Kelele maeneo ya makazi, Lugola awatangazia Ma OCD ‘ama zao ama zake’

Muktasari:

Waziri Kangi Lugola anayehusika na mambo ya ndani awatangazia ama zao ama zake wakuu wa polisi wa wilaya (OCD) nchini Tanzania watakaoshindwa kudhibiti kelele za muziki katika maeneo mbalimbali asema malalamiko yamekuwa mengi kila mahali.

Dar es Salaam. Waziri wa Mambo ya Ndani nchini Tanzania,  Kangi Lugola amewatangazia 'ama zao ama zake'  wakuu wa polisi wa wilaya (OCD) nchini humo watakaoshindwa kudhibiti kelele zinatokana na muziki wa baa, kumbi za starehe, klabu za usiku na baadhi ya taasisi za dini zisizofuata utaratibu.

Lugola ametoa msimamo huo leo Jumatatu Septemba 9, 2019 wakati alipotembelea baa ya Buscar la Vida iliyopo eneo la Mbezi Beach wilayani Kinondoni jijini Dar es Salaam.

Amesema amekuwa akipata malalamiko mara kwa mara ya kelele kutoka kwa wananchi na amebaini OCD wameshindwa kudhibiti kelele hizo kwa mujibu wa sheria ya jeshi hilo sura 322 kifungu cha 42 kinachotoa mamlaka kwa polisi kudhibiti kelele zinazotokana na muziki.

"Kuanzia nukta hii ninayoongea, ikitokea nimepigiwa simu na mwananchi kwamba kuna kelele za muziki eneo fulani huyo OCD ama zake ama zangu. Naomba nirudie kuna watu wanadhani ni mchezo nawaambia ama zao ama zangu kama wakishindwa kudhibiti.”

"Nataka JPM (Rais John Pombe Magufuli), akifumba na kufumbua  akute Watanzania wana roho safi na wameondokana na kero hii ya kelele iliyopo nchi nzima. Naziomba taasisi za dini zifuate utaratibu wa kuendesha ibada zao," amesema Lugola.

Mwanasheria wa Baraza la Taifa la Uhifadhi na Usimamizi wa Mazingira (Nemc), Manchare Heche amemuagiza mmiliki wa baa hiyo Celina Koka kuwasilisha nyaraka na vibali kwenye ofisi yao ili kujiridhisha kwa kuwa baa hiyo ipo kwenye makazi ya watu na shule.