ACT-Wazalendo wajipanga kupinga uteuzi wa mkurugenzi NEC mahakamani - VIDEO

Kiongozi wa Act Wazalendo, Zitto Kabwe akiwa na wakili wake, Jebra Kambole (wa pili kulia) wakitoka katika chumba cha mahakama kuu jijini Dar es Salaam jana, baada ya shauri la chama hicho kujiunga katika kesi ya kupinga ukomo wa uraisi kutajwa katika mahakama hiyo. Kesi hiyo imeahirishwa hadi tarehe 10 mwezi huu mwaka 2019, kutokana na mkulima Dezydelius Mgoya aliyefungua kesi hiyo kutokuwepo mahakamani hapo. Picha na Ericky Boniphace

Muktasari:

  • Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe amesema chama hicho kimemuagiza wakili, Jebra Kambole kuangalia misingi ya kisheria ili kufungua kesi ya kupinga uteuzi wa mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Dk Wilson Charles.

Dar es Salaam. Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe amesema chama hicho kimemuagiza wakili, Jebra Kambole kuangalia misingi ya kisheria ili kufungua kesi ya kupinga uteuzi wa mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Dk Wilson Charles.

Ametoa kauli hiyo leo Jumatano Septemba 2, 2019 muda mfupi baada ya kutoka kusikiliza kesi ya kupinga ukomo wa urais iliyofunguliwa na Dezydelius Mgoya ambayo chama hicho kimeomba kujumuishwa.

Akiwa katika viwanja vya Mahakama Kuu, Dar es Salaam Zitto amesema wameshangazwa na uamuzi wa Rais John Magufuli kumteua Charles aliyewahi kugombea ujumbe wa halmashauri kuu ya Taifa ya Chama cha Mapinduzi (NEC).

“Suala hili la wasimamizi wa uchaguzi ambao ni wanachama wa vyama vya siasa kuteuliwa lipo mahakamani, kuna kesi imefunguliwa na Bob Wangwe na wanasheria pamoja na wanaharakati.”

“Mahakama ikatoa amri kwamba  wasimamizi wa uchaguzi hawapaswi kuwa wanachama, makada au mashabiki  wa vyama vya siasa,” amesema Zitto.

Amesema kitendo cha kuteuliwa kwa Wilson ni dharau kwa mahakama ambayo imeshatoa uamuzi kuwa hawapaswi kusimamia uchaguzi.

Amebainisha kuwa kulingana na suala hilo kuwa muhimu, wanashauriana na vyama vingine vya siasa kwa ajili ya kuchukua hatua za kisheria kuzuia uteuzi huo.

“Tumeshamuagiza Kambole atazame misingi ya kisheria ili kuhakikisha tunazuia uteuzi. Tunahitaji uchaguzi huru tunaangalia namna bora ya kuweza kuchukua hatua za kisheria.”

“Tunataka wakili atazame jambo hili kulingana na uamuzi wa mahakama katika kesi ya awali (ambayo Serikali ilikata rufaa) na sasa tunasubiri uamuzi wa rufani ili kuhakikisha tunazuia uteuzi wa wanasiasa kusimamia uchaguzi,” amesema Zitto.