VIDEO: Askofu Mkuu, wenzake kortini wakituhumiwa kutapeli

Thursday May 9 2019

 

By Juma Mtanda, Mwananchi [email protected]

Morogoro. Askofu Mkuu wa Kanisa la Agape Wuema Sanctuary Ministry International Tanzania Ltd, Martin Gwila na wenzake wanne wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Wilaya ya Morogoro kwa shtaka la kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.

Viongozi wengine wa kanisa hilo waliopandishwa kizimbani leo Alhamisi Mei 9, 2019 ni Cedmon Sulutya, Mhasibu Onesmo Lumuliko maarufu Duma  na Apolinary Sodah.

Askofu huyo na wenzake wanadaiwa kutenda kosa hilo Januari 21, 2017 eneo la Mango Garden kata ya Nunge Manispaa ya Morogoro dhidi ya walalamikaji 219 wakiwamo wanajeshi wastaafu, polisi wastaafu  na mgambo walioahidiwa kupatiwa kazi ya ulinzi.

Akisoma hati ya mashtaka mbele ya Hakimu Mkazi Mahakama ya Wilaya ya Morogoro, Alisile Mwankejela, Wakili wa Serikali, Eulyane Ndunguru, ameiambia mahakama kuwa Januari 21, 2017 viongozi wa Agape walitenda kosa hilo.

Akitoa ushahidi wake mbele ya mahakama, Cosmas Ndongo (65) ameeleza kuwa Januari 21, 2017 eneo la Mango Garden Manispaa ya Morogoro viongozi wa Agape walitoa tangazo la kazi za ulinzi.

Ndongo amedai kuwa katika tangazo hilo lilieleza wanahitaji wawe wamepitia mafunzo ya kijeshi, polisi, JKT, kampuni za ulinzi au mgambo.

Advertisement

Alidai kila muombaji alitakiwa kujaza fomu na kupata kitabu cha mwongozo ambavyo alitakiwa kulika Sh 65,000; kitabu Sh5,000 na Sh60,000 ada ya uombaji na baada ya maombi kukubaliwa mshahara ungekuwa Sh100,000 kwa siku.

Shahidi wa pili katika kesi hiyo, Gabriel Mei amedai baada ya taratibu zote za kujaza fomu walisubiri  kupigiwa simu na wahusika ili kuanza kazi lakini ilikuwa kinyume chake, miezi mitatu baadaye walitoa taarifa kituo cha polisi.

Mtei ameendelea kuieleza mahakama kutokana na maelezo ya mshahara mnono wa Sh100,000 kwa  siku, kila mtu alivutiwa kuipata hiyo kazi.

Washtakiwa wanatetewa na Wakili Daudi Mkulya, huku ikiwa tayari mashahidi wanne wametoa ushahidi wao.

Kesi hiyo imeahirishwa hadi Mei 21, 2019 itakapoendelea.

 

Advertisement