Advertisement

Mwakilishi ahofia hoja ya ‘kumbana’ Seif kukataliwa

Thursday February 13 2020
seif pic

Mwakilishi wa jimbo la Shauri Moyo Hamza Hassan Juma akichangia hoja katika ukumbi wa Baraza la wawakilishi uliopo Chukwani nje kidogo ya mjini wa Unguja. Picha na Muhammed Khamis

Unguja/Dar. Mwakilishi wa Shaurimoyo (CCM), Hamza Hassan Juma amesema ana wasiwasi wa kukataliwa kwa hoja yake katika Baraza la Wawakilishi (BLW) anakotaka watu wanaojiunga na vyama vya siasa wasiruhusiwe kugombea urais, uwakilishi na udiwani Zanzibar kabla ya kutimiza miaka miwili tangu walipojiunga.

Akizungumza na Mwananchi jana, Juma alisema wasiwasi alionao ni wa kawaida, kwa kuwa inaweza kukataliwa au kukubaliwa wakati wa uwasilishaji wake.

Hata hivyo, alisema tayari amemaliza kupitia vifungu vyote vya hoja yake hiyo na anachosubiri ni kuiwasilisha katika baraza hilo.

Alipoulizwa ni kitu gani kimeshindika kuiwasilisha jana kama alivyoahidi, alisema ni kutokana na kutokuwapo kwa Spika wa Baraza hilo, Zubeir Ali Maulid.

Licha ya wasiwasi huo, Hamza alisema anaamini hoja yake ni nzuri.

“Nimeambiwa Spika yupo Dar es Salama kwenye vikao vya chama mara atakaporudi tu nitafika ofisini kwake na kumkabidhi nilichokusudia,” alisema.

Advertisement

Alisema ikiwa atakubaliwa kuiwasilisha bungeni, ana uhakika itapata wachangiaji wengi ambao wataichambua zaidi.

Uamuzi wa mwakilishi huyo umekishtua Chama cha ACT-Wazalendo ambacho kimesema kitapinga sheria hiyo mahakamani endapo itapishwa kwa kuwa inakiuka misingi ya katiba, na utawala bora.

Endapo hoja hiyo iliyoshtukiwa awali na Maalim Seif Sharif Hamad itapitishwa na kutungwa sheria, itakuwa kitanzi kwa mshauri huyo wa ACT-Wazalendo na wenzake ambao Machi 18, 2019 walihama CUF na kujiunga chama hicho.

Maalim Seif na timu yake walijiunga na ACT wakipinga uamuzi wa kumtambua Profesa Ibrahim Lipumba kuwa mwenyekiti wa CUF.

Wanasheria watofautiana

Wakizungumzia suala hilo, Wakili Godwin Ngwilimi alisema kisheria endapo suala hilo litapita, watakaoathiriwa ni wanasiasa watakaohama vyama baada ya sheria hiyo kuanza kutekelezwa.

“Kikanuni, haitawahusu wagombea waliojiunga na vyama vya siasa miezi kadhaa iliyopita, muswada wa sheria ukiwahusisha hao itakuwa ni kinyume na msingi wa katiba, walalamikaji wanaweza kwenda mahakamani,” alisema Ngwilimi.

Lakini John Seka, rais wa zamani wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS), alisema Baraza hilo linaweza kutunga sheria inayoweza kuathiri walengwa wa miezi kadhaa kabla ya kutungwa kwake.

“Baraza linaweza kufanya hivyo, likatunga sheria inayoathiri waliojiunga hivi karibuni, si lazima athari zake zianze kuonekana baada ya kuanza utekelezaji wake, Katiba imesema Bunge litatunga tu sheria,” alisema Seka.

Advertisement