Wagombea CCM walivyopita chujio uchaguzi wa 1980

Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamini Mkapa akizungumza katika mkutano wa Rais John Magufuli na viongozi wakuu wastaafu uliofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam, juzi. Picha na Ikulu

Kamati ya shughuli za Tanu ilikutana mjini Dar es Salaam Septemba 2, 1980 kwa ajili ya kutayarisha mambo yatakayofikishwa mbele ya kikao cha Kamati Kuu ya CCM iliyokutana Septemba 8 na 9.

Miongoni mwa mambo hayo ni majina ya wagombea ubunge yaliyojadiliwa na kupendekezwa na kamati za utendaji za wilaya na mikoa na kamati za utekelezaji za jumuiya tano za chama hicho ambacho ndicho pekee kilikuwa kikifanya shughuli za siasa wakati huo.

Kikao cha kamati hiyo kilichofanyika chini ya uenyekiti wa Mwalimu Julius Nyerere, kilipendekeza majina ya wagombea ubunge wa wilaya 111 na wagombea ubunge wa Taifa kutoka mikoa 25 ya Tanzania na jumuiya tano za CCM ambazo ni Juwata, Washirika, Wazazi, Vijana na UWT.

Kamati hiyo pia ilijadili na kupendekeza majina ya wagombea ubunge kutoka Baraza la Wawakilishi Zanzibar.

Kwa utaratibu ulivyokuwa, kati ya wabunge 32 wa Baraza la Wawakilishi, 22 walichaguliwa baraza hilo na kumi walitoka nje, yaani mmoja kutoka kila wilaya za Tanzania Visiwani.

Kikao cha Kamati ya Kudumu ya Shughuli kilikuwa mwanzo wa vikao vya Taifa vya kujadili majina ya walioomba kugombea ubunge.

Majina ya waombaji hao yalikuwa yamewasilishwa kwa kamati hiyo wilaya, mikoa na Jumuiya za chama.

Kamati za utendaji za wilaya zilifanya vikao vyake vya kuwajadili waombaji ubunge Agosti 23 na 25 na kamati za utendaji za mikoa zilikutana Agosti 26 kwa shughuli hiyo.

Wakati hayo yakiendelea, mkurugenzi wa uchaguzi, Elias Kazimoto alitangaza kuwa tume yake imeongeza muda wa kampeni za wagombea ubunge wa wilaya kuanzia Oktoba Mosi badala ya Oktoba 13 kama ilivyokuwa imepangwa awali.

Visiwani Zanzibar, kamati maalumu ya Kamati Kuu ya CCM iliyosimamia shughuli zote za Serikali iliketi mjini Dar es Salaam Septemba 6 kupendekeza majina ya watu wanaofaa kugombea urais wa Zanzibar.

Kulingana na kifungu cha 63(3) cha katiba ya CCM, wakati uchaguzi unapowadia, kamati maalumu ya kamati kuu ambayo ina jukumu la kuangalia na kusimamia shughuli zote za Serikali kwa upande wa Zanzibar, ilifanya uteuzi wa mwanzo wa majina ya watu wanaofaa kugombea urais wa Zanzibar.

Septemba 12, Halmashauri Kuu ya CCM ilimteua Aboud Jumbe kuwa mgombea pekee wa kiti cha urais katika uchaguzi huo.

Wakati huo, Jumbe alikuwa ni Rais wa Zanzibar, mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi na makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Hii ilikuwa ni mara ya kwanza kwa Rais wa Zanzibar kuchaguliwa kwa kupigiwa kura tangu mapinduzi ya mwaka 1964, na mara ya kwanza tangu Zanzibar ilipopata katiba yake.

Wakati Halmashauri Kuu ya CCM ikikutana, tayari ilikuwa imeshajulikana kuwa watu milioni 6.88 walikuwa wamejiandikisha kupiga kura.

Taarifa hiyo ilitolewa na Kazimoto aliyesema makadirio yalikuwa ni watu milioni nane.

Idadi ya 1980 ya waliojiandikisha kupiga kura ilikuwa na ongezeko la watu milioni 1.3 ikilinganishwa na waliojiandikisha mwaka 1975.

