AAFP wataka vijana wakutanishwe kujipanga uchaguzi

Muktasari:

  • Mwenyekiti wa Taifa AAFP amesema chama hicho kitashindwa kwa asilimia 60 Serikali za Mitaa lakini kishindo cha ushindi kitakuwa mwakani

Dodoma. Chama cha Wakulima (AAFP) kimeomba Rais John Magufuli kuwakutanisha viongozi wa vijana kwa vyama vitakavyoshiriki uchaguzi wa Serikali za Mitaa ili kupunguza machafuko nchini.

Hata hivyo, AAFP wameahidi kuwa katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa watashinda kwa asilimia 60 huku wakisema kishindo kitakuwa uchaguzi wa mwakani.

Mwenyekiti wa Vijana Taifa wa AAFP, Magizeli Mwamele ametoa kauli hiyo leo Septemba 16,2019 akisema bila kuwapo jukwaa la pamoja, vijana watachapana makonde kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa na Uchaguzi Mkuu itakuwa ni tatizo kubwa.

 “Mtu pekee anayeweza kumaliza tatizo ni Rais John Magufuli, atuite wenyeviti wote kwa ngazi ya Taifa ili tuzungumze umuhimu wa amani na kukubaliana namna ya kuingia kwenye uchaguzi nasi tutawapa maelekezo vijana wetu,” amesema Mwamele.

Ametaja sababu za kuwaita viongozi wa vijana ni kutokana na mihemko waliyonayo ambayo bila kuzuiwa italeta tatizo huku akieleza kwamba baadhi ya wenyeviti wa vijana Taifa hawaivi jambo linalotoa tafsiri mbaya wakati wa matokeo.

Mwenyekiti wa AAFP Wilaya ya Mpwapwa, Sevelini Machila ameitaka Serikali kutotumia vyombo vya dola kuzuia demokrasi badala yake waachie uwanja huru kwa watu wote ili uwepo ushindani wa kweli.