Mkandarasi jela miaka 7

Thursday February 20 2020

 

By Pamela Chilongola, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imemhukumu mkandarasi wa majengo, Alfred Ndeka (60) kifungo cha miaka saba jela baada ya kukutwa na hatia ya kujipatia Sh116 milioni kwa udanganyifu.

Hakimu Vicky Mwaikambo alitoa hukumu hiyo namba 230/2016 baada ya kuridhishwa na ushahidi wa mashahidi watano wa upande wa mshtaka na vielelezo 11 vilivyowasilishwa.

Vicky alisema Mahakama imejiridhisha na ushahidi uliotolewa pasi na kuacha shaka kuwa mshtakiwa alitenda kosa hilo hivyo, inamhukumu kifungo cha miaka saba kwenda jela ili iwe fundisho kwa wengine.

“Kutokana na ushahidi na vielelezo vilivyotolewa unathibitisha ulipokea Sh116 milioni kwa njia ya udanganyifu huku ukijua kufanya hivyo ni kosa la kisheria,” alisema Vicky.

Awali wakili wa Serikali, Glory Mwenda alidai Desemba 2014 eneo la Kinondoni mshtakiwa alijipatia Sh116 milioni kutoka kwa Anthony Mkindo akidanganya kuwa fedha hizo zimetumika kununua vigae vya kuenzeka nyumba katika kampuni ya Nabaki Afrika.

Kabla ya kumtia hatiani, wakili wa Serikali, Glory Mwenda aliiomba mahakama hiyo impe mshtakiwa adhabu kali kwa mujibu wa sheria ili iwe fundisho kwa wengine wenye tabia hiyo.

Advertisement

Awali, Vicky alimpa mshtakiwa nafasi ya kujitetea na aliiomba mahakama hiyo impunguzie adhabu kwa kuwa anaumwa na anategemewa na familia.

Hata hivyo, Vicky alitupilia mbali maombi hayo na kwamba sheria lazima itende haki.

Advertisement