Ni agizo la Mungu kutii mamlaka ya nchi

Shaloom wana wa Mungu, jina langu naitwa Mchungaji John Kyashama kutoka Kanisa la River Healing Ministry of Tanzania, lililopo Kiluvya kwa komba –Bumbulu Jijini Dar es Salaam. Mimi pia ni mwanasheria.

Siku ya leo nitazungumzia suala muhimu kuhusu kutii mamlaka ya nchi.

Moja ya mahitaji makubwa kwa kanisa la Mungu ni namna ambavyo viongozi wa kanisa wanatekeleza maagizo ya biblia kwa waumini wao.

Tukisoma Waraka wa Warumi 13:1-2, biblia inazungumzia kuhusu umuhimu wa kutii mamlaka iliyopo ambayo ni Serikali.

Yesu alipokuwa duniani alichukua muda kuelezea kwa wazi uongozi wa kidunia ukisoma katika Mathayo 20:25-28.

Biblia inaandika: “Hivyo Yesu akawaita, akawaambia mnajua kwamba watawala wa mataifa hutawala watu wao kwa mabavu a wakuu hao kumiliki watu wao. Lakini kwenu isiwe hivyo, ila anayetaka kuwa mkuu kati yenu sharti awe mtumishi wa wote; na anayetaka kuwa wa kwanza kati yenu sharti awe mtumishi wetu. Jinsi hiyo hiyo mwana wa mtu hakuja kutumikiwa bali kutumikia na kutoa maisha yake kwa fidia ya wengi.”

Kwa hiyo, Yesu alitamka hivi haitakuwa hivyo kwenu na kuweka wazi kwa wanafunzi wake kamwe wasithubutu kutumia mkono mzito wa utawala na njia za kibinafsi za uongozi.

Baadala yake wale wanaomfuata Yesu wanapaswa kuwa watumishi wa watu wote.

Hii tabia ya viongozi wa kidini kukemea watawala wa kidunia katika madhabahu ya nyumba za ibada inapaswa kuangaliwa kwa makini, maana Bwana Yesu alisema viongozi wa kidini wanapaswa kuonyesha hali ya unyenyekevu na utii kwa watawala wa serikali.

Ni vyema kuelewa hili kwa jicho la uchambuzi: “Utumishi na uongozi,” kwa namna fulani huonekana kama yanapingana.

Kwa upande mwingine mtumishi ni yule aliyeajiriwa na mtu mwingine ambaye hutenda mapenzi ya mwajiri wake, usalama wa kazi yake hutegemea hilo.

Utumishi unamaanisha shughuli ambazo ni matokeo ya mwitikio wa nafasi ya chini kiutumishi na roho ya kujiitiisha chini ya mwingine. Uongozi kwa upande mwingine unamaanisha kuanzisha.

Inahusisha mwelekeo, ushawishi na hamasa. Unadai shughuli za awali kuhusika kiubunifu, shabaha na kuwajenga wengine kiasi kwamba kwa pamoja wanaweza kutoa tija zaidi kuliko mtu mmoja peke yake hangeweza kufikia.

Uongozi ni kujua unakokwenda na kuwa na uwezo wa kuwavumilia wengine waende pamoja nawe kama ambavyo Mungu katika nchi yetu alivyotupa mtu wake Rais John Magufuli, tunapaswa kumuombea.

Watu wanahamasishwa kutenda kwa ubora katika kutambua kwamba kila kitu kinatendwa kwa utukufu wa Mungu.

Wakolosai 3:23 inasema: “Lolote mlifanyalo, lifanyeni kwa moyo, kama kwa Bwana, wala si kwa wanadamu.”

Yesu kristo alifundisha makutano makubwa katika matukio mengi, lakini shabaha yake ilibakia katika kuwajenga wafuasi waliokuwa karibu naye zaidi.

Yesu alitumia miaka mitatu na nusu akidhihirisha nguvu ya ujumbe wake katika mahubiri yake na uponyaji na baadaye katika mauti yake ya kujitoa sadaka na ufufuo wake wa kimaajabu.

Alikuwa mfano hai wa ujumbe wake kwa wanafunzi wake.

Pale mwanzoni katika muafaka Yesu aliwapa wanafunzi wake fursa ya kushiriki huduma yake kwa kuwatuma kama wamishenari. Wakati huduma yao iliposhindwa Yesu alitoa maelekezo kwa wakati kusahihisha tatizo Mathayo 17:14-21.

Yesu aliwaandaa wanafunzi wake waweze kubeba uwepo wake wa kimwili.

Ni vyema viongozi wa nyumba za ibada wakakumbuka kwamba Mungu amewapa karama za kiroho.

Na hii ni dhamira kwamba hata waumini hutulia na kupata utosherevu katika huduma zinazotumia karama zao za kiroho.

Uwezo wetu Mungu aliotupa wa vipawa vya asili tunatakiwa tuwe makini wakati tunavitumia.

Kiongozi wa kiroho hutakiwi kutumia uwezo wa asili wa karama kushawishi waumini kupingana na serikali yao inayowaongoza.

Katika maisha ni vyema tukakubali kuongozwa na ukweli uliomo katika neno la Mungu.

Familia zetu ni sehemu ya Serikali hilo lifahamike wazi kwa viongozi wa dini.

Ufunguo wa mafanikio ya huduma katika kanisa na serikali ni urari. Wanafamilia zetu ndio wananchi wa Taifa hili, kwa hiyo kiongozi wa kidini unatakiwa kufahamu kwamba kujaribu kutenganisha familia, kanisa na serikali ni jambo ambalo haliwezekaniki kamwe.

Kwa hiyo mahubiri yetu yawe na maudhui yanayojenga zaidi wanafamilia ili zipate uelewa wa kuweza kushirikiana vyema na serikali yao halali.

Ukisoma kumbukumbu la torati 6:7 inasema: “Nawe uwafundishe watoto wako kwa bidii, na kuyanena uketipo katika nyumba yako, na utembeapo njiani, na ulalapo, na uondokapo.”

Vile vile katika Mithali 22:6 inasema hivi: “Mlee mtoto katika njia impasayo, naye hataiacha hata atakapokuwa mzee.”

Kwa maombi na mafundisho zaidi nitafute kwa 0754570451