KESI YA ZITTO: Mwenyekiti aieleza mahakama jinsi operesheni kuwaondoa wavamizi ilivyoanza

Wednesday August 14 2019

 

By Hadija Jumanne, Mwananchi. [email protected]

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Kijiji cha Mpeta wilayani Uvinza, mkoani Kigoma, Petro Salum(50) ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kuwa kabla ya kufanyika kwa operesheni ya kuwaondoa wavamizi waliovamia eneo la Ranchi ya Taifa (NARCO) iliyopo, wilayani humo, aliombwa eneo kwa ajili ya kuwaweka wananchi watakaotolewa katika hifadhi hiyo.

Shahidi huyo amedai  ombi hilo lilitolewa na Mkuu wa Wilaya ya Uvinza, mkoani Kigoma, ambaye hata hivyo hakumtaja jina lake mahakamani hapo.

Salum ambaye ni shahidi wa nane katika kesi ya uchochezi, inayomkabili Mbunge wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo), Zitto Kabwe ameieleza mahakama hiyo leo Jumatano Agosti 14, 2019  wakati akitoa ushahidi wake dhidi ya mshtakiwa huyo.

Akiongozwa na wakili wa Serikali Mkuu, Tumaini Kwema mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama hiyo, Huduma Shaidi, shahidi huyo amedai operesheni hiyo ilipangwa kufanyika wiki nzima katika eneo la Mwanduhubandu, katika kijiji cha Mpeta, kuanzia Oktoba 15 hadi 22, 2018.

 

Amedai kabla ya kuanza kwa kazi hiyo, mkuu wa wilaya ya Uvinza, ambaye hakumtaja jina, alienda kwa mwenyekiti huyo kuonana naye na kumuomba eneo kwa ajili ya kuwaweka wavamizi ambao watatolewa katika Ranchi hiyo.

Advertisement

 

"Nakumbuka kabla ya zoezi la kuwaondoa wavamizi katika eneo lile la Ranchi ya taifa, DC wa Uvinza alikuja kwangu na kuniomba eneo kwa ajili ya kuwaweka wale wananchi watakaoondolewa katika eneo la Ranchi" amedai Salum.

Salum amedai baada ya ombi hilo, alikutana na uongozi wa kijiji kwa ajili ya kujadili ombi hilo, ambapo eneo lilipatikana na kupimwa viwanja 400.

"Baada ya kupatikana eneo hilo, DC alikuja tena kwangu na kufanya mkutano na wananchi na kuwataka wahame katika Ranchi hiyo.”

“Hata hivyo, baadhi ya wavamizi hao waliondoka katika Ranchi hiyo na kupewa maeneo mapya katika vile viwanja 400 tulivyotenga" amedai mwenyekiti huyo ambaye yupo eneo hilo tangu 2004.

Amedai sababu ya wananchi hao kuhamishwa katika eneo hilo inatokana kuwa eneo hilo ni mali ya halmashauri na kwamba wananchi walienda kuweka makazi  yao katika Ranchi hiyo bila utaratibu wa kisheria.

Salumu amedai kijiji chake cha Mpeta kina wananchi zaidi ya 3,000 na kwamba Oktoba 15, 2018 kazi ya operesheni ilianza  katika eneo la Mwanduhubandu lililopo katika kijiji hicho.

Hata hivyo, siku hiyo ya kuanza kwa operesheni ya kuwaondoa wavamizi hao mwenyekiti huyo hakushiriki kazi hiyo, lakini Oktoba 18, 2018 alishiriki kazi hiyo na kutafuta miili ya askari polisi wawili na raia  mmoja.

Amedai  miili ya askari polisi wawili ambao waliwakuta katika eneo la Ranchi hiyo, Oktoba 19, 2018  ni Mkaguzi wa Polisi, Ramadhani Mdimi, koplo Mohamed Mgeza.

"Kama mwenyekiti wa kijiji nilipewa taarifa na mwananchi wangu aitwaye Deus Mapembe, kuwa mwanae Salum Deus haonekani, hivyo tulianza kumtafuta kwa kwenda katika gereza la Bangwe lililopo wilaya ya Kigoma, huko hatukumkuta tukaenda sehemu ya kuhifadhia maiti katika hospitali ya mkoa wa Kigoma ya Mawenzi, ambapo tuliukuta mwili wa Deus na kisha kuuchukua na kuupeleka nyumbani kwao kwa ajili ya mazishi," amedai shahidi.

Hata hivyo, shahidi huyo amedai watu waliokufa katika operesheni hiyo ni watu wanne na sio 100 kama ilivyodaiwa.

Endelea kufuatilia Mwananchi  kwa taarifa zaidi kuhusu kesi hii

Advertisement