Shughuli pevu kufukuzia kitambulisho cha Taifa

Wakazi wa Jiji la Dodoma wakiwa katika foleni ya kufuatilia vitambulisho vya taifa katika ofisi za Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) jijini humo. Picha na Habel Chidawali

Moshi. Zikiwa zimebaki siku tano kufikia siku ya ukomo wa usajili wa laini za simu kwa kutumia namba za kitambulisho cha Taifa, kitambulisho hicho kimeonekana kuwa lulu, lakini mbali na usajili wa simu usipokuwa nacho utakutana na ugumu katika katika kukamilisha mambo 10 siku za usoni.

Mateso wanayoyapata wananchi wasiokuwa na vitambulisho hivyo kwa sasa katika kuvifukuzia inatokana na kutaka kwao kuwahi kusajili laini za simu kwa njia ya alama za vidole.

Mwamko wa kutafuta kitambulisho cha Taifa umeonekana zaidi mwaka 2019 na Januari 2020, baada ya Mamlaka ya Mawasiliano (TCRA) kutangaza kuzima simu ambazo hazijasaliwa kwa alama za vidole.

Kwa mujibu wa TCRA hadi Januari 12, mwaka huu laini za simu milioni 26 ndizo zilizokuwa zimesajiliwa kati ya 48 milioni.

Ili uweze kusajili laini yako kwa mfumo wa alama za vidole, ni lazima uwe na kitambulisho cha Taifa au namba za kitambulisho hicho.

Upatikanaji wa kitambulisho hicho hupitia mchakato mrefu ikiwemo kuwasilisha vithibitisho vya uraia kama vyeti vya kuzaliwa au viapo ambavyo ni lazima vithibitishwe na Idara ya Uhamiaji.

Ingawa kwa sasa umuhimu wake unaonekana zaidi katika usajili wa simu, lakini ukweli ni kuwa unaweza kukutana na mateso siku za usoni utakapohitaji huduma nyingine katika taasisi mbalimbali kama huna kitambulisho hicho.

Unayoweza kukwama kwa kukosa kitambulisho hicho

Moja ya changamoto unayoweza kukutana nayo ni wakati utakapohitaji pasi ya kusafiria ya kielektroniki ambayo bila kuwa na kitambulisho cha Taifa huwezi kuipata, hii itakufanya ushindwe kusafiri.

Nyingine ni unapotafuta ajira serikalini, kusajili kampuni kwa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (Brella) na unapotafuta leseni ya udereva Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

Pia kitambulisho cha Taifa kitahitajika katika kutafuta leseni ya biashara, hati ya makazi, hati ya kiwanja, kumdhamini mtu polisi, mahakamani na unapotaka kuingia kwenye mifuko ya hifadhi za jamii.

Baadaye kuna mipango ya kuunganisha kanzi data ya Nida na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) ili itumike katika kuhuisha daftari la kupigia kura ili kitambulisho hicho kitumike kupigia kura.

Wadau wafunguka

Mkurugenzi wa Leopard Hoteli ya mjini Moshi, Priscus Tarimo akizungumzia umuhimu wa kitambulisho hicho alisema kina faida nyingi ikiwamo kumtambulisha mtu halisi na kuepukana na matapeli.

“Lakini kitambulisho hiki ni muhimu wakati wa kutafuta `passport (pasi ya kusafiria), kuziba mianya ya ukwepaji kodi na kuongeza mapato, kuondoa udanganyifu wa umri na kudhibiti uhalifu,”alisema.

Mkazi wa jijini Dar es Salaam, Ally Janja alisema kitambulisho hicho ni mihimu kwani ndicho kinachoonyesha utaifa wa mtu na pia kudhibiti uhalifu kitaifa na kimataifa.

Samson Mollel, mjasiriamali katika stendi kuu ya mabasi jijini Arusha alisema kitambulisho cha Taifa ni muhimu kwani kitasaidia kuwatambua Watanzania na wasio Watanzania na kudhibiti uhalifu.

“Mimi ni mhanga wa wizi wa mtandaoni na nilipokwenda polisi kumfuatilia mhusika hatukufanikiwa kwa sababu kitambulisho alichosajili nacho kilikuwa ni cha bandia. Hiki cha Nida ni baba lao,” alisema.

Wakili wa kujitegemea, Peter Mshikilwa alisema kitambulisho cha Taifa ndio uraia na kwamba kina faida nyingi na sasa kimekuwa ni muhimu hata katika kupata huduma katika taasisi za umma.

Mshikilwa alisema hata kwa mtu anayetaka kusajili kampuni Brella ni lazima awe na kitambulisho cha Taifa vinginevyo kampuni haiwezi kusajiliwa akiongeza hilo litasaidia kuwajua wanahisa halisi.