Watu 78 kutoka Afrika Kusini wawekwa karantini katika mpaka wa Tunduma

Mkuu wa Mkoa wa Songwe Brigedia Jenerali Nicodemus Mwangela

Muktasari:

Idadi ya wasafiri waliowekwa karantini katika mji wa Tunduma Mkoa wa Songwe imeongezeka kutoka sita wiki iliyopita hadi kufikia 84.

Tunduma. Idadi ya wasafiri waliowekwa karantini katika mji wa Tunduma Mkoa wa Songwe imeongezeka kutoka sita wiki iliyopita hadi kufikia 84.

Wasafiri hao ambao walikuwa wanatoka Afrika ya Kusini, ambayo ni miongoni mwa nchi zenye maambukizi zaidi ya virusi vya corona Africa, walikuwa wakipita katika mpaka wa Tanzania na Zambia mjini Tunduma.

Miongoni mwao 55 ni Watanzania, 11 ni raia wa Afrika Kusini na 12 ni raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

Mkuu wa Mkoa wa Songwe Brigedia Jenerali Nicodemus Mwangela alisema hayo jana alipofanya ukaguzi wa maandalizi ya utayari wa kupambana na ugonjwa unaosababishwa na virusi vya corona kwa mkoa huo, hususani maeneo ya mipakani ya Ileje na Tunduma.

Mwangela alisema wasafiri hao walipoingia nchini kupitia mpaka wa Tunduma walipimwa na kukutwa hawana dalili za virusi vya corona lakini kwa kuwa wametoka katika nchi yenye maambukizi zaidi wametengwa katika karantini kwa ajili ya matazamio ya afya zao.

Alisema utaratibu huo ni kwaajili ya kuwaaangalia ndani ya siku 14 kama watakuwa hawana dalili za Covid-19 wataruhusiwa kuendelea na safari zao.

Mkuu huyo wa mkoa aliwaagiza viongozi katika sekta mbalimbali kuendelea kutoa elimu ya namna ya kujikinga na virusi vya corona na kuwa katika ofisi na taasisi zote usafi uzingatiwe, hasa suala la kunawa mikono kwa maji na sabuni kila mahali.

Aliliagiza Jeshi la Polisi Mkoa wa Songwe kufanya msako katika maeneno ya stendi za mabasi ili kubaini endapo kuna raia yeyote kutoka katika nchi zenye maambukizi zaidi ya Covid-19 ambao huenda wamepitia njia zisizo rasmi wawekwe karantini.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe, George Kyando alisema jeshi hilo limepiga marufuku mabasi kujaza abiria kuliko uwezo wa gari (level seat), kutokuwa na vitakasa mikono kwenye mabasi au maji na sabuni kwa ajili ya kunawa.

Pia ni marufuku ya mabasi kuanza safari bila kupuliziwa dawa.

Alisema atakayepuuzia marufuku hizo ambazo zimelenga kuweka tahadhari ya kutosambaza ugonjwa wa virusi vinavyosababisha corona atakuwa anataka kusambaza ugonjwa kwa makusudi, jambo ambalo ni kosa kisheria hivyo hatua kali zitachukuliwa dhidi yake.

Mganga Mkuu wa Mji wa Tunduma Dk Enock Mwambalaswa alisema wasafiri wote waliowekwa karantini wanapimwa mara mbili kwa siku ili kufuatilia maendeleo ya afya zao na endapo atatokea mwenye dalili za virusi vya hatua za haraka zitachukuliwa.

Alithibitisha kuwa hadi sasa wote wanaendelea vizuri na hakuna aliyebainika kuwa na viashiria vya ugonjwa huo.

Ugonjwa wa Covid-19 ulianzia China Desemba mwaka jana hadi sasa umesawapata watu 964,772 na kuua kati yao 49,246. Hapa nchini umewapata watu 20, umeua mmoja na wawili wamepona.