Samia awaonya wanachama CCM

Makamu wa Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan

Muktasari:

Makamu wa Rais nchini Tanzania, Samia Suluhu Hassan amewaonya wanachama wa CCM walioanza kupita katika majimbo mbalimbali kutengeneza mazingira ya kupitishwa kuwania nafasi hiyo ya uwakilishi wa wananchi bungeni.

Dar es Salaam. Makamu wa Rais nchini Tanzania, Samia Suluhu Hassan amewaonya wanachama wa CCM walioanza kupita katika majimbo mbalimbali kutengeneza mazingira ya kupitishwa kuwania nafasi hiyo ya uwakilishi wa wananchi bungeni.

Ametoa onyo hilo leo Alhamisi Februari 13, 2020 katika maadhimisho ya miaka 43 ya kuzaliwa kwa chama hicho Mkoa wa Dar es Salaam.

Amesema chama hicho kina taratibu zake katika kusimamia uchaguzi na kwamba muda ukifika wote wataruhusiwa kutangaza nia na kuchukua fomu za kuwania nafasi mbalimbali katika uchaguzi ujao.

"Kuna fununu kwamba baadhi ya watu wameanza kujipitisha pitisha huko majimboni. Ninawaomba mfuate kanuni na taratibu za chama.”

" Kama wewe ni mchezaji, subiri filimbi ipigwe ndipo uanze kucheza, sio unaanza kucheza peke yako, filimbi ikipigwa mpira unakukuta uko golini, unatia,”amesema Samia.

Amewataka wanachama wa CCM kupendana na kwenda kwenye uchaguzi mkuu wakiwa wamoja.

Amesema kufarakana miongoni mwao ni chanzo cha kuwapa ushindi wapinzani.

Amesisitiza kwamba mtu anayefaa kugombea apewe nafasi hiyo badala ya kuondolewa sifa au kuvuliwa uanachama ili mradi asipate nafasi kwa sababu tayari viongozi wana watu wao.

"Mtu anafaa kugombea lakini anaandikiwa sifa mbovu, kisha anaenguliwa. Mwenendo huu hautupeleki kuzuri, tunapoelekea kwenye uchaguzi mkuu tushikamane ili twende pamoja, tushinde pamoja," amesema Samia.