Mbowe ataja sababu kumteua Mnyika, Kigaila na Mwalimu

Muktasari:

Baraza Kuu la Chadema  limeidhinisha John Mnyika kuwa katibu mkuu na  Benson Kigaila, Salum Mwalimu kuwa naibu katibu mkuu baada ya kuteuliwa na mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe.

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe ametaja sababu ya kumteua Mbunge wa Kibamba, John Mnyika kuwa katibu mkuu wa chama hicho kuchukua nafasi ya Dk Vicent Mashinji.

Leo Ijumaa Desemba 20, 2019 saa 11 asubuhi katika ukumbi wa Mlimani City Dar es Salaam, Mbowe ametoa sababu hizo mbele ya wajumbe wa baraza kuu la chama hicho.

Mbali na Mnyika, Kiongozi huyo wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni  amemteua  Benson Kigaila kuwa naibu katibu mkuu Bara akichukua nafasi iliyoachwa na Mnyika huku Salum Mwalimu akiendelea na nafasi yake ya naibu katibu mkuu Zanzibar.

Tofauti na utaratibu wa awali, Mbowe amemtangaza John Heche kuwa mjumbe wa sekretarieti ya  kamati kuu ya chama hicho.

Akieleza sababu ya kumteua Mnyika amesema ni kutokana na mbunge huyo kukulia ndani ya chama hicho kikuu cha upinzani nchini Tanzania.

"Huyo mtu hajui, nasikitika hata kamati kuu haijui. Ninaowateua ni watu mnaowaamini, wamekulia ndani ya chama," amesema Mbowe.

 

Amesema amechagua viongozi madhubuti watakaoweza kupambana kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2020.

"Tuna kipindi kifupi sana kuelekea kwenye uchaguzi mkuu, hakuna kulala, tutafanya kazi usiku na mchana. Viongozi tutasumbuana kweli kweli. Tunahitaji kushinda Dola sio kushiriki uchaguzi," amesema Mbowe.

 

Huku akimtaja msajili msaidizi wa vyama vya siasa nchini Tanzania, Sisty Nyahoza aliyekuwepo kwenye mkutano huo, Mbowe amesema, "Hatuhitaji kupata kibali cha mtu. Sisty najua hilo jambo linakugusa. Sisi ni wanyeyekevu msitufanye kuwa wakorofi."

Akiwazungumzia Kigaila na Mwalimu, amesema ametambua mchango wa Mwalimu kwa kazi aliyofanya alipokuwa madarakani.

"Sijamteua Kigaila afikirie kuna sherehe za Fiesta. Kati ya sasa na uchaguzi sitaki kumwona makao makuu, Chadema ni msingi tunaimarisha."

"Mwalimu natambua mchango wake Zanzibar na Bara bado tunahitaji mchango wake," amesema Mbowe.

Kuhusu Heche amesema mbunge huyo aliyeangushwa kwenye uchaguzi wa mwenyekiti wa Kanda ya Serengeti bado ana mchango mkubwa kwenye  chama.

Kwenye uchaguzi wa Kanda ya Serengeti kulikuwa na ushindani mkali na Heche alishindwa na Esther Matiko.

"Matiko ataendelea na cheo chake, lakini bado tunatambua mchango wa Heche kwenye chama, " amesisitiza.

Awali, Mbowe amesema tangu amekuwa mwenyekiti hapendi kuteua majina mawili ili yapigiwe kura kwani kura hizo zinaweza kukipasua chama.

"Tusikigawe chama kwa makundi, gharama yake ni kubwa. Tusijaribu sumu kwa kuonja," amesema Mbowe huku akishangiliwa.