VIDEO: Ali Kiba, Harmonize wapishana msiba wa Mbalamwezi wa kundi la The Mafik

Saturday August 17 2019

 

By Nasra Abdallah, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. “Wamepishana”. Ndivyo unavyoweza kusema baada ya wasanii wakali wa muziki wa Bongo Fleva nchini Tanzania, Ali Kiba na Harmonize kupishana katika msiba wa msanii Abdallah Matimbwa maarufu Mbalamwezi wa kundi la The Mafik.

Tukio hilo limetokea leo Jumamosi Agosti 17, 2019 katika msiba wa msanii huyo ambaye kwa mujibu wa rafiki zake alitoweka katika sikukuu ya Eid na siku nne baadaye polisi walitoa taarifa za kupatikana kwa mwili wake.

Katika msiba uliokuwa Tandika mtaa wa Mindu jijini Dar es Salaam, Ali kiba alifika saa sita mchana na saa moja baadaye Harmonize naye alifika eneo hilo, kuanza kusalimiana na wasanii mbalimbali.

Dakika chache baada ya msanii huyo wa kundi la WCB  kufika, Ali Kiba aliyekuwa ameketi na wasanii wengine akiwemo Fid Q alinyanyuka na kuaga wasanii wa kundi la The Mafik, Hamadai na Rhino King na kuondoka.

Harmonize baada ya kusalimiana na waliokuwa nje , aliingia ndani kuwapa pole wafiwa, kisha kuondoka akiwa anasindikizwa na walinzi.

Wasanii waliokuwepo katika msiba huo ni Barnaba, Sheta, Chege, Sam G, Chege, Dogo Aslay, na mtayarishaji wa  muziki Hanscana.

Advertisement

Mwili wa msanii huyo umezikwa leo saa 5 asubuhi katika makaburi ya Tamla.

 

Advertisement