VIDEO: Ajali ilivyoua baba na mama, watoto wao watatu wakanusurika

Morogoro. Ni huzuni na bahati. Ndivyo unavyoweza kusema baada ya simulizi kuhusu Yonusi Baraka, mwenye umri wa miaka sita, Grace Baraka (2) na mdogo wao, Yoelina walionusurika katika ajali iliyochukua maisha ya wazazi wao.

Safari ya kumpeleka mmoja wa watoto kwenda kuanza shule Gairo, imekatisha maisha ya wazazi na kuweka wingu katika masomo ya ndugu hao watatu wa familia hiyo.

Ilikuwa ni katika mchepuko wa daraja la Kiyegea wilayani Kilosa ambako lori lililogonga gari aina ya Toyota Noah lililokuwa na abiria zaidi ya 10, lilikatisha maisha ya Baraka Chimbedelele na Holipa Patrick na abiria wengine watatu.

Lakini watoto hao walinusurika kifo na badala yake walipata majeraha na kulazwa Hospitali ya Mkoa wakitoka Hospitali ya Mtakatifu Joseph iliyopo Dumila ambako walipelekwa mara baada ya ajali.

Jana Grace aliruhusiwa kurejea nyumbani, huku Yonusi aliyeumia zaidi kichwani, akiendelea na matibabu. Yoelina ambaye ni kichanga hakupata majeraha yoyote.

Miili ya wazazi wao, ilizikwa juzi.

Safari ililenga kumpeleka Yonusi kuanza masomo na kusalimia, lakini sasa suala la masomo yake na matunzo yao litategemea jinsi familia itakavyojipanga.

“Bado hatujaamua wataishi wapi, lakini tutapanga baada ya matibabu yao na kurejea nyumbani,” alisema Tangasi.

Akizungumza na Mwananchi hospitalini, Victoria Tangasi ambaye ni dada wa Holipa alisema walipata taarifa ya vifo Jumatatu na walipofuatilia walifahamishwa maiti zipo Hospitali ya Dumila.

Tangasi alisema walikuwa wanawasiliana na mdogo wake pamoja na shemeji yake tangu wanaanza kwa safari yao Morogoro.

Alisema siku ya ajali walipiga simu kueleza kuwa wanakwenda Gairo kusalimia.

Alisema ilipofika saa 12:00 jioni simu zao zilikuwa hazipatikani na hata walipotuma ujumbe mfupi kufahamu wamefika wapi, hawakujibiwa.

“Tukadhani wameahirisha safari,” alisema.

Alisema baada ya kukosa mawasiliano nao, siku iliyofuata asubuhi wakaendelea na kazi nyingine, lakini majira ya saa 5:00 asubuhi walipata taarifa za ajali.

Victoria alisema katika eneo la Dumila kuna ndugu alimpigia simu ili kwenda Hospitali ya St Joseph kuangalia majeruhi na miili ya marehemu.

“Niliangalia majeruhi sikuwatambua ila nilipoonyeshwa maiti, ndipo nikawatambua Holipa na Baraka,” alisema.

“Nilipofika hospitali mtoto alikuwa analia sana, tulimchukua na kumpeleka nyumbani. Kadi ya kliniki ya Noelina pia ilitusaidia kuwatambua kwa haraka. Nilifika hapa jana (juzi) kwa ajili ya kuwahudumia watoto hawa.”

Muuguzi kiongozi wa wodi waliyolazwa watoto hao, Zaituni Pwetete alisema Yonusi alipata majeraha kichwani.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Wilbroad Mutafungwa alisema bado wanamtafuta dereva wa lori lililosababisha ajali hiyo, Said Kifaila (30) na ameomba yeyote atakayemuona atoe taarifa polisi.