TLS yapata hofu mabadiliko ya sheria kutikisa utendaji wake wa kazi

Sunday January 19 2020Mkurugenzi wa Twaweza, Aidan Eyakuze

Mkurugenzi wa Twaweza, Aidan Eyakuze 

By Khalifa Said, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Kamati ya Bunge ya Sheria na Katiba imewaalika wadau wa sheria kuchangia marekebisho katika Sheria ya Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS) yanayoleta hofu ya kuathiri uhuru katika utendaji kazi wa chama hicho.

Katika marekebisho ya sheria Na. 8 ya mwaka 2019 yanapendekeza kufanyika mabadiliko ya sheria ya TLS pamoja na mabadiliko ya sheria za Serikali za Mitaa (Mamlaka ya wilaya) na Mamlaka za Miji.

Muswada huo ulikuwa bado haujawekwa katika tovuti ya Bunge mpaka jana, lakini gazeti la Mwananchi liliona nakala yake na inaonekana mabadiliko hayo japo ni madogo, yatakuwa na athari kwa TLS.

Marekebisho hayo yanajikita katika kuweka vikwazo kwa sifa ya uanachama wa Baraza la TLS, kuanzishwa kwa ukomo wa wajumbe wa baraza ambao utakuwa ni mihula miwili kila mwaka na kuanzishwa kwa utoaji wa hesabu na ripoti kuhusu TLS ambapo ripoti za ukaguzi, ripoti za mwaka na taarifa za mikutano mikuu zitatakiwa kupelekwa kwa Waziri anayehusika na masuala ya sheria.

Mapendekezo mengine kwa sheria hiyo ni pamoja na kuanzishwa kanuni zitakazotawala kazi za mkutano mkuu wa TLS ambao sasa hautajumuisha wanachama wote bali mahudhurio yatakuwa ya uwakilishi.

Pia mapendekezo yanataka mikutano mikuu iwe inafanyika wiki ya pili ya Aprili ambapo kwa utaratibu wa sasa wajumbe 15 wa chama hicho wanaweza kuitisha mkutano mkuu, lakini mabadiliko yanataka theluthi moja ya wanachama wenye msimamo mmoja wakihusisha asilimia sawa ya uwakilishi kutoka kila kikundi cha ndani ya chama hicho wanaweza kudai mkutano huo.

Advertisement

Katika uchambuzi wao, Twaweza ambayo ni asasi isiyokuwa ya kiraia imetaka kurekebishwa kwa vifungu vya 52-61 kwa kifungu kimoja kikieleza “utawala na utendaji wa chama ni mambo ya chama husika na hivyo hayapaswi kudhibitiwa na chombo kingine cha Serikali.

Mkurugenzi wa Twaweza, Aidan Eyakuze alisema jana kuwa mabadiliko hayo yamemshtua kwa sababu Serikali inataka kuchukua udhibiti wa masilahi katika uhuru wa taasisi hiyo ambayo hulinda na kuhakikisha kuwepo kwa utawala wa sheria na utawala bora.

“Nadhani kwa kuweka mapendekezo ya mabadiliko hayo kwenye sheria ni kuingilia uhuru na umoja wa chama na ujumbe wetu kwa kamati ni kuhakikisha uhuru huo unalindwa,” alisema.

Mabadiliko hayo kwa sheria ya TLS yanafuatia mengine ya mwaka 2018 yaliyoanzisha vikwazo vya mtu anayetakiwa kuwa mjumbe wa Baraza la Utawala wa chama hicho. Moja kwa moja mabadiliko hayo yamekataza watumishi wa umma na wanasiasa kuwa kwenye nafasi hiyo.

Advertisement