Akamatwa kwa madai ya kuchapisha taarifa za uongo kuhusu corona Kilimanjaro

Moshi. Jeshi la Polisi Mkoa wa Kilimanjaro linamshikilia Afrikana Mlay kwa kutuhumiwa kuchapisha na kusambaza taarifa za uongo mtandaoni kuhusiana na ugonjwa wa corona.


Kaimu kamanda wa polisi Mkoa wa Kilimanjaro, James Manyama amesema kuwa Aprili 4, 2020 kada huyo alichapisha taarifa inayokinzana na takwimu za wagonjwa ambazo zinatolewa na Wizara ya Afya kwenye mitandao ya kijamii ya Instagram, What's App na Twitter.


Nukuu ya taarifa hiyo iliyosambazwa na kada huyo kwenye mitandao ya kijamii ni ''Ni kwa nini Serikali ya Tanzania inaficha sana takwimu za ugonjwa wa corona? kumekuwa na usiri mkubwa mno wa ugonjwa huu wa corona...ukweli uliopo mpaka sasa Tanzania kuna wagonjwa 200+wa corona na mpaka sasa waliokufa na corona ni wagonjwa wanne na hii yote imefanywa siri ya serikali na idara zake za takwimu.''


Kamanda Manyama amesema taarifa hizo zililenga kupotosha jamii juu ya ugonjwa huo hatari na pia kufifisha juhudi kubwa zinazofanywa na Serikali katika kupambana na ugonjwa huo.


''Upelelezi wa shauri hili umekamilika na tunatarajia kumfikisha mahakamani mara moja,''amesema Kamanda Manyama.


Kamanda Manyama alitoa rai kwa wananchi wote kuwa jambo lolote ambalo hawana uhakika nalo wasitume kwenye mitandao wajizuie kufanya hivyo ili waepuke kuingia kwenye mikono ya sheria.


''Jeshi la polisi liko macho kwenye maeneo yote hadi huko kwenye mitandao, lolote utakalolifanya kinyume na sheria utawajibika nalo kisheria na hatutakuwa na huruma kwa yeyote yule,'' amesema Manyama.