Umoja wa Mabunge duniani watoa tamko zito sakata la Lissu

Moshi. Umoja wa Mabunge Duniani (IPU) umetoa tamko kuhusu sakata la mbunge bwa zamani wa Singida Mashariki, Tundu Lissu likipendekeza kuundwa kwa jopo la wajumbe watakaomsindikiza kurejea nchini.

Chombo hicho pia kimeeleza kushangazwa na kitendo cha Bunge la Jamhuri ya Muungano kutounda kamati kuchunguza shambulio dhidi ya Lissu wakati alipata tatizo hilo akitokea katika shughuli za kibunge.

Lakini Spika Job Ndugai naye amemshangaa Lissu kwa kupeleka malalamiko yake IPU wakati suala lake liko mahakamani na huku akijua kuwa chombo hicho hakina uwezo wa kisheria kutekeleza maamuzi yake.

Lissu, ambaye pia alikuwa Mnadhimu wa Kambi ya Upinzani Bungeni, alitangaza kurejea nchini Septemba 7, 2019, lakini baadaye akafuta mpango huo kwa kile alichodai kuwa ni sababu za kiusalama.

Lissu alishambuliwa kwa risasi zipatazo 30 akiwa ndani ya gari, nje ya makazi yake jijini Dodoma Septemba 7, 2017 na siku hiyo usiku alihamishiwa Hospitali ya Nairobi nchini Kenya kutoka Hospitali ya Mkoa wa Dodoma. Baada ya hali yake kuimarika, alihamishiwa Ubelgiji kwa ajili ya kurekebisha mifupa iliyoharibiwa na risasi.

Lakini akiwa Ubelgiji, Spiga Ndugai alitangaza kiti chake kuwa wazi kwa maelezo kuwa hajulikani alipo na hakujaza fomu za mali na madeni.

Jana, alipoulizwa kuhusu taarifa ya IPU, Ndugai alisema atatoa taarifa Ijumaa, siku ambayo Bunge litaahirisha shughuli zake.

“Sijaliona (tamko la IPU) kabisa, lakini nikiliona nitakuwa tayari kueleza, nitatoa ufafanuzi,” alisema Ndugai.

“Cha muhimu ni kwamba IPU ni umoja wa mabunge yaliyo chini ya mwamvuli wa mfumo wa Umoja wa Mataifa, si chombo cha uchunguzi.

“Nisiseme sana nitasema keshokutwa. (Lissu) amepeleka kesi mahakamani sasa IPU itaingiliaje mambo ya ndani ya nchi ambayo yanahusisha mahakama?”

Uamuzi wa IPU kupendekeza kuundwa kwa kamati ndogo ya kumsindikiza Lissu, umetolewa na Kamati ya Haki za Binadamu ya IPU baada ya kusikiliza malalamiko yake.

Kamati hiyo pia ilisikiliza malalamiko ya wabunge 90 wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) ambao ubunge wao ulibatilishwa na pia ilitoa maamuzi dhidi ya malalamiko ya wabunge kutoka nchi za Ecuador, Venezuela, Maldives, Mongolia, Philippines, Israel na Palestina.

Kuundwa kwa kamati ndogo

Katika moja ya maamuzi nane ya kamati, kwa mujibu wa taarifa rasmi ya IPU iliyosambaa mitandaoni jana, ni pendekezo la kumsindikiza Lissu.

“Kamati inaamini kuzuru Tanzania kutatoa fursa muhimu kukutana na Serikali, Bunge na mahakama au mtu yeyote atakayesaidia kutoa uelewa wa suala hilo la kurejea kwa Lissu,” inasema.

Inasema kamati inaamini kwamba mamlaka ya Bunge la Tanzania itajibu maombi ya kamati hiyo ya IPU iliyokutana Geneva, Uswisi kati ya Januari 20 hadi 30.

Kamati pia imekubali kuwa malalamiko ya Lissu yanakubalika chini ya kanuni za uchunguzi na uamuzi wa malalamiko za IPU na ina mamlaka ya kuchunguza.

Mbali na hilo, kamati hiyo imesikitishwa na jaribio la mauaji dhidi ya Lissu na tuhuma dhidi ya mamlaka katika jaribio hilo ambalo imesema Lissu alinusurika kimiujiza.

Kamati hiyo imesema ni jambo linalolatiza kwamba Lissu alivuliwa ubunge wake wakati ilikuwa wazi kwa Bunge na umma kwamba Lissu alikuwa nje kwa matibabu kutokana na shambulio hilo.

“Kamati inapongeza hatua za haraka zilizochukuliwa kumpeleka eneo salama na kuhakikisha anapata matibabu, lakini inataka kujua Bunge lilichukua hatua gani kufuatilia uchunguzi,” inasema.

Hivyo kamati inasema inapenda kupata maoni kutoka kwa mamlaka ya chombo hicho cha kutunga sheria kuhusu sababu Lissu avuliwe ubunge.

Kamati hiyo pia inataka kupata taarifa rasmi ya Serikali kuhusu ukweli na uhalali wa kisheria kuhusu kila hatua inayohusu kukamatwa kwake na kushitakiwa mahakamani.

Kamati hiyo poia inasema inatambua Lissu anataka kurejea Tanzania haraka, hivyo imeshauri kuundwe kamati ndogo ambayo itamsindikiza hadi Tanzania siku atakapokuwa akirejea.

Kamati imemuomba katibu mkuu wa IPU kuwasilisha uamuzi huo kwa mamlaka ya kibunge ya Tanzania na kuomba ruhusa ya kutembelea Tanzania kama ilivyopendekezwa.

Pia Kamati itaendelea na uchunguzi wa malalamiko hayo katika kikao chake kijacho.

Uamuzi huo umepokelewa kwa furaha na Lissu.

“Ushauri wangu ni kwamba wabunge wetu wote ambao wameathiriwa na vitendo hivi wawasilishe malalamiko yao kwa IPU ili yachunguzwe,” alisema.

“Mtaona katika taarifa hiyo jinsi ambavyo malalamiko kutoka sehemu mbali mbali duniani, ikiwemo Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, yameshughulikiwa”.

Lissu alisema kufanya hivyo kutaongeza shinikizo kwa watawala na uongozi wa Bunge ili angalau vyombo hivyo na wananchi wajue vitendo vya ukiukaji haki za wabunge vinamulikwa duniani.

Vitisho na kukamatwa

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Lissu aliwasilisha malalamiko sita kuhusu ukiukwaji wa haki za binadamu, vitisho na kukamatwa.

Pia alilalamikia kutokuwepo kwa mwenendo wa haki wa vikao vya Bunge la Tanzania, kuminywa kwa uhuru wa kutoa maoni na kujieleza na kukiukwa kwa haki ya mikusanyiko.

Katika malalamiko yake, Lissu alieleza jinsi alivyonusurika kifo aliposhambuliwa na watu wasiojulikana nje ya nyumba za viongozi wa serikali yenye ulinzi wakati wote, lakini siku hiyo walinzi hawakuwepo.

Kwa ufupi, pia ameelezea alivyovuliwa ubunge Juni 2019 kutokana na kutokuwepo bungeni, ilihali ilikuwa wazi kwa umma kuwa alikuwa nje ya nchi kwa matibabu.

Lissu alieleza kuwa Spika wa Bunge la Tanzania na Naibu Spika na baadhi ya mawaziri wa Serikali ya Tanzania ndio waliofanya uamuzi wa kumpakiza ndege kwenda Kenya kwa matibabu.