Ali Mufuruki ashauri Tanzania kuridhia soko huru la Afrika

Mwenyekiti na Ofisa Mtendaji mkuu wa kampuni ya Infotech investment Group, Ali Mfuruki

Muktasari:

Wakati Serikali ikiendelea na tafakari kabla ya kuridhia mkataba wa soko la pamoja la biashara Afrika (AfCFTA) ambao iliusaini Julai 2018, wafanyabiashara nchini wamesema inapaswa kuridhia upesi ili Wataanzania waanze kujiandaa na namna watakavyonufaika na soko hilo.

Dar es Salaam. Wafanyabiashara nchini Tanzania wamesema Serikali haina budi kuridhia mkataba wa soko huru la Afrika (AfCFTA) pamoja na kufanya kampeni maalumu ya kuwaelewesha Watanzania juu ya fursa wanazoweza kuzipata kupitia mkataba huo.

Leo Alhamisi Septemba 12, 2019 Taasisi ya Sekta binafsi Tanzania (TPSF) iliandaa mkutano na wafanyabiashara kujadili mustakabali wa Tanzania kuelekea AfCFTA na namna Tanzania inavyopaswa kujiandaa na soko hilo ambapo kwa pamoja wafanyabiashara waliohudhuria wamesema soko lina fursa nyingi kuliko hasara.

Mwenyekiti na Ofisa Mtendaji mkuu wa kampuni ya Infotech investment Group, Ali Mfuruki ambaye alikuwa mtoa mada katika mkutano huo amesema Tanzania haina budi kuridhia mkataba huo bila hofu kwani kuna nchi kubwa na ndogo ambazo tayari zimeridhia na nyingine zinaendelea.

“Mwaka jana Tanzania na nchi nyingine 44 za Afrika zilisaini mkataba huo lakini nchi chache ziliridhia, kwa Afrika Mashariki bado Tanzania na Burundi, wafanyabiashara tunapaswa kusukuma hili kuhakikisha Tanzania nayo inaridhia ili wengine watakapoanza mwakani nasi tuweze kunufaika na soko hilo kubwa lenye watu zaidi ya bilioni 1.2,” amesema Mfuruku ambaye amekuwa akihudhuria mikutano kadhaa ya kikanda kuelekea kuanza kwa soko hilo.

Amesema ni muhimu kuridhia na kujiandaa kwani bila kujiandaa mkataba huu utazinufaisha nchi zilizo tayari tu na Watanzania wafahamu kuwa biashara ni kuvuka mipaka na mkataba huu unaleta urahisi wa kuvuka mipata.

Mufuruki amesema Afrika inaweza kuendelea kwa kufanya ushirika ili sehemu kubwa ya biashara katika bara hili ibaki Afrika.

“Ushirika siku zote ni kwa watu wasio lingana hivyo hakuna haja ya kuogopa kushirikiana kwa kigezo cha nchi kutolingana kiuchumi, ‘Its ok to step back but not to hold back’,”

Katika mkutano huo, Mkurugenzi Mtendaji wa TPSF, Godfrey Simbeye amesema hata Tanzania isiporidhia Julai 2020 soko hilo litaanza na hakuna mbadala wa kutojiunga kama nchi nyingi zitakuwa tayari zimejiunga hivyo ni vyema nasi tukajiunga haraka.

“Manufaa ni makubwa biashara siku zote inakuzwa na soko, kama tunaweza kufanya biashara katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo kusini mwa Afrika (Sadc) wigo wa soko likipanuka zaidi nasi tutatuza zaidi,” amesema Simbeye.