VIDEO: Abdul Nondo ajitosa kuwania uongozi ACT-Wazalendo

Muktasari:

  • Aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa Mtandao wa Wanafunzi wa Vyuo Vikuu Tanzania (TSNP) amejitosa kuwania uenyekiti wa ngome ya vijana wa chama cha siasa cha upinzani nchini Tanzania cha ACT-Wazalendo.

Dar es Salaam. Mwanachama wa Chama cha ACT Wazalendo, Abdu Nondo amesema chama hicho kinaitaji Mwenyekiti wa Ngome ya Vijana atakaeunganisha nguvu ndani na nje ya chama hicho.

Nondo ameyasema hayo leo Ijumaa Februari 21, 2020 wakati akizungumza na waandishi wa habari baada ya kukabidhiwa fomu yakugombea nafasi ya Mwenyekiti wa Ngome hiyo Taifa.

Amesema chama tawala CCM kikirusha mishale hakirushi kwa chama hicho pekee bali kinatupa mishale kwa vyama vyote vya upinzani nchini Tanzania.

“Tunaitajia mwenyekiti wa vijana ambaye ataona umuhimu wakuunganisha nguvu sio ndani ya chama chetu hata nje ya chama, Serikali na CCM ikirusha mishale yake inatupa kwa Chadema, NCCR-Mageuzi na upinzani kwa ujumla,” amesema Nondo

Amesema chama hicho lazima kipate mwenyekiti wa vijana ambaye atawiwa kuunganisha nguvu ndani ya chama chetu, kuunganisha vijana kutoka vyama vingine ili kuwa pamoja na kuweza kustahimili mishale itayopigwa na chama tawala.

“Hii itatusaidia sana kuimarisha demokrasi, kuimarisha maslahi ya vijana, kupigania maendeleo ya nchi yetu na kuzidisha uzalendo wa hali ya juu katika Taifa letu,”amesema

Nondo aliyewahi kuwa mwenyekiti wa Mtandao wa Wanafunzi wa Vyuo Vikuu Tanzania (TSNP) amesema chama hicho kinahitaji mwenyekiti wa vijana atakayetambua hujuma dhidi ya chama hicho hasa kwa viongozi.

Amesema chama hicho kinahitaji kijana atakayekuwa tayari kuunganisha vijana, kulinda chama, viongozi wa chama na mfumo wa vyama vingi nchini,” amesema