Alichokisema Zitto kuhusu Sumaye kung’oka Chadema

Muktasari:

Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe amesema hawajafanya mazungumzo yoyote na waziri mkuu mstaafu, Frederick Sumaye ambaye leo mchana Jumatano Desemba 4, 2019 ametangaza kuwa si mwanachama wa Chadema.

Dar es Salaam. Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe amesema hawajafanya mazungumzo yoyote na waziri mkuu mstaafu, Frederick Sumaye ambaye leo mchana Jumatano Desemba 4, 2019 ametangaza kuwa si mwanachama wa Chadema.

Zitto ametoa maelezo hayo saa chache baada ya Sumaye kumaliza kuzungumza na waandishi wa habari na kueleza sababu za kujiondoa Chadema, moja ikiwa ni hali ya sintofahamu iliyoibuka katika uchaguzi wa uenyekiti Kanda ya Pwani ambao alipigiwa kura 48 za hapana kati ya 76.

Katika maelezo yake ya leo, Sumaye aliyekuwa waziri mkuu mwaka 1995 hadi 2005 alieleza kuwa hana mpango wa kuhamia ACT-Wazalendo, wala chama chochote cha siasa na atabaki kuwa mshauri asiye na upande.

Katika ukurasa wa mtandao wake wa kijamii wa Twitter, Zitto amesema, “nipo mahakamani tangu asubuhi mpaka sasa nikiendelea na kesi ya uchochezi dhidi yangu. Ninasikia tumetajwa tajwa kuhusu Mzee Sumaye. Itoshe kusema kuwa chama cha ACT hakina mazungumzo yeyote na waziri mkuu huyo mstaafu. Nashauri apewe nafasi ya kupumzika kama alivyoomba.”

Amesema chama hicho kimehuzunishwa na Sumaye kuondoka katika chama cha upinzani cha Chadema.

“Sisi kama chama tumehuzunishwa na uamuzi wa Mzee Sumaye kupumzika siasa. Ilikuwa ni tunu katika upinzani kuwa na waziri mkuu mstaafu katika ngazi zake za uongozi. Bila shaka tutachota maarifa na uzoefu wake kama mwenyewe alivyoruhusu. Chama chetu kinaheshimu na kuthamini wastaafu,” amesema Zitto.

Ameongeza, “kwa upande wangu nawatakia kila la kheri wenzetu wa Chadema katika uchaguzi wao unaoendelea. Dhamira yetu ya kuunganisha nguvu ya vyama vya upinzani ili kukabiliana na CCM haina mashaka. Mara baada ya uchaguzi wa wenzetu tutaendelea na mazungumzo ya ushirikiano na uongozi mpya.”