Uenyekiti wa Mbowe unavyotikisa ndani, nje

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe

Mwanza. Desemba 18, Freeman Mbowe atakuwa akisubiri matokeo ya uchaguzi wa mwenyekiti wa Chadema, akiwa na matumaini ya kurejea madarakani kuongoza kwa kipindi kingine cha miaka mitano.

Uenyekiti wa Mbowe umekuwa ukizua mjadala ndani na nje ya chama hicho kikuu cha upinzani nchini jambo ambalo limewafanya wachambuzi kuja na mawazo tofauti.

Huku zikiwa zimebaki siku kama sita kabla ya uchaguzi wa mwenyekiti wa chama hicho, hali ni tofauti na ilivyokuwa Septemba 15, 2014 wakati Mbowe aliposhinda kwa kupata kura 789-- sawa na asilimia 97.3-- akimshinda Gambaranyera Mongateo aliyepata kura 20 tu.

Safari hii mjadala wa kumtaka apishe wengine, ambao hasa ulitoka nje ya chama, sasa umejipenyeza ndani kiasi cha kujikuta akirushiwa lawama kuwa anataka ashikilie milele nafasi hiyo kutoka kwa baadhi ya wanachama na hata aliyekuwa mjumbe wa kamati Kuu, Frederick Sumaye, ambaye ameamua kujivua madaraka yote na kujitoa ndani ya Chadema.

Si mara ya kwanza kwa suala la kugombea nafasi ya uenyekiti kutikisa Chadema tangu Mbowe awe kiongozi wa chama hicho mwaka 2004.

Aliyekuwa naibu katibu mkuu wa chama hicho, Zitto Kabwe alizua sintofahamu alipojitosa kugombea uenyekiti mwaka 2009, hali ambayo ilitishia kupasua chama hicho baada ya kuibuka kwa makundi.

Hata hivyo, joto hilo lilitulia baada ya Baraza la Wazee la Chadema kuingilia kati kwa kumsihi Zitto kujitoa kwenye kinyang’anyiro hicho akiahidiwa kuwa angepewa nafasi ya kugombea uchaguzi unaofuata yaani 2014.

Kabla ya mwaka huo wa uchaguzi, Zitto alifukuzwa pamoja na wenzake jambo ambalo lilimfanya Mbowe kutokuwa na upinzani mkali katika uchaguzi wa mwaka 2014 hivyo kushinda kwa asilimia 97.3 dhidi ya Mongateo.

Ingawa majina ya wanaogombea nafasi hiyo ya uenyekiti mwaka huu bado hayajatangazwa, Sumaye na Cecil Mwambe walijitangaza wenyewe kuwania nafasi hiyo kumpinga Mbowe. Tayari Sumaye amejitoa katika chama hicho.

Hata hivyo, gumzo limekuwa ni kubwa, likimtaka mbunge huyo wa Hai, Mbowe apishe wengine hata kama katiba ya Chadema inampa fursa ya kuendelea kugombea kama haki yake ya kidemokrasia.

Wako wanaosema kama Chadema inapambania demokrasia na utamaduni wa kupokezana vijiti, Mbowe hana budi kuthibitisha hilo kwa kutogombea tena uenyekiti na kupisha wengine, lakini wanaomtetea wanasema katiba haijaweka ukomo na bado wanamuhitaji, hasa baada ya kuonyesha ustahimilivu katikati ya magumu.

Hadi sasa, Mbowe, ambaye alichukuliwa fomu na vijana wa chama hicho kwa ajili ya kutetea nafasi yake, hajaweka bayana msimamo wake kuhusu mjadala huo.

Lakini tofauti hiyo ya misimamo inaonekana wazi kwa wanasiasa, wasomi na hata watu wengine walioamua kutumia mitandao ya kujamii kueleza fikra zao za kumuunga mkono Mbowe au kumpinga.

“Pengine kelele za ukomo wa uongozi ndani ya Chadema zinachangiwa na chama hicho kujipambanua kuwa cha kidemokrasia,” anasema mhadhiri wa zamani wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Onesmo Kyauke.

“Ni wajibu wa wana-Chadema kujenga misingi na mfumo wa kupokezana kijiti katika ngazi zote ikiwemo nafasi ya uenyekiti wa Taifa.

“Kufanya hivyo ndiko kutawapa na kuwajengea uhalali wa kutetea na kudai demokrasia ikiwemo kulindwa kwa misingi ya kikatiba ya ukomo wa uongozi nje ya chama.”

Mchambuzi huyo wa masuala ya kisiasa anasema vyama vya upinzani vinavyotoa ushindani kwa CCM katika uongozi wa Taifa, vina wajibu wa kulinda, kutetea na kutekeleza kivitendo demokrasia ndani ya vyama vyao.

Ameonya kuwa ni hatari kwa demokrasia na mfumo wa kupokezana kijiti kwa watu kutumia hoja ya kiongozi kupendwa kukaa madarakani kipindi kirefu kwa sababu iko siku hoja hiyo itatumiwa vibaya kwa maslahi ya kundi dogo lenye ushawishi.

“Ni hatari demokrasia ya kupokezana vijiti kukosekana ndani ya vyama vya upinzani kwa sababu CCM yenye wabunge wengi, inaweza kutumia hoja ya kiongozi kupendwa na wananchi kubadili Katiba kuondoa ukomo wa urais,” anasema Dk Kyauke.

Lakini wanaopingana na hoja hiyo wanaona shinikizo la kumtaka Mbowe asigombee linatoka kwa watu ambao hawamo ndani ya Chadema na wanaohofia kuendelea kukua kwa chama hicho.

