Nchi wanachama wa SADC kujadili mabadiliko tabianchi

Muktasari:

Makatibu wakuu wa Mazingira, Maliasili na Utalii wa nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) wataweka mkakati wa pamoja wa  kubaliana na changamoto za mabadiliko ya tabia nchi  na ujangili katika nchi wanachama.

Arusha. Makatibu wakuu wa Mazingira, Maliasili na Utalii wa nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) wataweka mkakati wa pamoja wa  kubaliana na changamoto za mabadiliko ya tabia nchi  na ujangili katika nchi wanachama.

Hayo yameelezwa leo Jumatano Oktoba 23, 2019 na katibu mkuu ofisi ya makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Joseph Malongo katika mkutano wa sekta wa SADC mjini Arusha.

“Katika kikao hiki tunatarajia kuweka mkakati wa kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchini jinsi yanavyoathiri ongezeko la vimbunga lakini pia  kuingia kwa viumbe vamizi,” amesema.

Katibu mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii, Profesa Adolf Mkenda amesema wanatarajia kuzungumzia  vita dhidi ya ujangili, biashara ya wanyamapori na mkakati wa kukuza utalii katika nchi za SADC.

Amesema mkutano unaotarajiwa kuangalia mwenendo wa hali ya mazingira, mabadiliko ya tabianchi na  hali ya utalii na misitu katika nchi za jumuiya hiyo.

Naye naibu katibu mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dk Aloyce Nzuki amesema katika mkutano huo watajadili utekelezaji wa mikakati ya hifadhi na usimamizi wa mazingira.

Amesema mapendekezo ya mikutano na makatibu wakuu na watendaji wa sekta ya Maliasili, Utalii na Mazingira  yanatarajiwa kufikishwa katika mkutano wa  Mawaziri unatarajiwa kufunguliwa na makamu wa Rais,  Samia Suluhu Hassan Oktoba 25, 2019.

Nchi wanachama wa SADC ni Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Eswatini, Lesotho, Madagascar, Malawi, Mauritius, Msumbiji, Namibia, Shelisheli, Afrika Kusini, Tanzania, Zambia na Zimbabwe.