Polisi Tanzania wakiri kuwajeruhi wanne kwa risasi Geita

Kamanda wa polisi mkoa wa Geita, Mponjoli Mwabulambo.

Muktasari:

Jeshi la polisi mkoani Geita limewajeruhi watu wanne kwa risasi kufuatia tukio la wananchi kuvamia kituo cha polisi cha  Nyawilimwilwa kilichopo wilayani Geita wakitaka kumtoa mtuhumiwa.

Geita. Watu wanne wamejeruhiwa kwa kupigwa risasi na polisi wilayani Geita, kufuatia vurugu zilizotokea wakati wa kugawa maeneo ya kijiji  cha Kibwela kata ya Nyawilimwilwa wilayani humo na kusababisha wananchi kuandamana na kuvamia kituo cha polisi wakitaka kumtorosha mtuhumiwa.

Mbali na watu hao wanne, jeshi hilo pia linawashikilia watu wengine wanne wanaotuhumiwa kushiriki katika vurugu hizo zilizo sababisha wananchi kuvamia kituo cha polisi.

Taarifa iliyotolewa na kamanda wa polisi mkoa wa Geita, Mponjoli Mwabulambo amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema limetokea jana Jumatano Januari 29, 2020 baada ya wananchi zaidi ya 300 kuvamia kituo cha polisi cha Nyawilimwilwa wakitaka kumtoa mtuhumiwa.

Kamanda Mwabulambo amesema wananchi wa kijiji hicho walikua wakipinga sera ya matumizi bora ya ardhi wakiongozwa na mwenyekiti wa kitongoji  cha Mkalale, Alex Abel aliyewahamasisha wananchi kupinga hatua za serikali zilizokuwa zikiainisha maeneo ya kijiji kwa kupanga matumizi bora ya ardhi.

“Polisi walipopata taarifa walifika na kukuta mabango yanayoonyesha matumizi bora ya ardhi yameondolewa na huyu mwenyekiti ndio alikuwa kiongozi polisi walimchukua wananchi walijihamasisha wakajipanga wakiwa na silaha za fimbo na mawe wakafika kituoni walitulizwa lakini hawakusikiliza na ndipo polisi wakatumia nguvu,” amesema Mwabulambo.

Kamanda amesema katika vurugu hizo watu wanne walijeruhiwa ambapo watatu risasi ziliwapata kifuani ambao ni Gervas Elisha (23), Juma Mashauri(33) na Samuel Misungwe huku Mateso Hoja (30) akijeruhiwa mkono wa kulia na wote wamelazwa katika hospitali ya mkoa wa Geita kwa matibabu.

 

Endelea kufuatilia mitandao ya Mwananchi kwa habari zaidi