“Simtetei Mbowe wala sina nia ya kuingilia mchakato wa uchaguzi ndani ya Chadema,” alisema mwenyekiti wa Chaumma, Hashim Rungwe alipoulizwa na Mwananchi kuhusu suala hilo.

“Ila inashangaza kusikia na kuona kelele nyingi zinapigwa kuhusu uenyekiti wa Mbowe wakati wapo viongozi wa vyama vingine waliokaa madarakani kipindi kirefu kuliko yeye.”

Rungwe alisema wako viongozi walioongoza vyama kwa muda mrefu kuliko Mbowe, akitoa mfano wa Profesa Ibrahim Lipumba wa CUF, John Cheyo (UDP) na Agustino Mrema wa TLP.

“Hawa nadhani hawapigiwi kelele kwa sababu vyama vyao si tishio kwa CCM,” alisema Rungwe ambaye pia ni wakili wa kujitegemea.

Rungwe amewapa changamoto wanaohoji demokrasia ya uchaguzi ndani ya Chadema katika nafasi ya uenyekiti kufanya hivyo pia kwa kuhoji upatikanaji wa wagombea wa uenyekiti na umakamu ndani ya CCM.

Mawazo hayo yanafanana na ya mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine (Saut) jijini Mwanza, Dk Peter Mataba ambaye anasema Chadema wanapaswa kuwa makini na kelele zinazotoka ndani au nje ya chama kuhusu kiongozi wao ambaye wanamuamini na kumhitaji.

“Kwenye siasa, kuna siasa halisi na siasa za figusu zenye mbinu ya kudhoofisha mshindani,” alisema Dk Mataba.

“Sijafuatilia zaidi hoja za kumpinga Mbowe, lakini kama wana-Chadema wanamhitaji na katiba yao inamruhusu, nadhani kumpinga ni kutimia kwa usemi wa wahenga kuwa ‘mti wenye matunda ndio unaorushiwa mawe’.”

Hoja hiyo pia ilizungumzwa na mwanafunzi wa sheria na mchambuzi wa masuala ya kisiasa na kijamii, Edwin Soko.

“Chadema wasipangiwe nani awaongoze, waachwe wajichagulie viongozi wao wenyewe. Kama bado wanaamini Mbowe ndiye anawafaa wasiingiliwe kwa sababu katiba yao inawaruhusu,” alisema Soko.

Soko, ambaye pia ni mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa Habari cha Mwanza na mtetezi wa haki za binadamu, alisema hoja kinzani kuhusu demokrasia ndani ya chama kimoja, inapotoka chama kingine ni ishara ya kutafuta mbinu za kukidhoofisha chama husika. “Chini ya Mbowe, Chadema imeimarika kwa kuongeza idadi ya wabunge hadi kufikia 49 mwaka 2016, wameshinda na kuongoza halmashauri kadhaa katika miji mikuu huku wakichukua uongozi wa kambi rasmi ya upinzani bungeni,” alisema Soko.

“Wawe (Chadema) makini na hoja ya muda wa uongozi wa Mbowe na wajifunze kutoka kwa upinzani Kenya ambao wamempa Raila Odinga uongozi wa tangu enzi ya Daniel Arap Moi, Kibaki na sasa Uhuru Kenyatta kutokana na uwezo wake kuhimili mikiki ya siasa za upinzani.”

Anasema uongozi na hasa nafasi ya uenyekiti wa vyama vikuu vya upinzani vinavyojipambanua kuwania kushika dola, unahitaji watu madhubuti, imara, wenye misimamo isiyoyumba na wastahimilivu wa dhoruba za kisiasa, sifa ambazo anasema zimeonyeshwa na Mbowe tangu baada ya uchaguzi mkuu wa 2015.

Freeman Aikaeli Mbowe alichaguliwa kwa mara ya kwanza kuwa mwenyekiti wa Chadema mwaka 2004 kumrithi Bob Makani. Mwaka 2005 aligombea urais na kushika nafasi ya tatu. Aliwahi kuwa mbunge wa Hai mwaka 2000 na akarejea kushika nafasi ya uenyekiti mwaka 2009 na 2014 akiwa pia mbunge.

Profesa Ibrahim Lipumba ameongoza CUF tangu apokee kijiti kutoka kwa Shaaban Mloo mwaka 1995. Mwaka 2015 alijivua vyeo vyote kutokana na kutokubaliana na CUF kukubali kuungana na vyama vingine kumuachia Edward Lowassa kugombea urais kwa tiketi ya upinzani.

Profesa Lipumba alirejea madarakani mwaka 2016, akifuta barua yake ya kujiuzulu na hivyo kuibua mgogoro mkubwa uliosababisha chama hicho kugawanyika. Amekuwa akigombea urais tangu mwaka 1995.

Augustine Lyatonga Mrema amekuwa mwenyekiti wa TLP tangu mwaka 1999 alipotokea NCCR-Mageuzi, chama alichojiunga nacho mwaka 1995 akitokea CCM. Aligombea urais mwaka 2000 na 2005 kwa tiketi ya TLP. Ni waziri wa zamani wa Serikali ya Awamu ya Pili. Ameshawahi kuwa mbunge wa Temeke na Vunjo ambako mwaka 2015 alishindwa na James Mbatia, ambaye ni mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi.

John Cheyo amekuwa mwenyekiti wa chama cha UDP tangu kilipoanzishwa mwaka 1992. Amewahi kuwa mbunge wa Jimbo la Bariadi hadi mwaka 2015.