Makonda atamani Kigamboni kufanana na mji wa Manhattan

Muktasari:

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda leo Jumanne Februari 11, 2020  amemwomba ruhusa Rais  wa Tanzania, John Magufuli aweze kuifanya Wilaya ya Kigamboni kufanana na mji wa Manhattan uliopo jiji la New York, Marekani.

Dar es Salaam. Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda leo Jumanne Februari 11, 2020  amemwomba ruhusa Rais  wa Tanzania, John Magufuli aweze kuifanya Wilaya ya Kigamboni kufanana na mji wa Manhattan uliopo jiji la New York, Marekani.

Makonda ametoa kauli hiyo katika hafla ya uzinduzi wa jengo la manispaa ya Kigamboni na jengo la mkuu wa Wilaya ya Kigamboni hiyo eneo la Gezaulole Kigamboni.

Amesema alipoteuliwa kuwa mkuu wa Wilaya alikuta wilaya hiyo na Ubungo hazijapangwa vizuri.

“Niruhusu mheshimiwa Rais kupitia miradi ya maji, umeme, hospitali, barabara niifinyanye wilaya ya Kigamboni kuwa wilaya ya kisasa.”

“Tumetembea huko duniani tumeona. Ukienda pale Manhattan, New York City upande wa pili utakuta kuna kisiwa cha Jersey, kuna mambo mazuri. Haka ndio ka kisiwa ketu kawe na hoteli nzuri za kitalii, fukwe nzuri. Mtu akitaka kwenda kula maisha anasema ni Kigamboni hapana sehemu nyingine,” amesema Makonda.

Kuhusu viwanda kujengwa Kigamboni, Makonda amesema, “ndio maana tumesema ile barabara ikikamilika show room zote ziwe Kigamboni. Dubai pale wameanzisha mji wa magari, Japan wameanzisha mji wa magari. Sisi Afrika Mashariki na Afrika ya kati tukiweka mji wa magari  Kigamboni watu watatoka Afrika yote kununua magari,” amesema.