti Kamanga aliyesema Lissu si wa kwanza kuomba hifadhi ubalozini.

Alitoa mfano wa mwanaharakati na mhariri wa Australia aliyenzisha mtandao wa Wikileaks, Julian Assange aliyekwenda kujificha katika ubalozi wa Ecuador nchini Uingereza baada ya kufichua taarifa za jeshi la Marekani.

“Pia kuna kesi nyingi tu za kimataifa kuhusu hilo suala la diplomatic asylum (hifadhi ya kidiplomasia),” alisema Profesa Kamanga.

Akifafanua zaidi, profesa wa sayansi ya siasa wa Chuo Kikuu cha Ruaha cha Iringa, Gaudence Mpangala alisema suala hilo linaendelea kuitia doa nchi kimataifa.

“Hiyo si ishara nzuri, kwa sababu nchi yetu inalaumiwa kwa uvunjifu wa haki za binadamu na lawama mojawapo ni matukio hayo, ingawa Serikali imekuwa ikikanusha,” alisema.

Alisema suala la haki za binadamu ni jambo la kwanza ambalo Mwalimu Nyerere alilitambua baada ya uhuru wa mwaka 1961.

“Mwalimu Julius Nyerere alipohutubia Bunge la kwanza la Jamhuri ya Tanganyika, alisema nchi yetu imepata uhuru. Jambo la kwanza ni kufuata haki za binadamu. Alizungumzia usawa wa binadamu na maendeleo ya binadamu, lakini la kwanza ni misingi ya haki za binadamu,” alisema Profesa Mpangala.