Mbowe: Ndani ya saa 72 Lissu atakuwa Rais, mimi Waziri mkuu Mungu akipenda

Sunday October 25 2020

Hai. Mwenyekiti wa Taifa wa Chadema, Freeman Mbowe, amesema ndani ya saa 72 zijazo, mgombea wao wa Urais, Tundu Lissu anakwenda kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mbowe ametoa kauli hiyo leo Jumapili Oktoba 25 katika mji mdogo wa Bomang'ombe wilaya ya Hai wakati akihutubia mkutano wa hadhara wa kampeni huku akisema Mungu akipenda, yeye anakwenda kuwa Waziri mkuu.

Hata hivyo, Mbowe ambaye pia  anagombea ubunge jimbo la Hai, alitahadharisha kuwa kitendo chochote cha kuwazuia mawakala wao 80,160 nchi nzima wasiingie kwenye vituo vya kupigia kura Oktoba 28, kunaweza kubadili historia ya Tanzania.

Hivyo, aliisihi Tume ya Taifa ya Uchaguzi na vyombo vya Usalama, kuhakikisha hakuna jaribio lolote la kuwazuia mawakala wao kuingia kwenye vituo kusimamia upigaji kura na wao watakuwa tayari kukubali matokeo kama uchaguzi utakuwa wa huru na haki.

 

"Uchaguzi huu sio kati ya Chadema na CCM wala uchaguzi huu sio kati ya Lissu na Magufuli (mgombea urais wa CCM) bali ni kati ya wanaopenda uhuru na haki na waliokandamiza uhuru na demokrasia," alisema Mbowe.

Advertisement

Mbowe amesema wamezunguka mikoa yote ya Tanzania na wananchi wapo tayari kufanya mabadiliko ya uongozi na kusisitiza kuwa kwa mwonekano na hamasa waliyoionyesha Watanzania, Lissu anakwenda kuwa Rais ndani ya saa 72 zijazo.

Hivyo, ameitaka NEC kuhakikisha uchaguzi huu hauvurugwi kwa namna yoyote kwa sababu gharama yake itakuwa kubwa na kusisitiza kuwa wako tayari kukubali kushindwa kama NEC na vyombo vingine vitahakikisha uchaguzi umekuwa wa wazi, huru na haki.

Advertisement