Siri za mahaba ya Mugabe na Tanzania

Kama kuna Mtanzania ambaye alikuwa hafahamu namna Rais mstaafu wa Zimbabwe, Robert Mugabe alivyokuwa akiipenda Tanzania, afuatilie simulizi fupi ya Rais mstaafu wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi.

Mbali na hiyo mwaka 2014, Mugabe alielezea kusikitishwa kwake na namna viongozi wa Afrika walivyoshindwa kumuenzi Mwalimu Julius Nyerere kutokana na mchango wake wa kuzikomboa nchi za Afrika.

“Ninataka kusema, mashujaa wengi wa Afrika wamepewa heshima, lakini mtu aliyefedheheshwa ni Mwalimu Julius Nyerere. Tulikuwa pale, tulifanya harakati za ukombozi pale na tulitegemea rasilimali za Tanzania, lakini hakuna kinachozungumzwa kuhusu huyu mtu na nchi yake katika Umoja wa Afrika,” alisema Mugabe katika moja ya mikutano na viongozi wa Afrika.

Mwaka 2015 jijini Harare nchini Zimbabwe, Mugabe alizindua kitabu kilichoitwa ‘Julius Nyerere, Asante Sana, Thank you Mwalimu.’ Ni kitabu kilichochapishwa na kituo cha utafiti na vielelezo cha kusini mwa Afrika (SARDC) chenye masimulizi mengi kuhusu Nyerere na Tanzania.

Katika kuunga mkono hayo, Rais mstaafu Mwinyi ametoa simulizi kuhusu uungwana wa Mugabe wa kufikia hatua ya kugawana umaskini wake na Tanzania, baada ya kupokea taarifa za kifo cha kiongozi huyo

kilichotokea Ijumaa iliyopita nchini Singapore alipokuwa akipatiwa matibabu.

“Akufaaye kwa dhiki ndiye rafiki. Rafiki yetu sisi wa kwanza kabisa ni ndugu Mugabe,” ni kauli ya Mwinyi akielezea namna Mugabe alivyoisaidia fedha Tanzania.

Mwinyi anasema alipochukua uongozi wa nchi mwaka 1985 kutoka kwa Mwalimu Nyerere aliikuta Hazina ya Taifa ikiwa haina kitu.

“Nilikwenda kwa Mwalimu Nyerere kumpa hali hiyo, na akanishauri kwamba tuna marafiki duniani, akiwamo komredi Mugabe, Rajiv Gandhi na wengine wengi, ‘hebu jaribu kuzungumza nao hawa’” anasema Mwinyi kwenye video aliyorekodiwa akizungumzia umuhimu wa Mugabe Tanzania.

Rajiv Gandhi alikuwa waziri mkuu wa sita wa India, kuanzia mwaka 1984 hadi alipouawa mwaka 1989. Alichukua nafasi hiyo baada ya waziri mkuu wa wakati (ambaye ni mama yake), Indira Gandhi kuuawa kwa kupigwa risasi na mmoja wa walinzi wake mwaka 1984.

Mwinyi anasema Hazina ilikauka kutokana na fedha nyingi kutumika kununulia silaha kwa ajili ya kuikomboa nchi wakati wa vita vya Kagera mwaka 1978-1979.

Anasema, pia hali hiyo ilitokana na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) kumsusia Mwalimu Nyerere kumkopesha fedha kwa kuwa alikataa masharti yao. “Lakini, akaja akatusaidia ndugu Mugabe tukaanza maisha.”

“Nakumbuka nilituma watu wawili mmoja wapo (Benjamin) Mkapa na ndugu Salim (Dk Salim Ahmed Salim), ama nimesahau lakini mmoja wapo kati ya hao alikwenda kwa Rajiv na mwingine kwa Mugabe kumuomba msaada.

“Mmoja wapo kati ya Mkapa au Salim akarudi hapa na kitita kizuri kabisa cha fedha ikawa ndiyo fungate yetu. Sasa kwa haya Waswahili wanasema akufaaye kwa dhiki ndiye rafiki. Rafiki yetu sisi wa kwanza kabisa ni ndugu Mugabe,” anasema Mwinyi.

“Tanzania imepoteza mtu mpenzi wa nchi yetu, tuna kila sababu ya kusema alitusaidia katika siku za dhiki, maana miaka hiyo ya 1985 karibu nchi zote za Kiafrika zilikuwa masikini, lakini tukagawana umasikini wake na sisi wenziwe.”

Mapenzi ya Mugabe kwa Tanzania yalijidhihirisha alipokuwa akizindua kitabu ambacho kimekusanya hotuba mbalimbali za Mwalimu Nyerere na hasa kuhusu ukombozi wa nchi za Afrika.

Kitabu hicho kilizinduliwa ikulu mjini Harare nchini Zimbabwe wakati huo Mugabe alikuwa bado yuko madarakani, alisema Mwalimu ni nembo adhimu ya uhuru na umoja na kwamba kitabu hicho kimejumuisha maeneo mengi ikiwamo juhudi za Afrika katika kupigania uhuru wa kisiasa.

Mugabe alisema Mwalimu amefanya mengi katika kubeba mzigo wa nchi za Afrika wakati wa kutafuta uhuru. “Alijitoa na kuhangaika sana. Alikuwa mtu wa kweli ambaye hakuna wa kulingana naye,” alisema Mugabe.