Ongezeko hilo ni asilimia 23.4 kutoka idadi ya wapigakura milioni 5.57 ya mwaka 1975.

Miongoni mwa majina yaliyoteuliwa na Halmashauri Kuu ya CCM Septemba 12 ni Edward Sokione, ambaye baadaye akawa Waziri Mkuu na Jackson Makweta (Waziri wa Nchi Katika Ofisi ya Waziri Mkuu).

Wawili hao walipita bila kupingwa, Sokoine akichukua jimbo la Monduli na Makweta jimbo la Njombe.

Mkoani Dar es Salaam, waliopitishwa na mkutano huo walikuwa ni Kitwana Kondo (alama ye jembe) na Martha Weja (alama ya nyumba).

Katika Wilaya ya Kinondoni waliopitishwa kugombea ni Derek Bryceson (jembe) na Ramadhani Kibugila (nyumba).

Wilaya ya Temeke ni Luteni Kanali Ali Mchumo (jembe) na Masudi Ali Masudi (nyumba).

Nafasi ya ubunge wa Taifa kutoka Mkoa wa Dar es Salaam, waliopitishwa ni Kijakazi Kyelula, Peter Macha na Peter Sao.

Mkoani Arusha, walikuwa Ole Saibul Alexander (nyumba) na Hubert Mbaga (jembe).

Arumeru walipitishwa Penieli Ole Saitabau (jembe) na Kivuyo Solomoni (nyumba). Wilaya ya Hanang walipitishwa Amri Ahmed (jembe) aliyepambanishwa na Mateo Qares (nyumba).

Siku mbili baadaye, Septemba 15 CCM iliteua majina mengine ya watu 25 kutoka jumuiya zake tano kugombea ubunge wa Taifa. Waligombea viti 15 vya Taifa vilivyotengwa kwa ajili ya jumuiya za Vijana, Washirika, Wazazi, Juwata na Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT).

Bunge la Jamhuri ya Muungano lilikuwa na viti 40 vya Taifa. Viti 25 kwa ajili ya mikoa na viti 15 kwa ajili ya Jumuiya za CCM.

Kufuatana na utaratibu, mbunge mmoja wa Taifa alichaguliwa kutoka kila mkoa.

Walioteuliwa kutoka UWT ni Babro Johanson, Getrude Mongela, Amina Feruzi, Mwanamkuu Makame na Bernadetta Kunambi.

Waliopitishwa kutoka Umoja wa Vijana ni Venance Ngula, Selemani Hamad, Nicholas Kuhanga, Anna Makinda na Luteni Kanali Makame Rashid.

Waliopitishwa kutoka Jumuiya ya Washirika ni Ndaki Ndaki, Nyambo Mwazavila, Benjamin Mkapa, Alfred Tandau na Mgeni Ally.

Kutoka Jumuiya ya Wazazi walikuwa Thabita Siwale, Gibson Mwaikambo, George Kahama, Ali Ali na Leader Stirling, na kutoka Juwata kulikuwa na Elias Mashasi, Hindu Lilla, Crispin Tungaraza, Mboni Cheka na Ismail Ismail.

Septemba 25 mjini Dar es Salaam mkutano mkuu wa CCM ulianza kikao chake katika Ukumbi wa Diamond Jubilee.

Huo ndio ulikuwa mkutano wa kwanza kwa CCM wa kuteua jina la mgombea pekee wa kiti cha urais tangu kilipoanzishwa Februari 5, 1977.

Miongoni mwa agenda za mkutano huo ilikuwa kuchagua mjumbe mmoja wa Halmashauri Kuu ya Taifa kutoka Kigoma kushika nafasi ya Alhaji Tawakal Karago ambaye mwaka 1979 CCM ilimnyang’anya uongozi na kumfukuza uanachama kutokana na utovu wa nidhamu.

Waliogombea nafasi hiyo walikuwa ni Damian Ruhinda, Peter Mayeye, Sheri Taki na Charles Rugiga.

Ruhinda aliibuka mshindi na kuwa mjumbe kutoka mkoa huo.

Katika mkutano huo, Mwalimu Nyerere pia aliteuliwa kuwa mgombea pekee wa urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.