“Nimefurahi sana kusikia kuwa jengo linalojengwa katika Umoja wa Afrika litakalotumiwa na baraza la usalama kupewa jina la Mwalimu Julius Nyerere,” alisema Mugabe ambaye ndiye alipendekeza jina hilo alipokuwa mwenyekiti wa Umoja wa Afrika.

Mugabe aliongeza kuwa Mwalimu pia alikuwa kiunganishi cha nchi za Afrika kwa China. Taifa hilo lilikuwa msaada mkubwa kwa nchi za Afrika.

“Nchi za magharibi zitajisingizia, zitadai, zitaadhibu lakini angalia mashariki (Mashariki ya mbali), una rafiki ambaye wakati wote anajihisi kama wewe, rafiki anashirikiana na wewe katika juhudi zako. Tunafuata nyayo za Mwalimu kuelekea mashariki. Leo uhusiano wetu na China umeimarika. Kitabu kinamwelezea mwanasiasa mkubwa mwenye weledi, mpiganaji na mzalendo wa kweli,” alisema Mugabe.

Mugabe alimwelezea Mwalimu Nyerere kwamba ni mtu aliyechangia harakati za ukombozi kwa nchi za mashariki ya kati ya Afrika, mwasisi wa Umoja wa Nchi Huru za Afrika. Imani ya Mwalimu ilikuwa uhuru utapatikana ikiwa watu watashirikiana.

Alisema kulikuwa na mkutano uliofanyika Geneva nchini Uswisi lakini kabla ya kwenda huko, Mwalimu Nyerere aliwakutanisha baadhi ya viongozi wa Afrika jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kuweka msimamo wa pamoja na matokeo ya mkutano huo ni kuanzishwa kundi la nchi za mstari wa mbele 1976.

“Tuliamua kwamba hakuna haja ya kuwavunja moyo wale waliotusaidia. Pia, Mwalimu alikuwa na sifa nyingine ya kuunganisha watu wake. Aliunganisha Tanganyika na Zanzibar,” alisema Mugabe na kuongeza kuwa Mwalimu alikuwa mtu asiyetetereka, kiongozi mwenye maono aliyesimama na wote katika mapambano ya ukombozi wa kusini mwa Afrika.

Mugabe anasema wakati wa kuanzishwa OAU, Mwalimu alifurahishwa na hatua hiyo ya kuanzishwa jumuiya hiyo na alitoa fursa ya Dar es Salaam kuwa mwenyeji wa mkutano wa kamati ya ukombozi ya OAU.

“Dar es Salaam ikiwa ni kituo ambako tulienda kwa ajili ya mafunzo, miongozo na mambo mengine,” alisema Mugabe.

Alisema ni Mwalimu ndiye aliwezesha yeye (Mugabe) kuwa na uhusiano na Mwenyekiti Mao Zedong wa China na kukajengwa reli kati ya Tanzania na Zambia (Tazara). “Leo, ushirikiano wa China na Afrika umekolezwa na FOCAC (Jukwaa la ushirikiano wa China na Afrika) na hii imetokana na Mwalimu aliyeasisi uhusiano na China.”

Mugabe alimwelezea Mwalimu kama ni mtu aliyejitoa katika ukombozi, umoja na maendeleo ya Afrika akisisitiza kwamba uongozi wake ni kioo cha jamii, mzalendo na anayestahiki heshima kubwa.

Akisisitiza umuhimu wa Mwalimu hilo Mugabe alirudia kwenye mkutano wa 35 wa viongozi wa nchi na serikali wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC), uliofanyika Gaborone,Botswana.

Alizitaka nchi za Afrika kuwaenzi wale waliojitoa kupigania ukombozi wa bara la Afrika. “Tuwakumbuke wale waliotuachia urithi huu. Hii inaweza kuwa ni kitu, je, tunaweza kuwa na fedha za kulipa fadhila zao,” alihoji Mugabe.

Mugabe aliwataka viongozi wenzake kuwa na utaratibu mahsusi wa kuenzi urithi wa waasisi kama vile Rais wa zamani wa Tanzania, Julius Nyerere, Rais wa zamani wa Zambia, Kenneth Kaunda na Rais wa zamani wa Botswana, Seretse Khama (ambaye kwa sasa ni marehemu), wametoa mchango mkubwa wa kuongoza ukombozi kwa Afrika.

“Ninataka sisi Wazimbabwe tusimame kwa ajili ya Nyerere. Afrika lazima ikumbushwe wajibu wa kumuenzi Nyerere, alibeba mzigo wa mafunzo kwa wapigania uhuru.

“Mwisho wa siku hakuna hata mmoja anayezungumzia Tanzania kwamba inastahiki kutajwa. Hata kutaja kidogo kwa kukamilisha kazi, kazi ya kutufanya tuwe marafiki, kazi ya kutoa mafunzo kwa wapigania ukombozi wa Afrika. Wote tulikwenda kwa njia mbalimbali, maeneo tofauti nchini Tanzania kwa ajili ya kuzikomboa nchi zetu na hatujarudi Tanzania,” alisema Mugabe.